Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Read the New Testament in 24 Weeks

A reading plan that walks through the entire New Testament in 24 weeks of daily readings.
Duration: 168 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
2 Timotheo 3-4

Watu Wengi Wataacha Kumpenda Mungu

Kumbuka hili: Katika siku za mwisho nyakati ngumu zitakuja. Watu watajipenda wenyewe na kupenda fedha. Watakuwa na majivuno na wenye jeuri. Watawatukana wengine kwa matusi. Hawatawatii wazazi wao. Watakuwa wasio na shukrani. Watapinga kila kinachompendeza Mungu. Hawatakuwa na upendo kwa wengine na hawatakubali kuwasamehe wengine. Watawasingizia wengine na hawataweza kujizuia. Watakuwa wakatili na watayachukia yaliyo mema. Watu watawasaliti rafiki zao. Watafanya mambo ya kipuuzi bila kufikiri na watajisifu wenyewe. Badala ya kumpenda Mungu watapenda starehe. Watajifanya kuwa wanamheshimu Mungu, lakini watazikana nguvu za uzima ambazo ndizo zinazotuwezesha kwa hakika kumpa utukufu na kumpendeza. Ukae mbali na watu wa jinsi hiyo.

Nasema hivi kwa sababu baadhi yao wanaziendea nyumba na kuwateka wanawake dhaifu, waliolemewa na dhambi na kuvutwa na kila aina ya tamaa. Wanawake hawa nyakati zote wanataka kujifunza, lakini hawawezi kamwe kuufikia ufahamu wote wa kweli. Kama ambavyo Yane na Yambre[a] walivyompinga Musa, ndivyo hata watu hawa wanavyoipinga kweli. Ni watu ambao akili zao zimeharibika, nao wameshindwa kuifuata imani. Lakini hawataendelea mbele zaidi, kwa sababu upumbavu wao utadhihirika wazi wazi kwa watu wote, kama ujinga wa Yane na Yambre ulivyojulikana.

Maelekezo ya Mwisho

10 Ninyi hata hivyo mmeyazingatia na kuyashika mafundisho yangu, mwenendo wangu na kusudi langu katika maisha, imani yangu, uvumilivu wangu, upendo wangu na ustahimilivu wangu, 11 mateso yangu na taabu zangu. Mnayajua mambo yaliyonitokea kule Antiokia, Ikonia, na Listra, mateso ya kutisha niliyoyastahimili! Lakini Bwana akaniokoa kutoka katika hayo yote. 12 Kwa hakika wote wanaoishi maisha yenye kumtukuza Mungu kama wafuasi wa Kristo Yesu watasumbuliwa. 13 Lakini watu waovu na wanaodanganya wengine wataendelea kuwa wabaya zaidi. Watawadaganya wengine na wao pia watajidanganya wenyewe.

14 Lakini imekupasa wewe kuendelea kuyashika mambo yale uliyojifunza na kuyathibitisha moyoni mwako kuwa ni ya kweli. Wewe unawajua na unawaamini wale waliokufundisha. 15 Na unajua kwamba umeyajua Maandiko Matakatifu tangu ukiwa mtoto. Maandiko hayo yana uwezo wa kukupa hekima. Hekima hiyo itakuongoza hadi kwenye wokovu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. 16 Maandiko yote tumepewa na Mungu. Na maandiko yote yanafaa kwa mafundisho kwa kusudi la kuwaonesha watu makosa yao na kuwafundisha njia sahihi ya kuishi 17 ili mtu anayemtumikia Mungu aweze kuandaliwa na kukamilishwa kwa ajili ya kufanya kila kazi njema.

Nakuamuru mbele za Mungu na mbele za Kristo Yesu, ambaye punde atawahukumu wale walio hai na wale waliokwisha kufa na juu ya kuja kwa mara ya pili kwa Kristo kwa sababu kwa hakika atatokea kuja kutawala kama Mfalme: Hubiri Ujumbe, uwe tayari kutimiza wajibu wako wakati ulio sahihi hata ule usio sahihi. Wathibitishie watu kwa wanafanya makosa na uwaonye juu ya yale yatakayowatokea. Ufanye hivi kwa subira kubwa na tahadhari katika yale unayofundisha.

Nasema hivi kwa sababu utakuja wakati ambapo watu hawatakuwa tayari kuyasikiliza mafundisho yenye uzima. Badala yake watawatafuta walimu wanaowapendeza. Watawatafuta walimu wanaosema yale wanayotaka kusikia. Na watayageuzia mbali masikio yao kutoka kwenye kweli na kugeukia simulizi za uongo. Lakini wewe ujizuie mwenyewe katika mambo yote; vumilia mateso; fanya kazi ya mhubiri wa Habari Njema; ifanye huduma uliyopewa na Mungu.

Kwangu mimi, nimemiminwa kama kinywaji cha sadaka, na wakati wa kuondoka kwangu kutoka katika maisha haya umekwisha kufika. Nimejihusisha katika mashindano ya thamani; nimemaliza mbio; nimeilinda imani. Sasa tuzo ya mshindi inaningoja, hii ni taji inatolewa kwa wenye haki. Bwana, aliye hakimu wa haki atanipa taji hiyo katika Siku ile. Ndio atanipa mimi na yeyote mwingine anayengojea kwa dhati kuja kwake.

Maelezo Binafsi

Jitahidi kuja kuniona mapema uwezavyo, 10 kwani Dema aliniacha kwa sababu aliupenda ulimwengu wa sasa na ameenda Thesalonike. Kreske ameenda Galatia, na Tito ameenda Dalmatia. 11 Luka ni peke yake aliyebaki nami. Mchukue Marko na uje naye utakapokuja, kwa sababu anaweza kunisaidia katika kazi yangu. 12 Namtuma Tikiko kule Efeso.

13 Utakapokuja njoo na koti nililoliacha katika nyumba ya Karpo kule Troa. Pia uniletee vitabu vyangu, hasa vile vya ngozi.

14 Iskanda aliye mfua vyuma amenitendea mabaya mengi. Bwana atamlipa kwa yale aliyotenda. 15 Wewe pia uwe mwangalifu kwake, kwa kuwa ameyapinga kwa juhudi mafundisho yetu.

16 Mara ya kwanza nilipokuwa nafanya utetezi wangu, hakuna hata mmoja aliyekuja kunisaidia. Badala yake wote wakaniacha. Na wasihesabiwe hayo na Mungu. 17 Lakini Bwana akasimama upande wangu na kunitia nguvu, ili ujumbe uweze kunenwa nami kwa ukamilifu ili kwamba Mataifa wote waweze kusikia. Na nikaokolewa kutoka katika mdomo wa simba. 18 Bwana ataniokoa kutokana na kila mashambulizi maovu na atanileta salama katika Ufalme wake wa mbinguni. Utukufu uwe wake milele na milele. Amina.

Salamu za Mwisho

19 Msalimu Priska na Akila na wale wa nyumbani mwake Onesiforo. 20 Erasto alibaki Korintho. Nilimwacha Trofimo kule Mileto kwa sababu alikuwa mgonjwa. 21 Jitahidi kuja kabla ya msimu wa baridi.

Ebulo anakusalimu, na Pude, Lino, na Klaudia, na ndugu na dada wote.

22 Bwana awe nawe. Neema ya Mungu iwe nanyi.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International