Read the New Testament in 24 Weeks
Maisha Yanayompendeza Mungu
4 Kaka na dada zangu sasa nina mambo mengine ya kuwaambia. Tuliwafundisha namna ya kuishi maisha yanayompendeza Mungu. Nanyi mnaishi hivyo. Na sasa tunawaomba na kuwatia moyo katika Bwana Yesu kuishi zaidi na zaidi katika njia hiyo. 2 Mnafahamu yote tuliyowaamuru kufanya kwa mamlaka ya Bwana Yesu Kristo. 3 Mungu anawataka muwe watakatifu. Anawataka mkae mbali na dhambi za zinaa. 4 Mungu anawataka kila mmoja wenu ajifunze kuuthibiti mwili wake mwenyewe. Tumieni miili yenu kwa namna iliyo takatifu na yenye heshima.[a] 5 Msiruhusu tamaa za mwili kuwatawala kama watu wasiomjua Mungu. 6 Msimtendee vibaya ndugu aliye mwamini wala kuwadanganya katika hili. Bwana atawahukumu watendao hivyo. Tumekwisha kuwaambia juu ya hili na kuwaonya. 7 Mungu alituita kuwa watakatifu na safi. 8 Hivyo kila anayekataa kuyatii mafundisho haya anakataa kumtii Mungu, siyo wanadamu. Na Mungu ndiye anayewapa ninyi Roho Mtakatifu.
9 Hatuna haja ya kuwaandikia juu ya kuwa na upendo kwa katika Kristo. Mungu amekwisha kuwafundisha kupendana ninyi kwa ninyi. 10 Ukweli ni kuwa, mnawapenda wanaoamini wote walioko Makedonia. Tunawatia moyo sasa, kuuonyesha upendo wenu zaidi na zaidi.
11 Fanyeni kila mnaloweza kuishi maisha ya amani. Mjishugulishe na mambo yenu wenyewe, na mfanye kazi kwa mikono yenu wenyewe,[b] kama tulivyowaambia mwanzo. 12 Mkifanya mambo haya, ndipo wale wasioamini wataheshimu namna mnavyoishi. Na hamtawategemea wengine.
Kuja Kwa Bwana
13 Kaka na dada, tunawataka mfahamu habari za wale waliokufa. Hatupendi muwe na huzuni kama watu wengine wasio na matumaini. 14 Tunaamini kuwa Yesu alikufa, ila tunaamini pia kuwa alifufuka. Hivyo tunaamini kuwa Mungu atawaleta katika uzima kupitia Yesu kila aliyekufa na kukusanywa pamoja naye.
15 Tunalowaambia sasa ni ujumbe wake Bwana. Sisi ambao bado tu hai Bwana ajapo tena tutaungana nae, lakini hatutawatangulia wale waliokwisha kufa. 16 Bwana mwenyewe atakuja kutoka mbinguni pamoja na sauti kuu yenye agizo, na sauti kubwa kutoka kwa malaika mkuu, na ishara ya Mungu ya mlio wa tarumbeta. Na watu waliokufa walio wake Kristo watafufuliwa kwanza. 17 Baada ya hayo, sisi ambao bado tungali hai mpaka wakati huo tutakusanywa pamoja na wale waliokwisha kufa. Tutachukuliwa juu mawinguni na kukutana na Bwana angani. Na tutakuwa na Bwana milele. 18 Hivyo tianeni moyo ninyi kwa ninyi kwa maneno haya.
Uwe tayari kwa ujio wa Bwana
5 Na sasa ndugu zangu, hatuna haja ya kuwaandikia juu ya nyakati na tarehe. 2 Ninyi mnafahamu vizuri kuwa siku ambayo Bwana atakuja itakuwa ya kushitukiza, kama mwizi anavyokuja usiku. 3 Watu watasema, “tuna amani na tuko salama.” Wakati huo ndipo uharibifu utakapowajia haraka, kama maumivu anayoyapata mwanamke anapojifungua. Na watu hao hawataweza kukwepa.
4 Lakini ninyi ndugu zangu, hamuishi katika giza. Na hivyo ile siku haitawashangaza kama mwivi. 5 Nyote ni watu wa nuru. Ni watu wa mchana. Hatuko katika usiku wala giza. 6 Hivyo tusiwe kama watu wengine. Tusiwe wasinziao. Tuwe macho na wenye kiasi. 7 Watu walalao, hulala usiku. Watu wanywao kupita kiasi, hunywa usiku. 8 Bali sisi ni watu wa mchana, hivyo tujitawale wenyewe. Tuvae imani na upendo vitulinde. Na tumaini la wokovu liwe kwetu kama kofia ya vita.
9 Mungu hakutuchagua tuangamie katika hasira yake. Mungu alituchagua tuwe na wokovu katika Bwana wetu Yesu Kristo. 10 Yesu alikufa kwa ajili yetu ili tuishi pamoja nae. Haijalishi kama tu hai au wafu atakapokuja. 11 Hivyo farijianeni ninyi kwa ninyi na msaidiane kukua imara katika imani, kama mnavyofanya sasa.
Maagizo ya Mwisho na Salamu
12 Tunawaomba mwatambue wale wanaofanya kazi kwa bidii miongoni mwenu, wale ambao, kama wafuasi wa Bwana, wanatumika kama viongozi wenu na kuwafundisha namna ya kuishi. 13 Wapeni heshima ya hali ya juu na upendo kwa sababu ya kazi wanayofanya.
Ishini kwa amani kila mmoja na mwenzake. 14 Tunawasihi, kuwaonya wale wanaokataa kuishi kwa kuwajibika.[c] Watieni moyo wanaoogopa. Wasaidieni walio dhaifu. Mvumilieni kila mmoja. 15 Asiwepo anae jaribu kulipiza baya kwa baya. Lakini kila mara mfanye lililo jema kwa kila mmoja wenu na kwa watu wote.
16 Mwe na furaha daima. 17 Msiache kuomba. 18 Shukuruni kwa kila jambo. Hivi ndivyo Mungu anavyotutaka tuishi katika Kristo Yesu.
19 Msiizimishe kazi ya Roho Mtakatifu. 20 Msiuchukulie unabii kama kitu kisicho cha muhimu. 21 Lakini pimeni kila kitu. Lishikeni lililo jema, 22 na mkae mbali na kila aina ya ovu.
23 Tunaomba kwamba Mungu mwenyewe, Mungu wa amani, atawafanya muwe watakatifu mkiwa wake. Tunaomba kwamba katika roho yote, nafsi yote, na mwili mzima mtahifadhiwa salama pasipo lawama Bwana wetu Yesu Kristo atakapokuja. 24 Yeye awaitae atawatendea haya. Mnaweza kumtumainia.
25 Kaka na dada zangu, tafadhali mtuombee. 26 Wasalimuni ndugu wote kwa salamu maalum ya watu wa Mungu.[d] 27 Ninawaagiza kwa mamlaka ya Bwana kuusoma walaka huu kwa waamini wote huko. 28 Neema ya Bwana wetu Yesu kristo iwe nanyi nyote.
© 2017 Bible League International