Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Read the New Testament in 24 Weeks

A reading plan that walks through the entire New Testament in 24 weeks of daily readings.
Duration: 168 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Wakolosai 3-4

Uhai Wenu Mpya

Mlifufuka pamoja na Kristo kutoka kwa wafu. Hivyo ishini maisha mapya, mkiyatazamia yaliyo mbinguni, ambako Kristo ameketi mkono wa kulia wa Mungu. Msiyafikirie yaliyo hapa duniani bali yaliyo mbinguni. Utu wenu wa kwanza umekufa, na utu wenu mpya umetunzwa na Kristo katika Mungu. Kristo ndiye utu wenu mpya sasa, na atakaporudi mtashiriki katika utukufu wake.

Kwa hiyo kiueni chochote kilicho cha kidunia kilichomo ndani yenu: uasherati, matendo machafu, mawazo na tamaa mbaya. Msijitakie na kujikusanyia vitu vingi, kwani ni sawa na kuabudu mungu wa uongo. Mungu ataionyesha hasira yake kwa wale wasiomtii,[a] kwa sababu ya maovu wanayotenda. Ninyi pia mlifanya maovu haya huko nyuma, mlipoishi kama wao.

Lakini sasa, jitengeni mbali na mambo haya katika maisha yenu: hasira, ukorofi, chuki, na mazungumzo yenye matusi. Msiambiane uongo ninyi kwa ninyi. Ninyi mmeyavua mavazi ya kale; utu wa kale mliokuwa nao na matendo mabaya mliyotenda hapo awali. 10 Na sasa mmevaa utu mpya unaofanywa upya kila siku hata kuufikia ufahamu kamili wa Kristo. Mfano wenu wa maisha mapya ni Kristo, aliye mfano na sura ya Mungu aliyewaumba ninyi. 11 Katika utu huu mpya haijalishi ikiwa wewe ni Myunani au Myahudi, umetahiriwa au hujatahiriwa. Haijalishi pia ikiwa unazungumza lugha tofauti au hata kama wewe ni mtu asiyestaarabika,[b] ikiwa ni mtumwa ama mtu huru. Kristo ndiye wa muhimu zaidi, naye yumo ndani yenu ninyi nyote.

Uhai Wenu Mpya Miongoni Mwenu

12 Mungu amewachagua na kuwafanya ninyi kuwa watu wake walio watakatifu. Anawapenda. Hivyo, jivikeni matendo haya na muwe na huruma: wema, wanyenyekevu, wapole na wenye subira. 13 Msikasirikiane, bali msameheane. Mtu yeyote akikukosea, msamehe. Wasameheni wengine kwa sababu Bwana amewasamehe ninyi. 14 Pamoja na haya yote, vaeni upendo. Upendo ndicho kitu kinachounganisha kila kitu katika umoja mkamilifu. 15 Amani inayotoka kwa Kristo itawale fahamu zenu. Mliitwa kwa ajili ya amani ili muwe pamoja katika mwili[c] mmoja. Mwe na shukrani daima.

16 Na mafundisho ya Kristo[d] yakae kwa wingi ndani yenu. Mfundishane na mshauriane ninyi kwa ninyi kwa hekima yote, mkiimba zaburi, nyimbo za sifa na nyimbo zinaowezeshwa na roho na kumshukuru Mungu katika mioyo yenu. 17 Kila mnachosema na kutenda, mkifanye kwa ajili ya Yesu Kristo Bwana wenu huku mkimshukuru Mungu Baba kupitia Yesu Kristo.

Utu Wenu Mpya Mkiwa Nyumbani

18 Wake, muwe radhi kuwatumikia waume zetu. Ni jambo sahihi kufanya katika kumfuata Bwana.

19 Waume wapendeni wake zenu na msiwe na hasira nao.

20 Watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote. Hili humfurahisha Bwana.

21 Wababa, msiwakorofishe watoto wenu, mkiwa wagumu kupendezwa nao; wanaweza kukata tamaa.

22 Enyi watumwa, watiini mabwana zenu katika mambo yote. Mwe watii kila wakati, hata kama wao hawawezi kuwaona. Msijifanye kazi kwa bidii ili wawatendee mema. Mnapaswa kuwatumikia mabwana[e] zenu kwa moyo kwa sababu mna hofu ya Bwana. 23 Kila kazi mnayoifanya, ifanyeni kwa bidii. Fanyeni kama mnamfanyia Bwana wenu wa mbinguni, na si kama mnamfanyia bwana wa dunia hii. 24 Mnajua kwamba mtapokea kutoka kwa Bwana ujira aliowaahidi watu wake. Ndiyo, mnamtumikia Kristo aliye Bwana[f] wenu halisi. 25 Kumbukeni kuwa Mungu hana upendeleo; kila afanyaye uovu ataadhibiwa kwa sababu ya uovu wake.

Enyi mabwana, wapeni kilicho chema na chenye haki watumwa wenu. Kumbukeni kuwa Mkuu wenu yuko mbinguni.

Mambo ya Kufanya

Msiache kuomba kamwe. Iweni tayari kwa lolote kwa kuomba na kushukuru. Mtuombee na sisi pia, ili Mungu atupe fursa za kuwaeleza watu ujumbe wake. Nimefungwa kwa sababu ya hili. Lakini ombeni ili tuendelee kuwaeleza watu siri ya kweli ambayo Mungu ameiweka wazi kuhusu Kristo. Niombeeni ili niseme yanayonipasa kusema, ili niweze kuiweka wazi kweli hii kwa kila mtu.

Iweni na hekima kwa namna mnavyochukuliana pamoja na wale wasioamini. Tumieni muda wenu vizuri kadri mwezavyo. Kila mnapozungumza pamoja na walio nje ya kundi lenu, muwe wema na wenye hekima. Ndipo mtaweza kumjibu kila mtu ipasavyo.

Habari Kuhusu Wale Walio Pamoja na Paulo

Tikiko ni ndugu yangu mpendwa katika Kristo. Yeye ni msaidizi mwaminifu na anamtumikia Bwana pamoja nami. Atawaambia kila kitu kuhusu mimi. Hii ndiyo sababu ninamtuma, ninataka mfahamu hali yetu, na ninamtuma awatie moyo ninyi. Ninamtuma yeye pamoja na Onesimo, ndugu mpendwa na mwaminifu kutoka kwenye kundi lenu. Watawaeleza kila kitu kilichotokea hapa.

10 Aristarko, aliyefungwa pamoja nami humu gerezani anawasalimu. Marko, binamu yake Barnaba anawasalimu pia. (Nimekwisha kuwaambia kuhusu Marko. Ikiwa atakuja, mpokeeni.) 11 Pia pokeeni salamu toka kwa Yesu, aitwaye pia Yusto. Hawa ni Wayahudi waamini pekee wanaofanya kazi pamoja nami kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Wamekuwa faraja kubwa sana kwangu.

12 Epafra, mtumishi mwingine wa Yesu Kristo, kutoka kwenu anawasalimu. Yeye anahangaika kwa ajili yenu kwa kuwaombea mara kwa mara, ili mkue kiroho na kupokea kila kitu ambacho Mungu anataka kwa ajili yangu. 13 Ninafahamu kwamba amefanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu ninyi na kwa ajili ya watu wa Laodikia na Hierapoli. 14 Pokeeni pia salamu kutoka kwa Dema na kutoka kwa rafiki yetu mpendwa Luka ambaye ni tabibu.

15 Wasalimuni kaka na dada zetu walioko Laodikia. Msalimuni pia Nimfa na kanisa lililo katika nyumba yake. 16 Baada ya kusoma barua hii, ipelekeni katika kanisa la Laodikia, ili isomwe huko pia. Ninyi nanyi msome barua niliyowaandikia wao. 17 Mwambieni Arkipo hivi, “Hakikisha unaifanya kazi aliyokupa Bwana.”

18 Hii ni salamu yangu ambayo nimeiandika kwa mkono wangu mwenyewe: Paulo. Msiache kunikumbuka nikiwa hapa gerezani. Ninawaombea neema ya Mungu iwe pamoja nanyi nyote.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International