Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Read the New Testament in 24 Weeks

A reading plan that walks through the entire New Testament in 24 weeks of daily readings.
Duration: 168 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
1 Timotheo 5-6

Usiseme kwa hasira kwa mtu mzima. Lakini sema naye kama baba yako. Watunze vijana kama kaka zako. Watendee wanawake wazee kama mama zako. Na watendee wanawake vijana kwa heshima zote kama vile ni dada zako.

Kuwatunza Wajane

Watunze wajane ambao hasa wanahitaji msaada. Lakini mjane akiwa na watoto au wajukuu, jambo la kwanza ambalo wanahitaji kujifunza ni hili: kutimiza wajibu waliyonao kwa wanafamilia wao. Kwa kuwapa heshima na kuwahudumia, watakuwa wanawalipa fadhila wazazi wao na pia mababu na nyanya zao. Na haya ndiyo mambo yanaompendeza Mungu. Mjane ambaye hakika anahitaji msaada ni yule ambaye ameachwa pekee yake. Anamuamini Mungu kumtunza katika mahitaji yake. Anayemuomba msaada Mungu wakati wote. Lakini mjane anayetumia maisha yake kujipenda ni hakika amekufa angali hai. Wambie waumini huko kutunza familia zao wenyewe ili kwamba asiwepo yeyote atakayesema wanafanya vibaya. Kila mtu atunze watu wa kwao, muhimu sana watunze familia zao. Kama hawatendi hayo watakuwa hawakubaliani na tunayoamini. Watakuwa wabaya kuliko hata asiyeamini.

Ili kuongezwa kwenye orodha ya wajane, mwanamke ni lazima awe na umri wa miaka 60 au zaidi, awe aliyekuwa mwaminifu kwa mume[a] wake. 10 Ni lazima ajulikane kwa mema aliyoyafanya: kulea watoto, kukaribisha wageni kwenye nyumba yake, kuwasaidia watu wa Mungu wenye uhitaji,[b] wenye shida, na kutumia maisha yake kufanya wema wa aina zote.

11 Lakini usiwaweke wajane wachanga katika orodha. Nguvu zao za mahitaji ya mwili zinawavuta wajiondea kwa Kristo, wanataka kuolewa tena. 12 Kisha watahukumiwa kustahili adhabu kwa kutofanya walichoahidi kutenda hapo kwanza. 13 Pia, wajane hawa vijana wanaanza kupoteza muda wao kwa kujihusisha na mambo ya watu wengine yasiyowahusu. Wanazungumzia mambo ambayo wasingepaswa kuzungumza. 14 Hivyo nataka wajane vijana kuolewa, kuzaa watoto, na kutunza nyumba zao. Kama wakifanya hivi, adui yetu hatakuwa na sababu ya kutupinga kwa sababu yao. 15 Lakini wajane wengine vijana wamegeuka na kumfuata Shetani.

16 Kama yupo mwanamke aliyeamini aliye na wajane katika familia yake, ni lazima awatunze yeye mwenyewe. Ndipo Kanisa halitakuwa na mzigo wa kuwatunza hao bali kuwatunza ambao hawana mtu yeyote wa kuwasaidia.

Mambo mengine zaidi juu ya Wazee na mengineyo

17 Wazee wanaoliongoza Kanisa katika njia nzuri wanapaswa kupokea heshima mara mbili;[c] hasa wale wanaofanya kazi ya kuhubiri na kufundisha. 18 Kama Maandiko yanavyosema, “Mnyama wa kazi akitumika kutenganisha ngano, usimzuie kula nafaka.”(A) Na Maandiko pia yanasema, “Mfanyakazi anatakiwa kupewa ujira wake.”(B)

19 Usimsikilize yeyote anayemshitaki mzee. Unatakiwa kuwasikiliza tu kama wapo wawili au watatu ambao wanaweza kusema alichokosea mzee. 20 Waambie wazee wanaotenda dhambi kwamba wana hatia, ufanye hivi mbele ya kanisa lote ili wengine wapate kuonywa.

21 Mbele ya Mungu na Kristo Yesu na malaika walioteuliwa, nakuambia fanya hukumu hizo bila upendeleo. Mtendee kila mtu sawa sawa.

22 Fikiri kwa makini kabla ya kuweka mikono yako juu ya yeyote kumfanya mzee. Usishiriki dhambi za wengine, na ujitunze uwe safi.

23 Timotheo, acha kunywa maji tu, kunywa na kiasi kidogo cha mvinyo. Hii itakusaidia tumbo lako, na hutaugua mara kwa mara.

24 Dhambi za watu wengine ni rahisi kuziona, hizo zinaonesha kwamba watahukumiwa. Lakini dhambi za wengine zitajulikana tu hapo baadaye. 25 Inafanana na mambo mazuri wanayofanya watu. Zingine ni rahisi kuonekana. Lakini hata kama si dhahiri sasa, hakuna hata moja itakayojificha milele.

Maagizo maalumu kwa Watumwa

Wote ambao ni watumwa waoneshe heshima kubwa kwa mabwana zao. Ndipo jina la Mungu na mafundisho yetu hayatakosolewa. Baadhi ya watumwa wanao mabwana ambao ni waamini, hivyo hao ni ndugu. Je, inamaanisha wasiwaheshimu mabwana zao? Hapana, watawatumikia hata kwa uzuri zaidi, kwa sababu wanawasaidia waaminio, watu wawapende.

Haya ni mambo ambayo lazima uyafundishe na kumwambia kila mtu kufanya.

Mafundisho ya Uongo na Utajiri wa Kweli

Watu wengine wanafundisha uongo na hawakubaliani na mafundisho ya kweli ambayo yanatoka kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Hawakubali mafundisho ambayo yanatuongoza kumheshimu na kumpendeza Mungu. Wanajivunia wanayoyafahamu, lakini hawaelewi chochote. Wamepagawa na wana ugonjwa wa kupenda mabishano na mapigano ya maneno. Na hayo yanaleta wivu, ugomvi, matusi, na uovu wa kutoaminiana. Daima wanaleta shida, kwa sababu ni watu ambao kufikiri kwao kumeharibiwa. Wamepoteza ufahamu wao wa ukweli. Wanafikiri kwamba kujifanya wanamheshimu Mungu ni njia ya kupata utajiri.

Kuishi kwa kumheshimu Mungu, hakika, ni njia ambayo watu hutajirika sana, kwa sababu inamaanisha wanaridhika na walivyo navyo. Tulipokuja ulimwenguni, tulikuja bila kitu, na tutakapokufa hatutachukua chochote. Hivyo, kama tukiwa na chakula na nguo, tutaridhika navyo. Watu ambao wanatamani kuwa matajiri wanajiletea majaribu wenyewe. Wananasa katika mtego. Wanaanza kutaka vitu vingi vya kijinga ambavyo vitawaumiza na kuwaharibu. 10 Kupenda fedha kunasababisha aina zote za uovu. Watu wengine wamegeuka kutoka kwenye imani yetu kwa sababu wanataka kupata fedha nyingi zaidi. Lakini wamejisababishia wenyewe maumivu mengi na huzuni.

Baadhi ya mambo ya Kukumbuka

11 Lakini wewe ni mali ya Mungu. Hivyo kaa mbali na mambo hayo yote, daima jaribu kutenda mema ili umheshimu Mungu na uwe na imani, upendo, uvumilivu, na upole. 12 Tunatakiwa tupigane kutunza imani yetu. Jaribu kwa bidii kadri unavyoweza kushinda vita vya thawabu. Tunza uzima wa milele. Ni uzima mliyouchagua kuupata mlipoikiri imani yenu katika Yesu; huo ukweli wa ajabu mliousema waziwazi kwa wote kuusikia. 13 Mbele ya Mungu na Kristo Yesu nakupa amri. Yesu ni yule aliyeshuhudia ukweli aliposimama mbele ya Pontio Pilato. Mungu ndiye anayetoa uhai kwa kila kitu. Nakuambia haya sasa: 14 Tenda niliyokuamuru kufanya bila dosari au kulaumu mpaka muda atakapo rudi. 15 Mungu atafanya hayo yatokee wakati utakapotimia. Yeye ni mwenye utukufu zaidi na mtawala pekee, mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana. 16 Mungu pekee hafi, anaishi katika nuru angavu sana ambayo watu hawawezi kusogea karibu. Hakuna mtu aliyemwona Mungu; wala anayeweza kumuona. Heshima na nguvu ni zake milele. Amina.

17 Wape amri hii wale ambao ni matajiri wa vitu vya ulimwengu huu. Waambie wasiwe na majivuno, bali wamtumaini Mungu wala si katika fedha zao. Fedha haziwezi kuaminiwa, lakini Mungu anatuhudumia kwa ukarimu mkubwa na anatupa vitu vyote ili tufurahi. 18 Waambie wale ambao ni matajiri watende mema. Wawe matajiri katika kuzifanya kazi njema. Na uwambie wawe tayari kutoa na kuwapa wengine vitu. 19 Kwa kufanya hivi, watajiwekea hazina kwa ajili yao wenyewe. Na hazina hiyo itakuwa ni msingi imara huo utakuwa msingi imara ambao maisha yao ya siku zijazo yatajengwa. Wataweza kuwa na maisha yaliyo ya kweli kabisa.

20 Timotheo, Mungu ameweka vitu vingi kwako uvitunze. Uvitunze vyema. Jitenge na watu wanaosema mambo yasiyofaa ambayo hayatoki kwa Mungu na wale wanaokupinga na “elimu” ambayo siyo “elimu” kabisa. 21 Watu wengine wanaodai kuwa na “elimu” wamepotea mbali kabisa kutokana na wanachoamini.

Ninaomba neema ya Mungu iwe kwenu nyote.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International