Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Read the New Testament in 24 Weeks

A reading plan that walks through the entire New Testament in 24 weeks of daily readings.
Duration: 168 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Matendo 3-4

Petro Amponya Kiwete

Siku moja Petro na Yohana walikwenda eneo la Hekalu saa tisa mchana, muda wa kusali na kuomba Hekaluni kama ilivyokuwa desturi. Walipokuwa wanaingia katika eneo la Hekalu, mtu aliyekuwa mlemavu wa miguu maisha yake yote alikuwa amebebwa na baadhi ya rafiki zake waliokuwa wanamleta Hekaluni kila siku. Walimweka pembezoni mwa mojawapo ya Malango nje ya Hekalu. Lango hilo liliitwa Lango Zuri. Na mtu huyo alikuwa akiwaomba pesa watu waliokuwa wanaingia Hekaluni. Siku hiyo alipowaona Petro na Yohana wakiingia eneo la Hekalu, aliwaomba pesa.

Petro na Yohana, walimtazama mtu huyo, wakamwambia, “Tutazame!” Akawatazama akitumaini kuwa wangempa pesa. Lakini Petro akasema, “Sina fedha wala dhahabu yoyote, lakini nina kitu kingine ninachoweza kukupa. Katika jina la Yesu Kristo wa Nazareti simama na utembee!”

Kisha Petro akamshika mkono wake wa kulia, akamnyenyua na kumsimamisha. Ndipo nyayo na vifundo vyake vikatiwa nguvu papo hapo. Akaruka juu, akasimama kwa miguu yake na akaanza kutembea. Akaingia ndani ya eneo la Hekalu pamoja nao huku akitembea na kurukaruka akimsifu Mungu. 9-10 Watu wote walimtambua. Walimjua kuwa ni mlemavu wa miguu ambaye mara nyingi huketi kwenye Lango Zuri la Hekalu akiomba pesa. Lakini sasa walimwona anatembea na kumsifu Mungu. Walishangaa na hawakuelewa hili limewezekanaje.

Petro Azungumza na Watu

11 Huku wakishangaa, watu wale waliwakimbilia Petro na Yohana pale walikokuwa katika Ukumbi wa Sulemani. Mtu yule aliyeponywa alikuwa akingali amewang'anga'nia Petro na Yohana.

12 Petro alipoona hili, aliwaambia watu: “Ndugu zangu Wayahudi, kwa nini mnashangaa hili? Mnatutazama kama vile ni kwa nguvu zetu tumemfanya mtu huyu atembee. Mnadhani hili limetendeka kwa sababu sisi ni wema? 13 Hapana, Mungu ndiye aliyetenda hili! Ni Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo. Ni Mungu aliyeabudiwa na baba zetu wote. Kwa kufanya hili, alimtukuza Yesu mtumishi wake, yule ambaye ninyi mlimtoa ili auawe. Pilato alipotaka kumwachia huru, mlimwambia Pilato kuwa hamumtaki Yesu. 14 Yesu alikuwa Mtakatifu na mwema, lakini mlimkataa na badala yake mlimwambia Pilato amwache huru mwuaji[a] na awape ninyi. 15 Na hivyo mlimwua yule awapaye uzima! Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu. Sisi ni mashahidi wa jambo hili kwani tuliliona kwa macho yetu wenyewe.

16 Huyu mlemavu wa miguu ameponywa kwa sababu tunalo tumaini katika Yesu. Nguvu ya Yesu ndiyo iliyomponya. Mnamwona na mnamfahamu mtu huyu. Ameponywa kabisa kwa sababu ya imani inayotokana na Yesu. Ninyi nyote mmeona hili likitokea!

17 Kaka zangu, ninajua kwamba hamkujua mlilomtendea Yesu wakati ule. Hata viongozi wenu hawakujua walilokuwa wanatenda. 18 Lakini Mungu alikwishasema kupitia manabii kuwa mambo haya yangetokea. Masihi wake angeteseka na kufa. Nimewaambia jinsi ambavyo Mungu alifanya jambo hili likatokea. 19 Hivyo lazima mbadili mioyo na maisha yenu. Mrudieni Mungu, naye atawasamehe dhambi zenu. 20 Kisha Bwana atawapa muda wa faraja kutokana na masumbufu yenu. Atamtuma Yesu kwenu, aliyemchagua kuwa Masihi wenu.

21 Lakini Yesu lazima akae mbinguni mpaka wakati ambapo kila kitu kitafanywa upya tena. Mungu alikwisha sema kuhusu wakati huu tangu zamani kupitia manabii wake watakatifu. 22 Musa alisema, ‘Bwana Mungu wako atakupa nabii. Nabii huyo atatoka miongoni mwa watu wako. Atakuwa kama mimi. Ni lazima mtii kila kitu atakachowaambia. 23 Na yeyote atakayekataa kumtii nabii huyo atakufa na kutengwa na watu wa Mungu.’(A)

24 Samweli, na manabii wengine wote walisema kwa niaba ya Mungu. Baada ya Samweli, walisema kuwa wakati huu ungekuja. 25 Na kile ambacho manabii walikisema ni kwa ajili yenu ninyi wazaliwa wao. Mmepokea Agano ambalo Mungu alilifanya na baba zenu. Mungu alimwambia baba yenu Ibrahimu kuwa, ‘Kila taifa duniani litabarikiwa kupitia wazaliwa wako.’(B) 26 Mungu amemtuma Yesu, mtumishi wake maalumu. Alimtuma kwenu kwanza, ili awabariki kwa kuwageuza kila mmoja wenu aache njia zake za uovu.”

Mitume Mbele ya Baraza Kuu la Wayahudi

Petro na Yohana walipokuwa wanazungumza na watu, ghafla baadhi ya viongozi wa Kiyahudi waliwaendea. Walikuwepo baadhi ya makuhani, mkuu wa askari wanaolinda Hekalu na baadhi ya Masadukayo. Walikasirika kwa sababu ya mafundisho ambayo Petro na Yohana walikuwa wanawafundisha na kuwaambia watu kuhusu Yesu. Mitume walikuwa wanafundisha pia kwamba watu watafufuka kutoka kwa wafu. Waliwakamata Petro na Yohana. Kwa kuwa ilikuwa jioni tayari, waliwaweka gerezani usiku ule mpaka siku iliyofuata. Lakini watu wengi waliowasikia mitume waliamini walichosema. Na siku hiyo idadi ya watu katika kundi la waamini ikafikia watu 5,000.

Siku iliyofuata, watawala wa Kiyahudi, wazee na walimu wa sheria walikutana Yerusalemu. Kuhani mkuu Anasi alikuwepo. Kayafa, Yohana, Iskanda na jamaa wengine wa kuhani mkuu walikuwepo pia. Waliwasimamisha Petro na Yohana mbele ya watu wote. Wakawauliza maswali mengi, “Mliwezaje kumponya mlemavu wa miguu huyu? Mlitumia nguvu gani? Mmefanya hili kwa mamlaka ya nani?”

Ndipo Petro, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akawaambia, “Enyi watawala nanyi wazee wa watu, mnatuuliza leo ni nini tulifanya kumsaidia huyu mlemavu wa miguu? Mnatuuliza nini kilimponya? 10 Tunataka ninyi nyote na watu wote wa Israeli mtambue kuwa mtu huyu aliponywa na nguvu ya Yesu Kristo kutoka Nazareti. Mlimpigilia Yesu msalabani, lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu. Mtu huyu alikuwa mlemavu wa miguu, lakini sasa ni mzima. Anaweza kusimama hapa mbele zenu kwa sababu ya nguvu ya Yesu! 11 Yesu ndiye

‘Jiwe[b] ambalo ninyi wajenzi mlilikataa.
    Lakini jiwe hili limekuwa jiwe na msingi.’(C)

12 Yesu peke yake ndiye anayeweza kuokoa watu. Jina lake ndiyo nguvu pekee iliyotolewa kumwokoa mtu yeyote ulimwenguni. Ni lazima tuokoke kupitia yeye!”

13 Viongozi wa Kiyahudi walijua kuwa Petro na Yohana walikuwa watu wa kawaida wasio na elimu yo yote. Lakini walikuwa wanazungumza kwa ujasiri bila woga; viongozi walishangaa. Walitambua pia kuwa Petro na Yohana walikuwa pamoja na Yesu. 14 Walimwona aliyeponywa akiwa amesimama kwa miguu yake mwenyewe pembeni mwa mitume. Na hivyo walishindwa kuzungumza chochote kilicho kinyume na mitume.

15 Viongozi wa Kiyahudi wakawaambia mitume watoke nje ya chumba cha mkutano wa baraza. Kisha viongozi wakajadiliana wao wenyewe juu ya nini wanachopaswa kufanya. 16 Wakaulizana, “Tuwafanye nini watu hawa? Kila mtu katika Yerusalemu anajua kuhusu muujiza walioufanya kama ishara kutoka kwa Mungu. Ni dhahiri, hatuwezi kusema muujiza huo haukufanyika. 17 Lakini ni lazima tuwatishe ili wasiendelee kuwaambia watu kutumia jina lile.[c] Ili tatizo hili lisisambae miongoni mwa watu.”

18 Hivyo viongozi wa Kiyahudi wakawaita Petro na Yohana ndani tena. Wakawaambia wasiseme wala kufundisha kitu chochote kwa kutumia jina la Yesu. 19 Lakini Petro na Yohana wakawajibu, “Mnadhani kipi ni sahihi? Mungu angetaka nini? Je, tunapaswa kuwatii ninyi au tumtii Mungu? 20 Hatuwezi kukaa kimya. Ni lazima tuwaambie watu kuhusu yale tuliyoona na kusikia.”

21-22 Viongozi wa Kiyahudi hawakupata sababu za kuwaadhibu mitume, kwa sababu watu wote walikuwa wanamsifu Mungu kwa kile kilichotendeka. Muujiza huu ulikuwa ishara kutoka kwa Mungu. Mtu aliyeponywa alikuwa na miaka zaidi ya arobaini. Hivyo viongozi wa Kiyahudi wakawaonya mitume tena na kuwaacha waende wakiwa huru.

Petro na Yohana Warudi kwa Waamini

23 Petro na Yohana waliondoka kwenye mkutano wa viongozi wa Kiyahudi na kurudi kwa waamini wenzao. Wakalieleza kundi la waamini kila kitu walichoambiwa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. 24 Waamini waliposikia hili, wote kwa pamoja wakamwomba Mungu wakiwa na nia moja. Wakasema, “Bwana wa wote, wewe ndiye uliyeumba mbingu, dunia, bahari na kila kitu ulimwenguni. 25 Baba yetu Daudi alikuwa mtumishi wako. Kwa msaada wa Roho Mtakatifu aliandika maneno haya:

‘Kwa nini mataifa yanatenda kwa kiburi?
    Kwa nini watu wanapanga mipango isiyofaa kama hii?
26 Wafalme wa dunia hujiandaa kwa mapigano,
    na watawala hukusanyika pamoja kinyume na Bwana
    na kinyume na Masihi wake.’(D)

27 Ndicho hasa kilichotokea wakati Herode, Pontio Pilato, mataifa mengine na watu wa Israeli walipokusanyika pamoja hapa Yerusalemu wakawa kinyume na Yesu; Masihi, Mtumishi wako mtakatifu. 28 Watu hawa waliokusanyika pamoja kinyume na Yesu waliwezesha mpango wako kukamilika. Ilifanyika kwa sababu ya nguvu zako na matakwa yako. 29 Na sasa, Bwana, sikiliza wanayosema. Wanajaribu kututisha. Sisi ni watumishi wako. Tusaidie ili tuseme yale unayotaka tuseme bila kuogopa. 30 Tusaidie, ili tuwe jasiri kwa kutuonesha nguvu zako. Ponya Wagonjwa. Fanya ishara na maajabu kutokea kwa mamlaka[d] ya Yesu mtumishi wako mtakatifu.”

31 Baada ya waamini kuomba, mahali walipokuwa palitikisika. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, na wakaendelea kuhubiri Habari Njema bila woga.

Ushirika wa Waamini

32 Kundi lote la waamini waliungana katika kuwaza na katika mahitaji yao. Hakuna aliyesema vitu alivyokuwa navyo ni vyake peke yake. Badala yake walishirikiana kila kitu. 33 Kwa nguvu kuu mitume walifanya ijulikane kwa kila mmoja kwamba Bwana Yesu alifufuliwa kutoka kwa wafu. Na Mungu aliwabariki sana waamini wote. 34 Hakuna aliyepungukiwa kitu. Kila aliyemiliki shamba au nyumba aliuza na kuleta pesa alizopata, 35 na kuzikabidhi kwa mitume. Kisha kila mtu akapewa kiasi alichohitaji.

36 Mmoja wa waamini aliitwa Yusufu. Mitume walimwita Barnaba, jina linalomaanisha “Mtu anayewatia moyo wengine.” Alikuwa Mlawi mzaliwa wa Kipro. 37 Yusufu aliuza shamba alilomiliki. Akaleta pesa na kuwapa mitume.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International