Read the New Testament in 24 Weeks
Baraka za Mungu Huja Kwa Imani
3 Ninyi watu wa Galatia, je mmepoteza fahamu zenu? Nilidhani mmeelewa kwa nini Yesu Kristo alisulubiwa msalabani! Niliwaeleza wazi kabisa jambo hilo, kama vile kuchora na kupaka rangi picha mbele ya macho yenu. Je, kuna mtu yeyote aliyewaloga mkasahau? 2 Niambieni jambo hili moja: Ni jinsi gani mlimpokea Roho? Je, mlimpokea Roho kwa kufuata sheria? Hapana, mlimpokea Roho kwa sababu ya ujumbe kuhusu Yesu unaoleta imani. 3 Mliyaanza maisha yenu mapya pamoja na Roho. Inakuwaje sasa mdhani kuwa mnaweza kukamilishwa na kitu kinyonge kama tohara kilichofanyika katika miili yenu?[a] Basi mmepoteza fahamu zenu! 4 Je, mlipata uzoefu huo mwingi pasipo manufaa yoyote? Sidhani kama hivyo ndivyo! 5 Je, Mungu anawapa ninyi Roho na kutenda miujiza miongoni mwenu kwa kuwa mnaifuata sheria? Hapana sivyo! Mungu anawapa ninyi baraka hizi kwa njia ya ujumbe unaoleta imani katika kumwamini Yesu.
6 Maandiko yanasema kitu hicho hicho kuhusu Ibrahimu. “Ibrahimu alimwamini Mungu, na Mungu akaikubali imani yake na akamhesabia haki.”(A) 7 Hivyo mnapaswa kuelewa kuwa watoto sahihi wa Ibrahimu ni wale walio na imani. 8 Maandiko yalieleza ambacho kingetokea katika siku zijazo. Maandiko haya yalisema kwamba Mungu angewafanya wasio Wayahudi kuwa wenye haki kwa njia ya imani. Mungu alizisema Habari Njema hizi kwa Ibrahimu kabla haijatokea. Mungu alimwambia Ibrahimu, “Kwa kukubariki wewe, nitawabariki watu wote duniani.”(B) 9 Kwa hiyo, wale wote wanaoweka imani yao kwa Mungu ndiyo wanaobarikiwa pamoja na Ibrahimu aliyekuwa mwaminifu.
10 Lakini watu wale wanaodhani kuwa kutii sheria ndicho kitu muhimu sana daima hukaa chini ya tishio la laana. Kama vile Maandiko yanavyosema, “Amelaaniwa mtu yeyote atakayeacha kuzishika na kuzitii sheria hizi zote.”(C) 11 Hivyo ni dhahiri kuwa hakuna anayeweza kuhesabiwa haki mbele za Mungu kwa kuifuata sheria. Maandiko yanasema, “Mwenye haki mbele za Mungu ataishi kwa imani.”(D)
12 Sheria haitegemei imani. Hapana, inasema kuwa njia pekee ambayo mtu anaweza kupata uzima kwa njia ya sheria ni kwa kutii amri zake.[b] 13 Sheria inasema kuwa sisi Wayahudi tuko chini ya laana kwa kutokuitii daima. Lakini Kristo alituweka huru kutoka katika laana hiyo. Alikubali kulaaniwa na sheria ili atuokoe. Maandiko yanasema, “Yeyote anayening'inizwa mtini[c] yuko chini ya laana.”(E) 14 Kwa sababu ya yale aliyoyafanya Kristo Yesu, baraka ambazo Mungu alimwahidi Ibrahimu zilitolewa pia kwa wasio Wayahudi. Kristo alikufa ili kwamba kwa kumwamini sisi sote, Wayahudi na wasio Wayahudi, tuweze kumpokea Roho ambaye Mungu aliahidi.
Sheria na Ahadi
15 Ndugu zangu, hebu niwape mfano kutoka maisha ya kila siku: Fikiri kuhusu makubaliano ambayo mtu hukubaliana na mwingine. Baada ya makubaliano hayo kufanywa rasmi, hakuna anayeweza kuongeza chochote kwenye makubaliano hayo na hakuna anayeweza kulipuuza. 16 Mungu aliweka agano kwa Ibrahimu na uzao wake. Maandiko hayasemi, “na kwa ajili ya uzao wenu”. Hilo lingekuwa na maana ya watu wengi. Lakini linasema, “na kwa uzao wako”. Hiyo ina maana ya uzao mmoja tu, na uzao huo ni Kristo. 17 Hii ndiyo maana yangu: Agano ambalo Mungu aliliweka na Ibrahimu lilifanywa rasmi na Mungu muda mrefu kabla ya kuja kwa sheria. Sheria ilikuja miaka 430 baadaye. Hivyo sheria haingeweza kulifuta agano hilo na kuibadili ahadi ya Mungu.
18 Baraka alizonazo Mungu kwa ajili ya watu wake hazipatikani kwa njia ya sheria. Ikiwa ingekuwa hivyo, basi isingekuwa ahadi ya Mungu inayotuletea sisi baraka hiyo. Lakini Mungu aliitoa bure baraka yake kwa Ibrahamu kama agano.
19 Hivyo kwa nini sheria ilitolewa? Sheria ililetwa baadaye kwa sababu ya makosa wanayotenda[d] watu. Lakini sheria ingeendelea kutumika hadi kuja kwa Uzao wa Ibrahimu. Huyu ni Uzao unaotajwa katika agano lililotolewa na Mungu. Lakini sheria ilitolewa kupitia malaika na malaika walimtumia Musa kama mpatanishi wa kuwapa watu sheria. 20 Hivyo mpatanishi anahitajika pale ambapo upande mmoja unapaswa kufikia mapatano. Lakini Mungu ambaye ni mmoja, hakumtumia mpatanishi alipompa ahadi Ibrahimu.[e]
Lengo la Sheria ya Musa
21 Je, hili lamaanisha kwamba sheria hutenda kazi kinyume na ahadi za Mungu? La hasha. Sheria iliyotolewa kamwe haikuwa na uwezo wa kuwaletea watu maisha mapya. Ingekuwa hivyo, basi tungehesabiwa haki mbele za Mungu kwa kuifuata sheria. 22 Lakini hilo halikuwa kusudi la sheria. Maandiko yanauweka ulimwengu wote chini ya udhibiti wa dhambi kama aina ya kifungo gerezani. Ili kile ambacho Mungu aliahidi kipokelewe kwa njia ya imani katika[f] Yesu Kristo. Hii hutolewa kwa wale wanaomwamini.
23 Kabla ya aliye mwaminifu kuja, sheria ilituweka sisi kama wafungwa. Hatukuwa huru hadi imani hii inayokuja[g] ilipofunuliwa kwetu. 24 Nina maana kuwa sheria ilikuwa ni mlezi aliyetusimamia[h] tu hadi Kristo alipokuja. Baada ya kuja kwake, tungefanyika kuwa wenye haki mbele za Mungu kwa njia ya imani. 25 Sasa kwa sababu imani hii imekuja, hatuhitaji tena kusimamiwa na kulelewa na sheria.
26 Hii ni kwa sababu ninyi nyote ni mali ya Kristo Yesu na ni watoto wa Mungu kwa njia ya imani. 27 Ndiyo, nyote mlibatizwa ili muunganike na Kristo. Hivyo sasa Kristo anawafunika kabisa kama kubadilisha nguo mpya kabisa. 28 Sasa, ndani ya Kristo haijalishi kama wewe u Myahudi au Myunani, mtumwa au huru, mwanaume au mwanamke. Wote mko sawa katika Kristo Yesu. 29 Na kwa vile ninyi ni wa Kristo, hivyo ninyi wazaliwa wa Ibrahamu. Ninyi ndiyo mtakaopokea baraka zote ambazo Mungu alimwahidi Ibrahimu.
4 Ninalolisema ni hili: Wakati mrithi wa vyote alivyomiliki baba yake bado ni mdogo, hana tofauti yo yote na mtumwa. Haijalishi kuwa anamiliki vitu vyote. 2 Wakati wa utoto bado anapaswa kuwatii wale waliochaguliwa kumtunza. Lakini anapoufikia umri ambao baba yake ameuweka, anakuwa huru. 3 Ndivyo ilivyo hata kwetu sisi. Mwanzoni tulikuwa kama watoto, tukiwa watumwa wa mamlaka za uovu[i] zinazoutawala ulimwengu huu wa sasa. 4 Lakini wakati sahihi ulipofika, Mungu akamtuma Mwanaye, aliyezaliwa na mwanamke na akaishi chini ya sheria. 5 Mungu alifanya hivi ili aweze kuwaweka huru wale waliokuwa chini ya sheria. Kusudi la Mungu lilikuwa kutuasili[j] sisi kama watoto wake.
6 Ninyi sasa ni watoto wa Mungu. Na ndiyo sababu Mungu amemtuma Roho wa Mwanaye mioyoni mwetu. Huyo Roho aliye ndani yetu hulia “Aba,[k] yaani Baba.” 7 Sasa ninyi si watumwa kama mwanzo. Ni watoto wa Mungu, na mtapokea kila kitu ambacho Mungu aliwaahidi watoto wake. Hii yote ni kwa sababu ya yale ambayo Mungu amewatendea ninyi.
Upendo wa Paulo kwa Waamini wa Galatia
8 Zamani hamkumjua Mungu. Mlikuwa watumwa wa miungu isiyokuwa halisi. 9 Lakini sasa mnamjua Mungu wa kweli. Hakika, Mungu ndiye anayewajua ninyi. Hivyo kwa nini sasa mnavigeukia vikosi dhaifu na visivyo na manufuaa yoyote mlivyovifuata hapo mwanzo? Mnataka kuwa watumwa wa mambo haya tena? 10-11 Inanipa wasiwasi kwa kuwa mnaadhimisha siku, miezi, misimu na miaka. Nina hofu ya kuwa nimefanya kwa bidii kazi bure kwa ajili yenu.
12 Ndugu zangu, naomba mniige mimi kama ambavyo mimi nimekuwa kama ninyi. Hamkunikosea kwa jambo lololote. 13 Mnajua kuwa nilikuja kwenu mara ya kwanza kwa sababu nilikuwa mgonjwa. Ndipo nilipowaeleza ninyi Habari Njema. 14 Ugonjwa wangu uliwaelemea. Hata hivyo hamkunikataa kutokana na fadhaa ama hofu. Bali, mlinikaribisha kama vile nilikuwa malaika kutoka kwa Bwana. Mlinipokea kama vile nilikuwa Kristo Yesu mwenyewe! 15 Mlikuwa na furaha sana wakati huo. Nini kimetokea kwa imani yenu ya awali kwamba mimi nilikuwa mtu niliyebarikiwa kipekee na Mungu? Naweza kusema bila shaka yoyote kwamba mngeliweza kufanya kitu chochote kunisaidia. Kama ingeliwezekana, mngeliyang'oa hata macho yenu na kunipa mimi. 16 Je, nimekuwa sasa adui yenu kwa sababu nawaambia ukweli?
17 Watu hawa[l] wanajitahidi sana kuonesha kuvutiwa nanyi,[m] lakini hiyo siyo nzuri kwenu. Wanataka kuwashawishi ninyi ili mtugeuke sisi na kuambatana nao. 18 Inapendeza daima kuwa na mtu anayevutiwa nawe katika jambo lililo jema. Hivyo ndivyo nilivyofanya nilipokuwa pamoja nanyi. Siku zote inapendeza, na si pale tu mimi nikiwapo. 19 Watoto wangu wadogo, nasikia uchungu tena kwa ajili yenu, kama mama anayejifungua. Nitaendelea kusikia uchungu huu mpaka watu watakapofikia kumwona Kristo wawatazamapo ninyi. 20 Natamani ningekuwa nanyi sasa. Ndipo labda ninapoweza kubadilisha namna ninavyoongea nanyi. Sasa sielewi nifanye nini juu yenu.
Mfano wa Hajiri na Sara
21 Baadhi yenu mnataka kuwa chini ya sheria. Niambieni, mnajua sheria inavyosema? 22 Maandiko yanasema kwamba Ibrahimu alikuwa na wana wawili. Mama wa mwana mmoja alikuwa ni mjakazi, na mama wa mwana mwingine alikuwa wa mwanamke aliye huru. 23 Mwana wa Ibrahimu kutoka kwa mjakazi alizaliwa kwa namna ya kawaida ya kibinadamu. Lakini mwana kutoka kwa mwanamke aliyekuwa huru alizaliwa kwa sababu ya ahadi ambayo Mungu alimpa Ibrahimu.
24 Habari hii ina maana nyingine kwenu. Wanawake wawili ni sawa na maagano mawili baina ya Mungu na watu wake. Agano moja ni sheria ambayo Mungu aliifanya katika Mlima Sinai, inayowafanya watu wawe watumwa. Mwanamke aliyeitwa Hajiri yuko kama agano la kwanza. 25 Hivyo Hajiri anauwakilisha Mlima Sinai uliopo Arabia. Na anafanana na Yerusalemu wa sasa, kwa sababu mji huu uko utumwani pamoja na watu wake. 26 Lakini Yerusalemu ya mbinguni ulio juu uko kama mwanamke aliye huru, ambaye ndiye mama yetu. 27 Maandiko yanasema,
“Ufurahi mwanamke, wewe uliye tasa.
Ufurahi kwani hukuwahi kuzaa.
Piga kelele na ulie kwa furaha!
Hukupata uchungu wa kuzaa.
Mwanamke aliye peke yake atapata watoto zaidi
zaidi ya mwanamke aliye na mume.”(F)
28 Ndugu zangu, ninyi ni watoto mliozaliwa kwa sababu ya ahadi ya Mungu, kama Isaka alivyozaliwa. 29 Lakini mwana mwingine wa Ibrahimu, aliyezaliwa kwa njia ya kawaida, alisababisha matatizo kwa yule aliyezaliwa kwa nguvu ya Roho. Ndivyo ilivyo leo. 30 Lakini Maandiko yanasemaje? “Mfukuze mjakazi na mwanawe! Mwana wa mwanamke aliye huru atapokea kila kitu alicho nacho baba yake, lakini mwana wa mjakazi hatapokea kitu.”(G) 31 Hivyo, kaka na dada zangu, sisi si watoto wa mjakazi. Ni watoto wa mwanamke aliye huru.
© 2017 Bible League International