Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Read the New Testament in 24 Weeks

A reading plan that walks through the entire New Testament in 24 weeks of daily readings.
Duration: 168 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Yakobo 4-5

Jitoe Mwenyewe kwa Mungu

Mapigano na magombano yanatokea wapi miongoni mwenu? Je, hayatoki kutoka ndani yenu wenyewe, kutoka katika tamaa zenu za starehe ambazo zinafanya vita siku zote ndani ya miili yenu? Mnataka mambo lakini hamyapati, hivyo mnaua na mnakuwa na wivu juu ya watu wengine. Lakini bado hamwezi kuyafikia mnayoyataka, hivyo mnagombana na kupigana. Nanyi ndugu zangu hampokei mambo mnayoyataka kwa sababu hamumwombi Mungu. Na mnapoomba, lakini hampokei cho chote kwa sababu mnaomba kwa dhamiri mbaya, ili muweze kuvitumia mlivyopatiwa kwa anasa zenu.

Watu msio waaminifu, hamjui kwamba kuupenda ulimwengu ni sawa na kumchukia Mungu? Yeyote anayetaka kuwa rafiki wa dunia hujifanya mwenyewe kuwa adui wa Mungu. Je, kile Maandiko yanachokisema hakina maana yoyote kwenu? Ile roho ambayo Mungu aliifanya ikae ndani yetu wanadamu imejaa tamaa yenye wivu? Lakini Mungu ametuonesha sisi, rehema kuu zaidi. Ndiyo maana Maandiko yanasema:

Mungu huwapinga wenye kiburi,
    lakini huwapa neema wale walio wanyenyekevu.(A)

Kwa hiyo jiwekeni chini ya Mungu. Mpingeni Shetani naye atawakimbia ninyi. Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Iosheni mikono yenu ninyi wenye dhambi na kuitakasa mioyo yenu enyi wanafiki! Ombolezeni na kulia! Kicheko chenu na kigeuzwe kuwa maombolezo, na furaha yenu igeuzwe kuwa huzuni kubwa. 10 Jinyenyekezeni chini ya Bwana, naye atawainua juu.

Wewe Siyo Hakimu

11 Ndugu, msiendelee kukosoana ninyi kwa ninyi. Yeye anayemnenea mabaya ndugu yake au anayemhukumu ndugu yake atakuwa anailaumu Sheria na atakuwa anaihukumu Sheria. Na kama utaihukumu Sheria, hautakuwa unafanya yale yanayosemwa na Sheria, bali utakuwa ni hakimu. 12 Kuna Mtoa Sheria mmoja tu na hakimu, ndiye Mungu aliye na uwezo wa kuokoa na kuangamiza. Hivyo wewe unafikiri ni nani, wewe unayemhukumu jirani yako?

Mwache Mungu Apange Maisha Yako

13 Sikilizeni mnaosema, “Leo au kesho tutasafiri kwenda kwenye mji huu au ule, na tutakaa mwaka mzima pale, tutafanya biashara hapo na kujipatia fedha nyingi.” 14 Hamjui hata yatakayotokea katika maisha yenu kesho yake tu. Kwani ninyi ni mvuke tu ambao huonekana kwa kipindi kifupi tu kisha hutoweka. 15 Badala yake, nyakati zote mngesema, “Kama Bwana anapenda, tutaishi na tutafanya hivi au vile.” 16 Kama ilivyo, ninyi mna kiburi na kujivuna. Majivuno yote ya jinsi hiyo ni uovu! 17 Hivyo sasa, mnaposhindwa kufanya mliyoyajua ni haki, mtakuwa na hatia ya dhambi.

Onyo kwa Matajiri na Wachoyo

Sikilizeni, ninyi matajiri! Ombolezeni na kulia kwa sauti kwa ajili ya dhiki inayowajia. Utajiri wenu umeoza, na mavazi yenu yameliwa na nondo. Dhahabu zenu na fedha vimeliwa na kutu! Hiyo kutu itakuwa ni ushuhuda dhidi yenu, na itaila miili yenu kama kwa moto. Mmejilimbikizia mali kwa ajili yenu katika kizazi hiki cha siku za mwisho! Angalieni! Mmeyazuia malipo ya wafanyakazi waliopalilia mashamba yenu. Sasa wananililia! Na kilio cha hao wanaovuna pia kimeyafikia masikio ya Bwana Aliye na Nguvu.

Mmeishi maisha ya anasa duniani na kujifurahisha na kila kitu mlichotaka. Mmeinenepesha miili yenu, kama wanyama walio tayari kwa siku ya kuchinjwa. Mmehukumu na kuua wale watu wasio na hatia, na ambao hawakupingana nanyi.

Uwe Mstahimilivu

Hivyo kina kaka na kina dada, muwe na subira; hadi kuja kwa mara ya pili kwa Bwana. Kumbukeni kuwa mkulima huyasubiria mazao yake yenye thamani yakue ardhini. Huyangoja kwa subira mpaka yapate mvua za masika na za vuli.[a] Hata ninyi pia mnapaswa kungoja kwa subira. Muwe imara mioyoni mwenu, kwa sababu kuja kwa Bwana mara ya pili kumekaribia. Kaka na dada zangu, msiendelee kunung'unikiana ninyi kwa ninyi, ili msije kuhukumiwa kuwa na hatia. Tazameni! Hakimu anasimama mlangoni akiwa tayari kuingia ndani.

10 Kina kaka na kina dada, fuateni mfano wa manabii waliosema kwa jina la Bwana. Wao walipata mateso mengi mabaya lakini walivumilia. 11 Na tunatoa heshima kubwa sana kwa wale wote waliostahimili mateso. Mmesikia juu ya uvumilivu wa Ayubu,[b] na mnayajua ya kuwa baada ya yote hayo Bwana alimsaidia. Hii basi inaonesha ya kuwa Bwana ni mwenye wingi wa rehema na huruma.

Uwe Makini na Unayosema

12 Juu ya mambo yote kaka zangu na dada zangu, usitumie kiapo unapotoa ahadi, Usiape kwa mbingu wala kwa dunia, ama kwa kitu kingine chochote. “Ndiyo” yenu na iwe “Ndiyo halisi”, na “Hapana” yenu na iwe “Hapana halisi”, ili msije mkaingia katika hukumu ya Mungu.

Nguvu ya Maombi

13 Je, miongoni mwenu kuna aliye na shida? Anapaswa kuomba. Je, yupo yeyote mwenye furaha? Anapaswa kuimba nyimbo za sifa. 14 Je, kuna yeyote kwenu aliye mgonjwa? Anapaswa kuwaita wazee wa kanisa kumwombea na kumpaka mafuta katika jina la Bwana. 15 Maombi yanayofanywa kwa imani yatamfanya mgonjwa apone, na Bwana atampa uzima. Kama atakuwa ametenda dhambi, Bwana atamsamehe.

16 Hivyo muungame dhambi ninyi kwa ninyi, na kuombeana ninyi kwa ninyi ili muweze kuponywa. Maombi yanayofanywa na mtu mwenye haki yana nguvu sana na yana matokeo makubwa sana. 17 Eliya alikuwa mwanadamu kama sisi tulivyo. Aliomba kwamba mvua isinyeshe, na haikunyesha katika ardhi kwa miaka mitatu na nusu. 18 Kisha akaomba tena inyeshe, na anga ikatoa mvua, na ardhi ikatoa mazao.

Kuwasaidia Watu Wanapotenda Dhambi

19 Kaka na dada zangu Ndugu zangu, kama mmoja wenu atapotoka katika kweli, na mwingine akamrejeza, 20 yule aliyemrejeza atambue kuwa yule anayemrejeza mtenda dhambi kutoka katika njia yake mbaya ataiokoa roho ya huyo mtu kutoka katika kifo cha milele na atasababisha dhambi nyingi zisamehewe.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International