Read the New Testament in 24 Weeks
Upendo Uwe Dira Yenu
13 Ninaweza kusema kwa lugha zingine, za wanadamu au za malaika. Lakini ikiwa sina upendo, mimi ni kengele yenye kelele na tuazi linalolia. 2 Ninaweza kuwa na karama ya unabii, ninaweza kuzielewa siri zote na kujua kila kitu kinachopaswa kujulikana, na ninaweza kuwa na imani kuu kiasi cha kuhamisha milima. Lakini pamoja na haya yote, ikiwa sina upendo, mimi ni bure. 3 Ninaweza kutoa kila kitu nilichonacho ili niwasaidie wengine na ninaweza hata kuutoa mwili wangu ili niweze kujisifu.[a] Lakini siwezi kupata chochote kwa kufanya haya yote ikiwa sina upendo.
4 Upendo huvumilia na ni mwema. Upendo hauna wivu, haujisifu na haujivuni. 5 Upendo hauna kiburi, hauna ubinafsi na haukasirishwi kirahisi. Upendo hautunzi orodha ya mambo waliyoukosea. 6 Upendo haufurahi wengine wanapokosa, lakini daima hufurahia ukweli. 7 Upendo kamwe haukati tamaa kwa watu. Kamwe hauachi kuamini, kamwe haupotezi tumaini na kamwe hauachi kuvumilia.
8 Upendo hautakoma. Lakini karama zote hizo zitafikia mwisho, hata karama ya unabii, karama ya kusema kwa lugha zingine na karama ya maarifa. 9 Hizi zitakoma kwa sababu maarifa haya na nabii hizi tulizonazo sasa hazijakamilika. 10 Lakini ukamilifu utakapokuja, mambo ambayo hayajakamilika yatakoma.
11 Nilipokuwa mtoto, nilizungumza kama mtoto, niliwaza kama mtoto, na kufanya mipango kama mtoto. Nilipokuwa mtu mzima, niliziacha njia za kitoto. 12 Ndivyo ilivyo hata kwetu. Kwa sasa tunamwona Mungu kwa taswira tu kama ilivyo katika kioo. Lakini, baadaye, tutamwona uso kwa uso. Kwa sasa ninajua sehemu tu, lakini wakati huo nitajua kila kitu, kama ambavyo Mungu amenijua mimi. 13 Hivyo mambo haya matatu yanaendelea; imani, tumaini na upendo. Na lililo kuu zaidi ya haya yote ni upendo.
Zitumieni Karama za Roho Kulisaidia Kanisa
14 Upendo uwe lengo la maisha yenu, lakini mnapaswa pia kuzitaka karama za Roho. Na itakeni sana karama ya unabii. 2 Nitafafanua ni kwa nini. Wenye karama ya kusema kwa lugha zingine hawazungumzi na watu. Huzungumza na Mungu. Hakuna anayewaelewa kwa sababu huzungumza mambo ya siri kupitia Roho. 3 Lakini wanaotabiri huzungumza na watu. Huwasaidia watu kuwa imara katika imani, na huwatia moyo na kuwafariji. 4 Wanaosema kwa lugha hujiimarisha wao wenyewe. Lakini wanaotabiri huliimarisha kanisa lote.
5 Ningependa ninyi nyote muwe na karama ya kusema kwa lugha zingine. Lakini ninachotaka zaidi ni ninyi kutabiri. Yeyote anayetabiri ni wa muhimu zaidi kuliko wale wanaosema kwa lugha zingine. Hata hivyo, ikiwa wanaweza kufasiri lugha hizo, basi kanisa linasaidiwa kutokana na kile wanachosema.
6 Ndugu zangu, je, itawasaidia nikija kwenu na kusema kwa lugha zingine? Hapana, itawasaidia pale tu nitakapowaletea ufunuo mpya au maarifa fulani, unabii au mafundisho. 7 Hii ni kweli hata kwa vitu visivyo na uhai vinavyotoa sauti kama filimbi na kinubi. Ikiwa muziki hauchezwi kwa ufasaha, hutaweza kujua ni wimbo gani unaopigwa. 8 Na katika vita, ikiwa tarumbeta haitatoa ishara vizuri, askari hawawezi kujua kuwa ni wakati wa kujiandaa kwa mapigano.
9 Ndivyo ilivyo hata kwenu ninyi. Watu hawataweza kuelewa unachosema, ikiwa utazungumza katika lugha tofauti wasiyoitambua. Utakuwa unazungumza hewani tu! 10 Ni dhahiri kuwa kuna lugha nyingi ulimwenguni, na zote zina maana. 11 Lakini ikiwa sielewi maana ya maneno wanayosema wengine, kwangu itakuwa sauti ya ajabu tu, na nitasikika kama ninayetoa sauti za ajabu. 12 Kwa kuwa mna nia kuhusu karama za Kiroho, muwe na hamu ya kulisaidia kanisa kuwa imara.
13 Hivyo wenye karama ya kusema kwa lugha waombe ili waweze kufasiri yale wanayosema. 14 Ninapoomba kwa lugha zingine, roho yangu inaomba, lakini akili yangu haifanyi chochote. 15 Hivyo nifanye nini? Nitaomba kwa roho yangu, lakini pia nitaomba kwa akili yangu. Nitaimba kwa roho yangu, lakini pia nitaimba kwa akili yangu. 16 Unaweza ukawa unamshukuru Mungu kwa roho yako. Lakini mtu mwingine ambaye haielewi lugha unayotumia hawezi kusema “Amina” kwa maombi yako ya shukrani. 17 Unaweza ukawa unamshukuru Mungu katika njia nzuri, lakini isiwasaidie wengine kuwa imara.
18 Ninamshukuru Mungu kwamba nimepewa karama ya kusema lugha aina nyingi mbalimbali kuliko yeyote kati yenu. 19 Lakini wakati wa mikutano ya kanisa napenda kuzungumza maneno matano ninayoyaelewa kuliko maelfu ya maneno katika lugha zingine. Ni afadhali nizungumze nikiwa katika uelewa wangu ili niwafundishe wengine.
20 Ndugu zangu, msiwaze kama watoto wadogo. Iweni kama watoto wachanga katika mambo maovu, lakini katika kuwaza kwenu muwe kama watu wazima, waliokua. 21 Kama Maandiko[b] yanavyosema,
“Kwa kutumia wanaozungumza lugha tofauti
na kutumia midomo ya wageni,
nitazungumza na watu hawa,
hata hivyo, hawatanitii.”(A)
Hivi ndivyo Bwana anasema.
22 Na kutokana na hili tunaona kwamba matumizi ya lugha zingine ni ishara kuonesha namna ambavyo Mungu anawashughulikia wasioamini, na si walioamini. Na unabii unaonesha namna ambavyo Mungu hutenda kazi kupitia wanaoamini, na si wasioamini. 23 Chukulieni kuwa kanisa lote limekusanyika nanyi nyote mkaanza kusema kwa lugha zingine. Ikiwa baadhi ya watu wasio sehemu ya kundi lenu au wasio waamini wataingia katika kusanyiko lenu, watasema ninyi ni wendawazimu. 24 Lakini chukulieni kuwa ninyi nyote mnatabiri na mtu asiyeamini ama asiyekuwa sehemu ya kundi lenu akaingia. Dhambi zao zitawekwa wazi kwao, na watahukumiwa kwa kila kitu mtakachosema. 25 Mambo ya siri katika mioyo yao yatajulikana. Na watapiga magoti na kumwabudu Mungu. Watakiri na kusema, “Pasipo shaka, Mungu yuko hapa pamoja nanyi.”[c]
Mikutano Yenu Inapaswa Kuwasaidia Wote
26 Basi ndugu, mnapaswa kufanya nini? Mnapokusanyika, mtu mmoja ana wimbo, mwingine ana mafundisho na mwingine ana kweli mpya kutoka kwa Mungu. Mmoja anasema kwa lugha nyingine na mwingine anafasiri lugha hiyo. Cho chote mnachofanya lazima kiwe na lengo la kumfanya kila mmoja wenu akue katika imani. 27 Mnapokusanyika, ikiwa kuna yeyote atasema na kanisa katika lugha, iwe watu wawili tu au isiwe zaidi ya watu watatu. Na wanapaswa wanene kwa zamu, mmoja baada ya mwingine. Na mwingine afasiri kile wanachosema. 28 Lakini ikiwa hakuna mfasiri, basi mtu yeyote anayesema kwa lugha nyingine anapaswa kunyamaza kimya. Wanapaswa kuzungumza katika nafsi zao wenyewe ama na Mungu.
29 Na manabii wawili au watatu tu ndiyo wanapaswa kuzungumza. Wengine watathmini kile wanachosema. 30 Na ujumbe kutoka kwa Mungu ukimjia mtu aliyekaa, mzungumzaji wa kwanza anapaswa kunyamaza. 31 Nyote mnaweza kutabiri mmoja baada ya mwingine. Kwa njia hii kila mmoja anaweza kufundishwa na kutiwa moyo. 32 Roho za manabii ziko chini ya udhibiti wa manabii[d] wenyewe. 33 Mungu si Mungu wa machafuko lakini ni Mungu wa amani. Hii ni kanuni kwa ajili ya mikutano yote ya watu wa Mungu.
34 Wanawake wanapaswa kunyamaza katika mikutano hii ya kanisa. Kama Sheria ya Musa inavyosema, hawaruhusiwi kuzungumza pasipo utaratibu bali wawe chini ya mamlaka. 35 Wakiwa na jambo wanalotaka kujua, wawaulize waume zao nyumbani. Ni aibu kwa mwanamke kuzungumza pasipo utaratibu katika mikutano ya kanisa.
36 Je, ni kutoka kwenu neno la Mungu lilikuja ama lilikuja kwa ajili yenu pekee? 37 Ikiwa yeyote kati yenu anafikiri kuwa yeye ni nabii au kwamba ana karama ya kiroho, anapaswa kuelewa kuwa ninachowaandikia ninyi nyote ni amri ya Bwana. 38 Ikiwa yeyote miongoni mwenu hatalikubali hili, basi hatakubaliwa.
39 Hivyo ndugu zangu, mzingatie sana kutabiri. Na msimzuie mtu yeyote kutumia karama ya kusema katika lugha zingine. 40 Lakini kila kitu kifanywe kwa usahihi na kwa utaratibu.
© 2017 Bible League International