Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Read the New Testament in 24 Weeks

A reading plan that walks through the entire New Testament in 24 weeks of daily readings.
Duration: 168 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
1 Wakorintho 2-3

Ujumbe Wangu: Yesu Kristo Msalabani

Wapendwa kaka na dada zangu katika Kristo, nilipokuja kwenu, niliwaambia siri ya kweli iliyofunuliwa na Mungu. Lakini sikuja kama mtu mwenye uwezo mkubwa wa kuongea au mwenye hekima ya juu. Nilipokuwa pamoja nanyi, niliamua kusahau kila kitu isipokuwa Yesu Kristo na kifo chake msalabani. Nilipokuja kwenu nilikuwa mdhaifu na mwenye hofu. Mafundisho na kuzungumza kwangu hakukuwa kwa maneno yenye hila. Lakini uthibitisho wa mafundisho yangu ilikuwa nguvu inayotolewa na Roho. Nilifanya hivi ili imani yenu iwe katika nguvu ya Mungu siyo katika hekima ya kibinadamu.

Hekima ya Mungu

Tunafundisha hekima kwa watu ambao macho yao yamefunguliwa ili waione hekima ya siri ya Mungu. Si hekima ya watawala wa ulimwengu huu wanaobatilika. Tunaisema hekima ya Mungu katika namna ambayo baadhi wanaweza kuiona na wengine hawawezi. Ni hekima iliyofichwa mpaka wakati huu na Mungu aliipanga hekima hii kabla ya kuumba ulimwengu, kwa ajili ya utukufu wetu. Hakuna mtawala yeyote wa ulimwengu huu aliyeielewa hekima hii. Ikiwa wangeielewa, wasingemwua Bwana wetu mkuu na mwenye utukufu mwingi msalabani. Lakini kama Maandiko yanavyosema,

“Hakuna aliyewahi kuona,
    hakuna aliyewahi kusikia,
hakuna aliyewahi kufikiri
    kuhusu kile ambacho Mungu amewaandalia wanaompenda.”(A)

10 Lakini Mungu ametuonesha mambo haya kupitia Roho.

Roho anaweza kuchunguza mambo yote. Anajua hata siri za ndani kabisa za Mungu. 11 Hakuna mtu anayejua mawazo ya mtu mwingine. Ni roho inayoishi ndani ya mtu huyo ndiyo inajua mawazo ya mtu huyo. Ndivyo ilivyo hata kwa Mungu, ni Roho wa Mungu peke yake ndiye anayeyajua mawazo ya Mungu. 12 Tulipokea Roho wa Mungu, si roho wa ulimwengu. Tulimpokea Roho wa Mungu ili tuweze kujua yote aliyotupa Mungu.

13 Tunapozungumza, hatutumii hoja tulizofundishwa na wenye hekima. Bali hoja tulizofundishwa na Roho. Tunatumia hoja za Roho kuelezea kweli za Roho. 14 Watu wasio na Roho wa Mungu, hawakubali vitu vinavyotoka kwa Roho. Hudhani kuwa ni vitu vya kipuuzi. Hawavielewi, kwa sababu havieleweki pasipo msaada wa Roho. 15 Aliye na Roho anaweza kujua mambo yote anayofundisha Roho. Na hatutahukumiwa kuwa na hatia na mtu yeyote.[a] 16 Kama Maandiko yanavyosema,

“Nani anaweza kujua anachokiwaza Bwana?
    Nani anaweza kumshauri?”(B)

Lakini sisi tumepewa tunawaza kama Kristo.

Walimu ni Watumishi tu wa Mungu

Ndugu zangu, nilipokuwa kwenu, sikuzungumza nanyi kama ninavyozungumza na watu wanaoongozwa na Roho. Nilizungumza nanyi kama watu wa kawaida wa duniani. Mlikuwa kama watoto katika Kristo. Mafundisho niliyowafundisha yalikuwa kama maziwa, siyo chakula kigumu. Nilifanya hivi kwa kuwa hamkuwa tayari kwa chakula kigumu. Na hata sasa hamjawa tayari. Bado hamwenendi katika Roho, mnaoneana wivu na mnabishana ninyi kwa ninyi kila wakati. Hii inaonesha kuwa bado mnazifuata tamaa zenu wenyewe. Mnaenenda kama watu wa kawaida wa ulimwengu huu. Mmoja wenu anasema, “Mimi ninamfuata Paulo,” na mwingine anasema, “Ninamfuata Apolo.” Mnaposema mambo kama haya, mnaenenda kama watu wa ulimwengu.

Je, Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Apolo na mimi si watumishi tu ambao Mungu alitutumia ili mmwamini Yesu Kristo. Kila mmoja wetu alifanya kazi aliyopewa na Bwana. Nilipanda mbegu na Apolo akamwagilia maji. Lakini Mungu ndiye aliyeiotesha na kuikuza. Hivyo aliyepanda na kuimwagilia si wa muhimu. Mungu ndiye wa muhimu, kwa sababu ndiye anayevifanya vitu viote vikue. Anayepanda na anayemwagilia maji wote wana nia moja. Na kila mmoja atalipwa kutokana na kazi yake yeye mwenyewe. Ninyi ni shamba la Mungu, ambamo tulifanya kazi pamoja kwa ajili yake.

Nanyi pia ni jengo la Mungu. 10 Nami kama mjenzi stadi nilijenga msingi wa nyumba hiyo kwa kutumia karama alizonipa Mungu. Wengine wanajenga pia katika msingi huo. Lakini kila mtu lazima awe mwangalifu kwa namna anavyojenga. 11 Yesu Kristo ndiye msingi uliokwishajengwa, na hakuna yeyote anayeweza kujenga msingi mwingine. 12 Watu wanaweza kujenga juu ya msingi huo kwa kutumia dhahabu, fedha, vito vya thamani, mbao, nyasi au majani. 13 Kila kazi atakayoifanya kila mtu itaonekana siku ya hukumu itakapofika, na itaonekana ilivyo mbaya au nzuri. Siku hiyo kila kazi ya mtu itajaribiwa kwa moto. 14 Mungu atampa thawabu mtu anayejenga juu ya msingi huu ikiwa kazi yake haitateketea kwa moto. 15 Lakini ikiwa itateketea atapata hasara. Lakini yeye mwenyewe ataokolewa, lakini itakuwa kama mtu anayeokolewa kutoka kwenye moto.

16 Hakika mnajua kuwa ninyi ni hekalu la Mungu na Roho wa Mungu anaishi ndani yenu. 17 Ndiyo, ninyi nyote kwa pamoja ni Hekalu la Mungu. Na yeyote atakayeliharibu Hekalu la Mungu ataadhibiwa na Mungu, kwa sababu Hekalu la Mungu ni mali yake yeye mwenyewe.

18 Msijidanganye. Yeyote anayejiona kuwa ana hekima kwa viwango vya ulimwengu huu, basi na awe mpumbavu. Hiyo ndiyo njia pekee itakayomfanya kuwa na hekima. 19 Ninasema hivi kwa sababu hekima ya ulimwengu huu ni upumbavu kwa Mungu. Kama Maandiko yanavyosema, “Mungu huwanasa katika mitego yao wenyewe wale wanaojidhania kuwa na hekima.”(C) 20 Pia Maandiko yanasema, “Bwana anajua mawazo ya wenye hekima. Anajua kuwa mawazo yao hayana maana.”(D) 21 Hivyo hakuna mtu yeyote duniani ambaye ninyi mnapaswa kujivunia. Kila kitu ni chenu: 22 Paulo, Apolo, Petro, ulimwengu, uzima, mauti, wakati uliopo na ujao, vyote hivi ni vyenu. 23 Ninyi ni wa Kristo, na Kristo ni wa Mungu.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International