Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Read the New Testament in 24 Weeks

A reading plan that walks through the entire New Testament in 24 weeks of daily readings.
Duration: 168 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Warumi 13-14

Kutii Watawala

13 Watiini watawala wa serikali. Hakuna anayeweza kutawala bila mamlaka ya Mungu. Mamlaka ya kutawala hutoka kwa Mungu. Hivyo yeyote anayekuwa kinyume na serikali hakika anakuwa kinyume na kitu ambacho Mungu amekiweka. Wale walio kinyume na serikali wanajiletea adhabu wao wenyewe. Watu wanaotenda mema hawawaogopi watawala. Bali wale wanaotenda mabaya ni lazima wawaogope watawala. Je, mnataka kuwa huru mbali na kuwaogopa hao? Basi mfanye yaliyo sahihi tu, nao watawasifu ninyi.

Watawala ni watumishi wa Mungu kwa ajili ya kuwasaidia ninyi. Lakini mkifanya yasiyo sahihi, mnayo sababu ya kuwa na woga. Hao wanayo mamlaka ya kuwaadhibu, na watayatumia mamlaka hayo. Wao ni watumishi wa Mungu ili wawaadhibu wale wanaofanya yale yasiyo sahihi. Kwa hiyo mnapaswa kuitii serikali, siyo tu kwa sababu mtaadhibiwa, bali kwa sababu mnajua kuwa ni jambo lililo sahihi kufanya hivyo.

Na hii ndiyo sababu mnalipa kodi. Watawala hawa wanapaswa kulipwa kwa ajili ya kutimiza wajibu wao wote walionao wa kutawala. Hakika wanatumika kwa ajili ya Mungu. Wapeni watu wote vile wanavyowadai. Kama wanawadai aina yoyote ya kodi, basi lipeni. Onesheni heshima kwa wale mnaopaswa kuwaheshimu. Na onesheni uadilifu kwa wale mnaopaswa kuwafanyia hivyo.

Kuwapenda Wengine Ndiyo Sheria Pekee

Msidaiwe chochote na mtu, isipokuwa mdaiwe upendo baina yenu. Mtu anayewapenda wengine anakuwa amefanya yote yanayoamriwa na sheria. Sheria inasema, “Usizini, usiue, usiibe, usitamani kitu cha mtu mwingine.”(A) Amri hizo zote na zingine hakika zinajumlishwa na kuwa kanuni moja tu, “Mpende jirani yako[a] kama unavyojipenda wewe mwenyewe.”(B) 10 Upendo hauwaumizi wengine. Hivyo kupenda ni sawa na kuitii sheria yote.

11 Nalisema hili kwa sababu mnajua kwamba tunaishi katika wakati ulio muhimu. Ndiyo, ni wakati wenu sasa kuamka kutoka usingizini. Wokovu wetu sasa uko karibu zaidi kuliko ilivyokuwa tulipoamini kwa mara ya kwanza. 12 Usiku karibu umekwisha. Na mchana karibu unaingia. Hivyo tunapaswa kuacha kufanya chochote kinachohusiana na giza. Tunapaswa kujiandaa kuupiga uovu kwa silaha za nuru. 13 Tunapaswa kuishi katika njia sahihi, kama watu walio wa mchana. Hatupaswi kuwa na tafrija za ovyo ama kulewa. Hatupaswi kujihusisha katika dhambi ya uzinzi au ya aina yoyote ya mwenendo usiofaa. Hatupaswi kusababisha mabishano au kuwa na wivu. 14 Bali, muwe kama Kristo Yesu katika kila jambo mnalolitenda,[b] ili watu watakapowaangalia, waweze kumwona yeye. Msifikirie namna ya kuridhisha matakwa ya udhaifu wa mwanadamu na tamaa zake.

Msiwakosoe Wengine

14 Iweni tayari kuwakubali wenye mashaka kuhusu yale ambayo waamini wanaweza kufanya. Tena msibishane nao kuhusu mawazo yao tofauti. Baadhi ya watu wanaamini kuwa wanaweza kula aina yoyote ya chakula,[c] lakini wale walio na mashaka wanakula mboga za majani tu. Wale wanaojua kuwa wanaweza kula chakula cha aina yoyote hawapaswi kujisikia kuwa ni bora kuliko wale wanaokula mboga za majani tu. Na wale wanaokula mboga za majani tu hawapaswi kuamua kuwa wale wanaokula vyakula vyote wanakosea. Mungu amewakubali. Huwezi kuwahukumu watumishi wa mtu mwingine. Hilo linamhusu bwana wao mwenyewe ikiwa watafaulu au watashindwa. Na watakubaliwa, kwa sababu Bwana yuko tayari kuwafanya wafaulu.

Watu wengine wanaweza kuamini kuwa siku moja ni ya muhimu zaidi kuliko nyingine. Na wengine wanaweza kuwa na uhakika kuwa siku zote ziko sawa. Kila mtu anapaswa kujihakikisha juu ya imani yake katika akili zake wenyewe. Wale wanaofikiri kuwa siku moja ni ya muhimu kuliko siku zingine wanafanya hivyo kwa ajili ya Bwana. Na wale wanaokula vyakula vya aina zote wanafanya hivyo kwa ajili ya Bwana. Ndiyo, wanamshukuru Mungu kwa ajili ya chakula. Na wale wanaokataa kula vyakula fulani wanafanya hivyo kwa ajili ya Bwana. Nao pia wanamshukuru Mungu.

Hatuishi au kufa kwa ajili yetu sisi wenyewe tu. Kama tukiishi, tunaishi kwa ajili ya Bwana. Na kama tukifa, tunakufa kwa ajili ya Bwana. Hivyo kuishi au kufa, sisi ni mali ya Bwana. Ndiyo sababu Kristo alikufa na kuishi tena ili awe Bwana juu ya wote waliokufa na wanaoishi.

10 Hivyo kwa nini unamhukumu kaka au dada yako katika familia ya Mungu? Au kwa nini unafikiri kuwa wewe ni bora kuliko wao? Sote tutasimama mbele za Mungu, naye atatuhukumu sisi sote. 11 Ndiyo, Maandiko yanasema,

“‘Hakika kama niishivyo’, asema Bwana,
    ‘kila mtu atapiga magoti mbele zangu,
    na kila mtu atasema kuwa mimi ni Mungu.’”(C)

12 Hivyo kila mmoja wetu ataeleza kuhusu matendo yake mbele za Mungu.

Msisababishe Wengine Wakatenda Dhambi

13 Hivyo tuache kuhukumiana sisi kwa sisi. Tuamue kutokufanya kitu ambacho kitasababisha matatizo kwa kaka au dada au kuathiri imani zao. 14 Najua kuwa hakuna chakula ambacho kwa namna yake chenyewe hakifai kuliwa. Bwana Yesu ndiye aliyenithibitisha juu ya jambo hilo. Lakini ikiwa mtu ataamini kuwa si sahihi kula chakula fulani, basi kwake yeye huyo hiyo haitakuwa sahihi akila chakula hicho.

15 Ikiwa utamuumiza kaka au dada yako kwa sababu ya chakula unachokula, hutakuwa unaifuata njia ya upendo. Kristo alikufa kwa ajili yao. Hivyo usiwaharibu kwa kula kitu wanachofikiri kuwa si sahihi kula. 16 Usiruhusu kile ambacho ni chema kwako kiwe kitu watakachosema ni kiovu. 17 Maisha katika ufalme wa Mungu siyo juu ya kile tunachokula na kunywa. Ufalme wa Mungu ni juu ya njia sahihi ya kuishi, amani na furaha. Vyote hii vinatoka kwa Roho Mtakatifu. 18 Yeyote anayemtumikia Kristo kwa kuishi namna hii anampendeza Mungu na ataheshimiwa na wengine.

19 Hivyo tujitahidi kwa kadri tuwezavyo kufanya kile kinacholeta amani. Tufanye kile kitakachomsaidia kila mtu kujengeka kiimani. 20 Msiruhusu kula vyakula kuiharibu kazi ya Mungu. Vyakula vyote ni sahihi kula, lakini ni makosa kwa yeyote kula kitu kinachomletea shida kaka au dada katika familia ya Mungu. 21 Ni heri kutokula nyama au kunywa divai au kufanya kitu chochote kinachoumiza imani ya kaka au dada yako.

22 Ilindeni imani yenu kuhusu mambo haya kama siri kati yenu na Mungu. Ni baraka kufanya kile unachofikiri ni sahihi bila kujihukumu mwenyewe. 23 Lakini ikiwa unakula kitu bila kuwa na uhakika kuwa ni sahihi, unakosea. Hii ni kwa sababu hukuamini kuwa ni sahihi. Na ukifanya chochote unachoamini kuwa si sahihi, hiyo ni dhambi.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International