M’Cheyne Bible Reading Plan
Paulo Akiwa Korintho
18 Baadaye, Paulo aliondoka Athene na kwenda katika mji wa Korintho. 2 Akiwa huko alikutana na Myahudi aliyeitwa Akila, aliyezaliwa katika jimbo la Ponto. Lakini yeye na mke wake aliyeitwa Prisila, walikuwa tu ndiyo wamehamia Korintho kutoka Italia. Waliondoka Italia kwa sababu Kaisari Klaudio alikuwa ametoa amri Wayahudi wote waondoke Rumi. Paulo alikwenda kuwatembelea Akila na Prisila. 3 Walikuwa watengenezaji wa mahema,[a] kama alivyokuwa Paulo, hivyo alikaa na kufanya kazi pamoja nao.
4 Kila siku ya Sabato Paulo alikwenda kwenye sinagogi na kuzungumza na Wayahudi na Wayunani, akijaribu kuwashawishi wamwamini Yesu. 5 Lakini baada ya Sila na Timotheo kufika kutoka Makedonia, Paulo alitumia muda wake wote kuuhubiri ujumbe wa Mungu kwa Wayahudi, akiwaeleza kuwa Yesu ndiye Masihi. 6 Lakini walimpinga Paulo na wakaanza kumtukana. Hivyo Paulo akakung'uta mavumbi kutoka kwenye nguo zake.[b] Akawaambia, “Msipookolewa, itakuwa makosa yenu ninyi wenyewe! Nimefanya yote ninayoweza kufanya. Baada ya hili nitawaendea watu wasio Wayahudi tu.”
7 Paulo aliondoka katika sinagogi na kuhamia nyumbani kwa Tito Yusto, mtu aliyekuwa anamwabudu Mungu wa Kweli, nyumba yake ilikuwa jirani na sinagogi. 8 Krispo aliyekuwa kiongozi wa sinagogi lile, pamoja na watu wote waliokuwa wanaishi nyumbani mwake walimwamini Bwana Yesu. Watu wengi katika mji wa Korintho walimsikiliza Paulo, wakaamini na wakabatizwa.
9 Wakati wa usiku, Paulo aliona maono. Bwana alimwambia, “Usiogope, na usiache kuzungumza na watu. 10 Niko pamoja nawe, na hakuna atakayeweza kukudhuru. Kuna watu wangu wengi katika mji huu.” 11 Paulo alikaa pale kwa mwaka mmoja na nusu akiwafundisha watu ujumbe wa Mungu.
Paulo Afikishwa Mbele ya Galio
12 Galio alipokuwa gavana wa Akaya, baadhi ya Wayahudi walikusanyika wakawa kinyume cha Paulo. Wakampeleka mahakamani. 13 Wakamwambia Galio, “Mtu huyu anawafundisha watu kumwabudu Mungu kwa namna ambavyo ni kunyume na sheria yetu!”
14 Paulo alikuwa tayari kuzungumza, lakini Galio aliwaambia Wayahudi, “Ningewasikiliza ikiwa malalamiko yenu yangehusu dhuluma au kosa jingine. 15 Lakini yanahusu maneno na majina tu, mabishano yanayohusu sheria zenu wenyewe. Ni lazima mtatue tatizo hili ninyi wenyewe. Sitaki kuwa mwamuzi wa jambo hili.” 16 Hivyo Galio akawafanya waondoke mahakamani.
17 Kisha wote kwa pamoja wakamkamata Sosthenesi, kiongozi wa sinagogi. Wakampiga mbele ya mahakama. Lakini Galio hakulijali hili pia.
Paulo Arudi Antiokia
18 Paulo alikaa na waamini kwa siku nyingi. Kisha aliondoka na kusafiri majini kwenda Shamu. Prisila na Akila walikuwa pamoja naye pia. Walipofika Kenkrea Paulo akanyoa nywele zake kwa sababu aliweka nadhiri[c] kwa Mungu. 19 Kisha walikwenda Efeso, ambako Paulo aliwaacha Prisila na Akila. Paulo alipokuwa Efeso alikwenda katika sinagogi na kuzungumza na Wayahudi. 20 Walimwomba akae kwa muda mrefu lakini alikataa. 21 Aliwaacha na kusema, “Nitarudi tena kwenu ikiwa Mungu atataka nirudi.” Na hivyo akaabili kwenda Efeso.
22 Alipofika Kaisaria, alikwenda Yerusalemu na kulitembelea kanisa pale. Baada ya hapo alikwenda Antiokia. 23 Alikaa Antiokia kwa muda kisha akaondoka akipita katika nchi za Galatia na Frigia. Alisafiri kutoka mji mmoja hadi mji mwingine katika mikoa hii, akiwasaidia wafuasi wa Yesu kuimarika katika imani yao.
Apolo Akiwa Efeso na Korintho
24 Myahudi aliyeitwa Apolo alikuja Efeso. Alizaliwa katika mji wa Iskanderia, alikuwa msomi aliyeyajua Maandiko vizuri. 25 Alikuwa amefundishwa kuhusu Bwana na daima alifurahia[d] kuwaeleza watu kuhusu Yesu. Alichofundisha kilikuwa sahihi, lakini ubatizo alioufahamu ni ubatizo aliofundisha Yohana. 26 Apolo alianza kuzungumza kwa ujasiri katika sinagogi. Prisila na Akila walipomsikia akizungumza, walimchukua wakaenda naye nyumbani mwao kisha wakamsaidia kuielewa njia ya Mungu vizuri zaidi.
27 Apolo alitaka kwenda Akaya. Hivyo waamini wa Efeso wakamsaidia. Waliwaandikia barua wafuasi wa Bwana waliokuwa Akaya wakiwaomba wampokee Apolo. Alipofika pale, alikuwa msaada mkubwa kwa wale waliomwamini Yesu kwa sababu ya neema ya Mungu. 28 Alibishana kwa ujasiri na Wayahudi mbele ya watu wote. Alithibitisha kwa uwazi kuwa wayahudi walikuwa wanakosea. Alitumia Maandiko kuonesha kuwa Yesu ndiye Masihi.
Yesu Aonya Kuhusu Wakati Ujao
(Mt 24:1-25; Lk 21:5-24)
13 Yesu alikuwa akiondoka katika eneo la Hekalu na moja ya wanafunzi wake akamwambia, “Mwalimu, tazama mawe haya yanavyopendeza na jinsi majengo haya yanavyopendeza!”
2 Yesu akamjibu, “Je, mnayaona majengo haya makubwa? Yote yatabomolewa. Kila jiwe litaporomoshwa hata chini. Hakuna jiwe lolote kati ya haya litakaloachwa mahali pake.”
3 Naye alipokuwa ameketi juu ya Mlima wa Mizeituni upande wa pili kuvuka Hekalu, Petro, Yakobo, Yohana na Andrea walimwuliza wakiwa faragha, 4 “Haya tuambie, ni lini mambo haya yatakapotokea? Ni ishara gani itakayoonesha ya kwamba yote yanakaribia kutimizwa?”
5 Yesu akaanza kuwaeleza, “Muwe waangalifu mtu asije akawadanganya. 6 Wengi watakuja huku wakilitumia Jina langu na kusema, ‘Mimi ndiye Masihi,’[a] nao watawadanganya wengi. 7 Mtasikia juu ya vita vinavyopiganiwa na mtasikia habari juu ya vita vingine vinavyoanza. Hata hivyo msishtushwe. Mambo hayo lazima yatokee, kabla ule mwisho wenyewe kufika. 8 Kwani taifa moja litapigana dhidi ya taifa lingine na ufalme mmoja utapigana dhidi ya ufalme mwingine. Yatatokea matetemeko mengi mahali pengi na kutakuwepo na njaa kali sehemu nyingi. Mambo haya yatakuwa ni mwanzo tu wa uchungu wa mama mzazi kabla ya mtoto kuzaliwa.
9 Hivyo mjihadhari! Wapo watu watakaowakamata na kuwapeleka mkahukumiwe kwa kuwa ninyi ni wanafunzi wangu. Watawapiga katika masinagogi yao. Mtalazimishwa kusimama mbele ya wafalme na watawala. Nanyi mtawaeleza habari zangu. 10 Kabla ya mwisho kufika, ni lazima kwanza habari Njema itangazwe kwa mataifa yote. 11 Wakati wowote watakapowakamata na kuwashitaki, msiwe na wasiwasi kujiandaa kwa yale mtakayoyasema, lakini myaseme yale mtakayopewa saa ile ile, kwa kuwa si ninyi mnaozungumza; bali, ni Roho Mtakatifu anayezungumza.
12 Na ndugu atamsaliti nduguye hata kuuawa, na baba atamsaliti mwanawe. Watoto nao watawaasi wazazi wao na hata kuwatoa wauawe. 13 Nanyi mtachukiwa na wote kwa sababu yangu. Lakini yeyote atakayevumilia hadi mwisho ataokoka.
14 Wakati mtakapoliona chukizo la uharibifu[b] likisimama mahali pasipotakiwa lisimame.” (Msomaji aelewe hii ina maana gani?[c]) “Kisha wale waliopo katika Uyahudi wakimbilie milimani. 15 Ikiwa mtu yupo katika paa la nyumba yake, asishuke chini na kuingia nyumbani mwake kuchukua kitu chochote. 16 Ikiwa mtu yupo shambani asirudi kuchukua vazi lake.
17 Wakati huo itakuwa hatari kwa wanawake walio waja wazito na wale wenye watoto wachanga. 18 Ombeni kwamba haya yasitokee wakati wa majira ya baridi. 19 Kwa kuwa taabu itakayotokea katika siku hizo itakuwa ile ambayo haijawahi kutokea tangu mwanzo pale Mungu alipoumba dunia hadi sasa. Na hakitatokea tena kitu kama hicho. 20 Kama Bwana asingelifupisha muda huo, hakuna ambaye angenusurika. Lakini yeye amefupisha siku hizo kwa ajili ya watu wale aliowateuwa.
21 Ikiwa mtu atawaambia, ‘Tazama, Kristo ni huyu hapa!’ ama ‘Ni yule pale!’ Usiliamini hilo. 22 Kwani Makristo wa uongo na manabii wa uongo watatokea, nao watafanya ishara na miujiza kuwadanganya watu ikiwezekana hata wale ambao Mungu amewachagua. 23 Kwa hiyo mjihadhari nimewaonya juu ya mambo haya kabla hayajatokea.
Yesu Atakaporudi Tena
(Mt 24:29-51; Lk 21:25-36; 19:12-13,40)
24 Lakini katika siku hizo, baada ya kipindi cha dhiki,
‘Jua litatiwa giza,
mwezi hautatoa mwanga,
25 nyota zitaanguka kutoka angani,
na mbingu yote itatikisika.’[d]
26 Ndipo watu watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni pamoja na nguvu kubwa na utukufu. 27 Baada ya hapo Mwana wa Adamu atawatuma malaika, na atawakusanya wateule wake kutoka kila upande wa dunia.
28 Jifunzeni somo hili kutoka katika mti wa mtini: Matawi yake yanaponyauka na kubeba majani, unajua kwamba kiangazi kimekaribia. 29 Vivyo hivyo, unapoona mambo haya yanaanza kutokea unajua kwamba muda umekaribia na umeshafika mlangoni. 30 Ninawaambieni ukweli: Kizazi hiki hakitapita kabla ya mambo haya yote hayajatokea. 31 Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
32 Hakuna anayejua wakiwemo malaika wa mbinguni ama Mwana bali baba peke yake lini siku au saa ile itakapowadia. 33 Mjihadhari; Kesheni! Kwani hamjui lini muda huo utafika.
34 Ni kama mtu anayeenda safarini na kabla ya kuondoka huiacha nyumba yake mikononi mwa watumishi wake. Kabla ya kuiacha nyumba yake anawaweka watumishi wake kusimamia kila mmoja akiwa na kazi yake maalumu. Kisha atamwamuru mlinzi mlangoni awe macho. 35 Vivyo hivyo ni lazima mjihadhari, kwa sababu hamjui ni muda gani mkuu wa nyumba atakuja; hamjui kama atakuja jioni, usiku wa manane, wakati jogoo anawika, au alfajiri. 36 Ikiwa atakuja ghafula, basi asiwakute mmelala. 37 Ninachowaambia, namwambia kila mmoja: ‘muwe tayari.’”
© 2017 Bible League International