M’Cheyne Bible Reading Plan
Baadhi ya Watu Wawa na Mashaka Kuhusu Mamlaka ya Yesu
(Mk 8:11-13; Lk 12:54-56)
16 Mafarisayo na Masadukayo walimjia Yesu. Walitaka kumjaribu, kwa hiyo wakamwomba awaoneshe muujiza kama ishara kutoka kwa Mungu.
2 Yesu akawajibu, “Ninyi watu mnapoona jua limezama, mnajua hali ya hewa itakavyokuwa. Anga ikiwa nyekundu, mnasema tutakuwa na hali ya hewa nzuri. 3 Na asubuhi, ikiwa anga ni nyeusi na nyekundu, mnasema mvua itanyesha. Hizi ni ishara za hali ya hewa. Mnaziona ishara hizi angani na mnajua zinamaanisha nini. Kwa namna hiyo hiyo, mnaona mambo yanayotokea sasa. Hizi ni ishara pia, lakini hamwelewi maana yake. 4 Ninyi watu mnaoishi sasa ni waovu na si waaminifu kwa Mungu. Ndiyo sababu kabla ya kuamini mnataka kuona muujiza. Lakini hakuna muujiza utakaofanyika ili kuwathibitishia kitu cho chote. Yona[a] ndiyo ishara pekee mtakayopewa.” Kisha Yesu akaondoka mahali pale.
Wafuasi Washindwa Kumwelewa Yesu
(Mk 8:14-21)
5 Yesu na wafuasi wake wakasafiri kwa kukatisha ziwa. Lakini wafuasi wakasahau kubeba mikate. 6 Yesu akawaambia, “Mwe waangalifu! Jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.”
7 Wafuasi wakajadiliana maana ya hili. Wakasema, “Amesema hivi kwa sababu tumesahau kubeba mikate?”
8 Yesu alipotambua kuwa wanajadiliana hili, akawauliza, “Kwa nini mnajadiliana kuhusu kutokuwa na mikate? Imani yenu ni ndogo. 9 Bado hamwelewi? Mnakumbuka mikate mitano waliyokula watu 5,000 na vikapu vingi mlivyojaza mikate iliyosalia? 10 Na mnakumbuka mikate saba waliyokula watu 4,000 na vikapu vingi mlivyojaza wakati ule? 11 Hivyo inakuwaje mnadhani kuwa mimi ninajali sana kuhusu mikate? Ninawaambia muwe waangalifu na mjilinde dhidi ya chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.”
12 Ndipo wafuasi wakaelewa Yesu alimaanisha nini. Hakuwa akiwaambia wajilinde na chachu inayotumika katika mikate bali wajilinde na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.
Petro Atambua Yesu ni Nani
(Mk 8:27-30; Lk 9:18-21)
13 Yesu alikwenda eneo la Kaisaria Filipi na akawauliza wafuasi wake, “Watu wanasema mimi ni nani[b]?”
14 Wakajibu, “Baadhi ya watu wanasema wewe ni Yohana Mbatizaji. Wengine wanasema wewe ni Eliya. Na wengine wanasema wewe ni Yeremia au mmoja wa manabii.”
15 Kisha Yesu akawauliza, “Na ninyi mnasema mimi ni nani?”
16 Simoni Petro akajibu, “Wewe ni Masihi, Mwana wa Mungu aliye hai.”
17 Yesu akajibu, “Umebarikiwa, Simoni mwana wa Yona. Hakuna aliyekufundisha hilo ila Baba yangu wa mbinguni ndiye amekuonesha mimi ni nani. 18 Hivyo ninakwambia, Wewe ni Petro. Na nitalijenga kanisa langu kwenye mwamba[c] huu. Nguvu ya mauti[d] haitaweza kulishinda kanisa langu. 19 Nitawapa funguo za Ufalme wa Mungu. Mnapohukumu hapa duniani, hukumu hiyo itakuwa hukumu ya Mungu. Mnapotamka msamaha hapa duniani, msamaha huo utakuwa msamaha wa Mungu.”[e]
20 Kisha Yesu akawaonya wafuasi wake wasimwambie mtu yeyote kuwa yeye ndiye Masihi.
Yesu Asema ni Lazima Afe
(Mk 8:31-9:1; Lk 9:22-27)
21 Kuanzia wakati huo Yesu alianza kuwaambia wafuasi wake kuwa ni lazima aende Yerusalemu. Alifafanua kuwa Viongozi wazee wa Kiyahudi, viongozi wa makuhani na walimu wa sheria watamfanya apate mateso kwa mambo mengi. Na aliwaambia wafuasi wake kuwa lazima auawe. Na siku ya tatu atafufuka kutoka kwa wafu.
22 Petro akamchukua Yesu na kwenda naye faragha mbali na wafuasi wengine. Akaanza kumkosoa Yesu kwa akasema, “Mungu akuepushe mbali na mateso hayo, Bwana! Hilo halitakutokea!”
23 Ndipo Yesu akamwambia Petro, “Ondoka kwangu, Shetani![f] Hunisaidii! Hujali mambo ya Mungu. Unajali mambo ambayo wanadamu wanadhani ni ya muhimu.”
24 Kisha Yesu akawaambia wafuasi wake, “Ikiwa yeyote miongoni mwenu anataka kuwa mfuasi wangu, ni lazima aache kujiwazia yeye mwenyewe na mahitaji yake. Ni lazima awe radhi kuubeba msalaba aliopewa na kunifuata mimi. 25 Yeyote kati yenu anayetaka kuokoa uhai wake, ataupoteza. Lakini ninyi mlioyaacha maisha yenu kwa ajili yangu mtaupata uzima wa kweli. 26 Haina maana kwenu ninyi kuupata ulimwengu wote, ikiwa ninyi wenyewe mtapotea. Mtu atalipa nini ili kuyapata tena maisha yake baada ya kuyapoteza? 27 Mimi, Mwana wa Adamu, nitarudi katika utukufu wa Baba yangu pamoja na Malaika. Na nitamlipa kila mtu kutokana na matendo yake. 28 Niaminini ninaposema wapo watu waliopo hapa watakaoishi mpaka watakaponiona nikija kama Mwana wa Adamu kutawala kama mfalme.”
© 2017 Bible League International