M’Cheyne Bible Reading Plan
Matatizo Mengi kwa waamini
12 Katika wakati huu huu, Mfalme Herode akaanza kuwatesa baadhi ya waamini waliokuwa sehemu ya kanisa. 2 Aliamuru Yakobo aliyekuwa kaka yake Yohana, auawe kwa upanga. 3 Herode alipoona kuwa Wayahudi wamelifurahia jambo hili, aliamua kumkamata Petro pia. Hii lilitokea katika kipindi cha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu. 4 Alimkamata Petro na kumfunga gerezani, ambako alilindwa na kundi la askari kumi na sita.[a] Herode alipanga kumleta Petro mbele ya watu ili ahukumiwe, lakini alisubiri mpaka baada ya sikukuu ya Pasaka. 5 Hivyo Petro aliwekwa gerezani lakini kanisa lilikuwa likiomba kwa Mungu bila kuacha kwa ajili yake.
Petro Atolewa Nje ya Gereza
6 Wakati wa usiku kabla ya siku ambayo Herode alipanga kumhukumu mbele ya watu, Petro, akiwa amefungwa minyororo miwili, alikuwa amelala katikati ya askari wawili. Na askari waliokuwa nje ya mlango walikuwa wanalinda gereza. 7 Ghafla malaika wa Bwana alikuwa amesimama pale, na chumba kilijaa mwanga. Malaika akamwamsha Petro kwa kumpiga upande, akasema, “Amka haraka!” Minyororo ikaanguka kutoka mikono mwa Petro. 8 Malaika akasema, “Vaa nguo na viatu vyako.” Petro alifanya kama alivyoambiwa. Kisha malaika akasema, “Vaa koti lako na unifuate.”
9 Hivyo malaika akatoka nje na Petro alimfuata. Hakujua kama kweli malaika alikuwa anafanya hili. Alidhani alikuwa anaona maono. 10 Petro na malaika wakavuka lindo la kwanza na lindo la pili. Kisha walifika kwenye lango la chuma lililowatenganisha na mji. Lango likafunguka. Baada ya kuvuka lango na kutembea umbali wa kama mtaa mmoja, malaika akatoweka ghafla.
11 Ndipo Petro akatambua kuwa haikuwa ndoto. Akawaza moyoni akisema, “Sasa ninajua kwamba Bwana hakika alimtuma malaika wake kwangu. Ameniokoa kutoka kwa Herode na kutoka kwenye mabaya yote ambayo Wayahudi walidhani yatanipata.”
12 Petro alipotambua hili, alikwenda nyumbani kwa Mariamu, mama yake Yohana, aliyeitwa Marko. Watu wengi walikuwa wamekusanyika pale wakiomba. 13 Petro alibisha kwenye mlango wa nje. Mtumishi wa kike aliyeitwa Rhoda alikuja ili afungue mlango. 14 Alipoitambua sauti ya Petro, alifurahi sana hata akasahau kufungua mlango. Akakimbilia ndani na kuliambia kundi, “Petro yuko mlangoni!” 15 Waamini wakamwambia, “Wewe una kichaa!” Lakini alipoendelea kusema kwamba ni kweli Petro yuko mlangoni. Waamini walisema, “Lazima atakuwa malaika wa Petro.”
16 Lakini Petro aliendelea kubisha mlangoni. Waamini walipoufungua mlango na kumwona, wakashangaa. 17 Petro akawafanyia ishara kwa mkono wake kuwaambia wanyamaze. Akawaeleza namna Bwana alivyomtoa nje ya gereza. Akasema, “Mwambieni Yakobo na ndugu wengine kilichotokea.” Kisha akawaacha na kwenda sehemu nyingine.
18 Siku iliyofuata askari walichanganyikiwa. Walijiuliza nini kimempata Petro. 19 Herode alimtafuta kila mahali lakini hakumpata. Hivyo aliwahoji walinzi na kuamuru wauawe.
Kifo cha Herode Agripa
Baadaye, Herode alihama kutoka Uyahudi na kwenda katika mji wa Kaisaria na kukaa huko kwa muda. 20 Herode aliwakasirikia sana watu katika miji ya Tiro na Sidoni. Lakini miji hii ilihitaji chakula kutoka katika nchi yake, hivyo baadhi yao walimjia wakitaka amani naye. Waliweza kumshawishi Blasto mtumishi binafsi wa Mfalme ili awasaidie.
21 Herode alichagua siku maalumu ya kukutana nao. Siku hiyo alivaa vazi zuri la kifalme. Aliketi kwenye kiti chake cha enzi na kuwahutubia watu. 22 Watu wakapaza sauti zao na kusema, “Hii ni sauti ya mungu, siyo mwanadamu!” 23 Herode hakumpa Mungu utukufu. Hivyo malaika wa bwana akampiga kwa ugonjwa. Akaliwa na minyoo ndani na kufa.
24 Ujumbe wa Mungu ulikuwa unasambaa, ukiwafikia watu wengi zaidi.
25 Baada ya Barnaba na Sauli kumaliza kazi yao Yerusalemu, walirudi Antiokia, walimchukua Yohana aliyeitwa Marko pamoja nao.
Sheria ya Mungu na Desturi za Kibinadamu
(Mt 15:1-20)
7 Mafarisayo na baadhi ya walimu wa Sheria waliokuja kutoka Yerusalemu walikusanyika mbele zake. 2 Hao wakawaona baadhi ya wanafunzi wake wakila chakula chao kwa mikono michafu (yaani bila kuosha mikono yao). 3 Kwani Mafarisayo na Wayahudi wengineo wote hawawezi kula isipokuwa wameosha mikono yao kwa njia maalumu, kulingana na desturi ya wazee. 4 Na wanaporudi kutoka sokoni, hawali chakula kwanza mpaka wamenawa. Na zipo desturi nyingi wanazozishika, kama vile kuosha vikombe, magudulia na mitungi ya shaba.[a]
5 Kwa hiyo Mafarisayo na walimu wa Sheria wakamwuliza Yesu, “Kwa nini wanafunzi wako hawafuati desturi za wazee, badala yake wanakula chakula chao kwa mikono isiyo safi?”
6 Yesu akawaambia, “Isaya alikuwa sahihi alipotoa unabii juu yenu enyi wanafiki, kama ilivyoandikwa:
‘Watu hawa huniheshimu kwa midomo yao,
lakini mioyo yao iko mbali nami.
7 Ibada wanayonitolea haifai,
kwa sababu wanawafundisha watu amri
zilizotungwa na wanadamu kana kwamba ndizo itikadi zao.’(A)
8 Mmezipuuza amri za Mungu, na mnashikilia desturi za binadamu.”
9 Yesu akawaambia, “Ninyi ni wazuri katika kuzikataa amri za Mungu ili kuanzisha desturi yenu. 10 Kwa mfano Musa alisema, ‘Mheshimu baba yako na mama yako,’(B) na yule mtu atakayesema maneno mabaya juu ya ‘mama au baba yake itampasa auwawe.’(C) 11 Lakini ikiwa mtu atamwambia baba au mama yake, ‘Nilikuwa na kitu ambacho ningekupa kikusaidie, lakini nimeahidi kukitoa wakfu kwa Mungu, nacho sasa ni kurbani.[b]’ 12 Kisha, anasema, hivyo hawezi kufanya kitu chochote kwa ajili ya kumsaidia baba au mama yake. 13 Kwa hiyo unalifanya neno la Mungu kuwa batili kwa desturi mlizozirithishana. Na mnafanya mambo mengi mengine yanayofanana na hayo.”
14 Yesu akaliita lile kundi kwake na kuwaambia, “Kila mmoja anisikilize na kunielewa. 15 Hakuna kitu kilicho nje ya mtu kinachoweza kumchafua kwa kumwingia. Lakini vitu vinavyotoka ndani ya mtu ndivyo vinavyomchafua.” 16 [c]
17 Na alipoliacha lile kundi na kuingia ndani ya nyumba, wanafunzi wake wakamwuliza juu ya fumbo lile. 18 Na akawaambia, “Hata nanyi hamuelewi pia? Je, hamuelewi ya kuwa hakuna kinachomwingia mtu kutoka nje kinachoweza kumchafua mtu? 19 Kwa sababu hakiingii ndani ya moyo wake bali kinaenda tumboni mwake na kasha kinatoka na kwenda chooni.” Kwa kuyasema hayo alivifanya vyakula vyote kuwa safi.
20 Na Yesu akasema, “Ni kile kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomchafua. 21 Kwani mambo hayo yote mabaya hutoka ndani ya moyo wa mwanadamu; yaani mawazo mabaya na uasherati, wizi, mauaji, 22 zinaa, ulafi, kufanya mabaya kwa watu, udanganyifu, kufanya uhuni, wivu, kutukana, kujivuna, na ujinga. 23 Mambo haya yote yanatoka ndani ya mtu nayo ndiyo yanayomfanya asikubalike kwa Mungu.”
Yesu Amsaidia Mwanamke Asiye Myahudi
(Mt 15:21-28)
24 Yesu akaondoka mahali pale na kuenda katika eneo lililozunguka Tiro. Aliingia katika nyumba na hakutaka mu yeyote ajue hilo, lakini hakuweza kufanya siri kuwepo kwake. 25 Mwanamke mmoja ambaye binti yake alikuwa na pepo mchafu mara moja akasikia juu ya Yesu hivyo alimwijia na kuanguka chini yake. 26 Mwanamke huyo alikuwa ni Mgiriki na siyo Myahudi, na alikuwa amezaliwa Foeniki ya Shamu. Yeye alimsihi amfukuze pepo yule kutoka kwa binti yake.
27 Yesu akamwambia, “Kwanza waache watoto watosheke, kwani sio haki kuwanyanganya watoto mkate wao na kuwapa mbwa.”
28 Lakini yeye akajibu, “Bwana hata mbwa walio chini ya meza wanakula mabaki ya chakula cha watoto.”
29 Kisha Yesu akamwambia, “kwa majibu haya unaweza kwenda nyumbani kwa amani: pepo mbaya amekwisha mtoka binti yako.”
30 Kwa hiyo akaenda nyumbani na akamkuta amelala akipumzika kitandani, na yule pepo tayari amekwisha mtoka.
Yesu Amponya Asiyesikia
31 Yesu akarudi kutoka katika eneo kuzunguka jiji la Tiro na akapita katika jiji la Sidoni hadi Ziwa Galilaya akipita katika jimbo la Dekapoli. 32 Pale watu wengine wakamletea mtu asiyeweza kusikia na tena aliyesema kwa shida. Nao wakamwomba Yesu amwekee mikono yake na kumponya.
33 Yesu akamchukua pembeni, kutoka katika kundi, na akaweka vidole vyake ndani ya masikio yake. Kisha Yesu akatema mate na kuugusa ulimi wa yule mtu. 34 Akaangalia juu mbinguni, akapumua na kumwambia “Efatha” yaani, “Funguka!” 35 Mara masikio ya mtu yule yakafunguka, na ulimi wake ukawa huru, na akaanza kuzungumza, vizuri.
36 Lakini kadiri jinsi alivyowaamuru wasimwambie mtu ndivyo walivyozidi kueneza habari hiyo. 37 Na watu wakashangazwa kabisa na kusema, “Yesu amefanya kila kitu vyema. Kwani amewafanya wale wasiosikia kusikia na wasiosema kusema.”
© 2017 Bible League International