M’Cheyne Bible Reading Plan
8 1-3 Sauli aliridhia kuwa kuuawa kwa Stefano lilikuwa jambo jema. Baadhi ya wacha Mungu walimzika Stefano, wakaomboleza na kumlilia kwa sauti kuu.
Matatizo Kwa waamini
Kuanzia siku hiyo Wayahudi walianza kulitesa sana kanisa na waamini katika mji wa Yerusalemu. Sauli pia alijaribu kuliharibu kanisa. Aliingia katika nyumba za waamini, akawaburuta wanaume na wanawake, na kuwafunga gerezani. Waamini wote walikimbia kutoka Yerusalemu, mitume peke yao ndiyo walibaki. Waamini walikwenda mahali tofauti tofauti katika Uyahudi na Samaria. 4 Walitawanyika kila mahali, na kila walikokwenda waliwahubiri watu Habari Njema.
Filipo Ahubiri Katika Samaria
5 Filipo[a] alikwenda katika mji mkuu wa jimbo la Samaria na kuwahubiri watu kuhusu Masihi. 6 Watu wa Samaria walimsikiliza Filipo na kuona miujiza aliyotenda. Wote walisikiliza kwa makini yale aliyosema. 7 Watu wengi miongoni mwao walikuwa na mapepo, lakini Filipo aliyakemea mapepo na yaliwatoka watu. Mapepo yalipiga kelele nyingi yalipokuwa yanawatoka watu. Walikuwepo pia watu wengi waliopooza na walemavu wa miguu pale. Filipo aliwaombea na wote walipona. 8 Kulikuwa furaha kubwa katika mji ule wa Samaria siku ile!
9 Mtu mmoja aliyeitwa Simoni alikuwa anaishi katika mji huo. Kabla Filipo hajaenda huko, Simoni alikuwa akifanya uchawi na kuwashangaza watu wote wa Samaria. Alijigamba na kujiita mtu mkuu. 10 Watu wote, kuanzia mdogo hadi mkubwa, waliamini yale aliyosema Simoni. Walisema, “Mtu huyu ndiye anayeitwa ‘Nguvu Kuu ya Mungu.’” 11 Simoni aliwashangaza watu kwa muda mrefu kwa uchawi wake na watu wote wakawa wafuasi wake. 12 Lakini Filipo alipowahubiri watu Habari Njema kuhusu Ufalme wa Mungu na Nguvu za Yesu Kristo. Wanaume na wanawake waliamini alichosema Filipo na wakabatizwa. 13 Simoni mwenyewe aliamini, na baada ya kubatizwa, alikaa karibu na Filipo. Alipoona miujiza na matendo makuu ya ajabu yaliyofanyika kupitia Filipo, alishangaa.
14 Mitume mjini Yerusalemu, waliposikia kuwa watu wa Samaria wameupokea Ujumbe wa Mungu, waliwatuma Petro na Yohana kwenda kwa watu wa Samaria. 15 Petro na Yohana walipofika, waliomba ili Roho Mtakatifu awashukie waamini wa Samaria. 16 Watu hawa walikuwa wamebatizwa katika jina la Bwana Yesu, lakini Roho Mtakatifu alikuwa bado hajamshukia hata mmoja wao. Na hii ndiyo sababu Petro na Yohana waliomba. 17 Mitume hawa wawili walipoweka mikono yao juu ya watu, Roho Mtakatifu aliwashukia.
18 Simoni aliyekuwa mchawi alipoona Roho Mtakatifu anatolewa kwa watu kwa kuweka mikono juu yao. Aliwapa pesa mitume. 19 Akasema, “Nipeni na mimi nguvu hii ili nitakapoweka mikono yangu juu ya mtu yeyote, atampata Roho Mtakatifu.”
20 Petro akamwambia Simoni, “Wewe pamoja na pesa zako mwangamie kwa sababu unadhani unaweza kununua karama kutoka kwa Mungu kwa pesa. 21 Huwezi kushirikiana nasi katika kazi hii. Moyo wako si safi mbele za Mungu. 22 Badili moyo wako! Achana na mawazo haya maovu na umwombe Bwana. Yumkini atakusamehe! 23 Kwa kuwa ninaona umejaa wivu mwingi nawe ni mfungwa wa uovu.”
24 Simoni akajibu, “Niombeeni kwa Bwana, ili haya uliyosema yasinipate.”
25 Ndipo wale mitume wawili waliwaambia watu waliyoona Yesu akitenda. Wakawaambia ujumbe wa Bwana. Kisha wakarudi Yerusalemu. Wakiwa njiani kurudi, walipitia katika miji mingi ya Wasamaria na kuwahubiri watu Habari Njema.
Filipo Amfundisha Mtu Kutoka Ethiopia
26 Malaika wa Bwana alimwambia Filipo, “Jiandae na uende kusini katika barabara ya jangwani inayoteremka kutoka Yerusalemu kwenda Gaza.”
27 Filipo alijiandaa na kwenda. Akiwa njiani alimwona mwanaume kutoka Ethiopia. Alikuwa towashi na ofisa muhimu wa Kandake, malkia wa Ethiopia. Alikuwa na mweka hazina mkuu wa malkia. Mtu huyu alikuwa amekwenda Yerusalemu kuabudu. 28 Na alikuwa anarudi Ethiopia. Alikuwa ameketi katika gari lake la kukokotwa na farasi akiwa anasoma kitabu cha nabii Isaya.
29 Roho Mtakatifu akamwambia Filipo, “Nenda kwenye gari hilo na uwe karibu yake.” 30 Hivyo Filipo akaenda karibu na gari, akamsikia mtu yule akisoma kutoka katika kitabu cha nabii Isaya. Filipo akamwuliza, “Unaelewa unachosoma?”
31 Yule mtu akajibu, “Nitaelewaje? Ninahitaji mtu wa kunifafanulia.” Ndipo akamwomba Filipo apande garini na aketi pamoja naye. 32 Sehemu ya Maandiko aliyokuwa anasoma ilikuwa hii:
“Alikuwa kama kondoo
anayepelekwa kwa mchinjaji.
Alikuwa kama mwana kondoo asivyopiga kelele
anapokatwa manyoya yake.
Hakusema kitu.
33 Alidhalilishwa,
na kunyimwa haki zake zote.
Maisha yake duniani yamekoma.
Hivyo hakutakuwa simulizi yoyote kuhusu wazaliwa wake.”(A)
34 Afisa[b] akamwambia Filipo, “Tafadhali niambie, nabii anazungumza kuhusu nani? Anazungumza kuhusu yeye mwenyewe au mtu mwingine?” 35 Filipo akaanza kuzungumza. Alianzia na Andiko hili na kumwambia mtu yule Habari Njema kuhusu Yesu.
36 Walipokuwa wanasafiri waliyakuta maji mahali fulani. Afisa akasema, “Tazama! Hapa kuna maji! Nini kinanizuia nisibatizwe?” 37 [c] 38 Ndipo Afisa akaamuru gari lake lisimame. Wote wawili, Filipo na Afisa, wakatelemka wakaingia kwenye maji na Filipo akambatiza towashi. 39 Walipotoka kwenye maji, Roho wa Bwana akamchukua Filipo; afisa hakumwona Filipo tena. Afisa aliendelea na safari yake kurudi nyumbani, akiwa mwenye furaha sana. 40 Lakini Filipo alionekana katika mji ulioitwa Azoto. Alikuwa akienda kwenye mji wa Kaisaria. Aliwahubiri watu Habari Njema katika miji yote wakati anasafiri kutoka Azoto kwenda Kaisaria.
Yesu Amponya Mtu Siku ya Sabato
(Mt 12:9-14; Lk 6:6-11)
3 Kwa mara nyingine tena Yesu alikwenda kwenye sinagogi. Huko alikuwepo mtu aliyekuwa na mkono uliolemaa. 2 Watu wengine walikuwa wakimwangalia Yesu kwa karibu sana. Walitaka kuona ikiwa angemponya mtu yule siku ya Sabato,[a] ili wapate sababu ya kumshitaki. 3 Yesu akamwambia yule mtu aliyekuwa na mkono uliolemaa, “Simama mbele ili kila mtu akuone.”
4 Ndipo Yesu akawaambia, “Je, ni halali kutenda mema ama kutenda mabaya siku ya Sabato? Je, ni halali kuyaokoa maisha ya mtu fulani ama kuyapoteza?” Lakini wao walikaa kimya.
5 Yesu akawatazama wote waliomzunguka kwa hasira lakini alihuzunika kwa sababu waliifanya mioyo yao kuwa migumu. Akamwambia mtu yule “nyosha mkono wako”, naye akaunyosha, na mkono wake ukapona. 6 Kisha Mafarisayo wakaondoka na papo hapo wakaanza kupanga njama pamoja na Maherode kinyume cha Yesu kutafuta jinsi gani wanaweza kumuua.
Wengi Wamfuata Yesu
7 Yesu akaondoka pamoja na wanafunzi wake hadi Ziwa Galilaya, na kundi kubwa la watu kutoka Galilaya likawafuata, pamoja na watu kutoka Uyahudi, 8 Yerusalemu, Idumea, na katika maeneo yote ng'ambo ya Mto Yordani na yale yanayozunguka Tiro na Sidoni. Lilikuwa kundi kubwa sana la watu. Wote walimjia Yesu kwa sababu walikuwa wamesikia mambo aliyokuwa anafanya.
9 Kwa sababu ya kundi, aliwaambia wanafunzi wake, kumtayarishia mashua mdogo, ili kwamba wasiweze kumsonga na kumbana. 10 Yesu alikuwa ameponya watu wengi. Hivyo wote wale waliokuwa na magonjwa waliendelea kujisogeza mbele kumwelekea ili wamguse. 11 Kila mara pepo wachafu walipomwona Yesu, walianguka chini mbele yake, na kulia kwa sauti, “Wewe ni Mwana wa Mungu!” 12 Lakini yeye aliwaamuru kila mara wasimwambie mtu yeyote yeye ni nani.
Yesu Achagua Wanafunzi Wake Kumi na Wawili
(Mt 10:1-4; Lk 6:12-16)
13 Kisha Yesu akapanda juu kwenye vilima na akawaita baadhi ya wanafunzi wake, hasa wale aliowataka wajiunge naye pale. 14 Akawachagua kumi na wawili, ambao aliwaita mitume. Aliwachagua ili waambatane pamoja naye, na kwamba aweze kuwatuma sehemu mbalimbali kuhubiri ujumbe wa neno la Mungu. 15 Pia aliwapa mamlaka ya kufukuza mashetani toka kwa watu. 16 Yafuatayo ni majina ya mitume kumi na wawili aliowateuwa Yesu:
Simoni ambaye Yesu alimwita Petro,
17 Yakobo mwana wa Zebedayo na Yohana ndugu yake (ambao wote Yesu aliwaita Boanergesi), yaani “wana wa ngurumo yenye radi”,
18 Andrea,
Filipo,
Bartholomayo,
Mathayo,
Thomaso,
Yakobo mwana wa Alfayo,
Thadayo,
Simoni Mzelote
19 na Yuda Iskariote,[b] ambaye ndiye aliyemsaliti Yesu.
Nguvu ya Yesu Inatoka kwa Mungu
(Mt 12:22-32; Lk 11:14-23; 12:10)
20 Kisha Yesu akaenda nyumbani. Kwa mara nyingine tena umati wa watu ukakusanyika, kiasi kwamba Yesu na wanafunzi wake hawakupata nafasi ya kula. 21 Familia ya Yesu ilipoyasikia haya, walikwenda kumchukua kwa sababu watu walisema amerukwa na akili.
22 Walimu wa Sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu walikuwa wanasema, “Yeye ana Beelzebuli[c] ndani yake! Kwani anafukuza mashetani kwa nguvu ya mkuu wa mashetani!”
23 Yesu akawaita na kuanza kuzungumza nao kwa kulinganisha: “Inawezekanaje Shetani ambaye ni roho mchafu kufukuza mashetani? 24 Ikiwa basi ufalme utagawanyika katika sehemu mbili zinazopingana zenyewe kwa zenyewe, ufalme huo hautaendelea. 25 Vivyo hivyo ufalme wa Shetani ukigawanyika naye akapigana dhidi ya pepo wake wabaya, basi huo utakuwa ndio mwisho wa ufalme wake. Pia ikiwa nyumba itapingana yenyewe kwa yenyewe, nyumba hiyo haitaweza kusalimika. 26 Kwa hiyo ikiwa Shetani atajipinga mwenyewe na kugawanyika basi hataweza kuendelea na huo utakuwa mwisho wake.
27 Hakika, hakuna anayeweza kuingia kwenye nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuzichukua mali zake bila kwanza kumfunga mtu huyo mwenye nguvu; hapo ndipo atakapoweza kuiba katika nyumba hiyo.
28 Ninawaambia ukweli: Watu wanaweza kusamehewa dhambi zao zote na maneno yao yenye matusi kwa Mungu. 29 Lakini yeyote atakayemtukana Roho Mtakatifu hatasamehewa kabisa. Kwa sababu mtu anayefanya hivyo atakuwa na hatia ya dhambi isiyosamehewa milele.”
30 Yesu alisema haya kwa sababu walimu wa sheria walikuwa wanasema, “Yeye ana pepo mchafu ndani yake.”
Wafuasi wa Yesu ni Familia Yake Halisi
(Mt 12:46-50; Lk 8:19-21)
31 Kisha mama yake Yesu na nduguze wakaja. Wao walisimama nje na wakamtuma mtu aende kumwita ndani. 32 Humo lilikuwepo kundi lililoketi kumzunguka, lakini wao wakamwambia, “Tazama! Mama yako, kaka zako na dada zako wako[d] nje wanakusubiri.”
33 Yesu akauliza, “Mama yangu ni nani na kaka zangu ni akina nani?” 34 Yesu akawatazama wale walioketi kumzunguka na akasema “Hapa yupo mama yangu na wapo kaka zangu na dada zangu! 35 Yeyote anayeyafanya mapenzi ya Mungu ndiye kaka yangu, dada yangu, na mama yangu.”
© 2017 Bible League International