Read the Gospels in 40 Days
Wanawali Kumi
25 Nyakati hizo, ufalme wa Mungu utafanana na wanawali kumi waliokwenda kusubiri kuwasili kwa bwana arusi wakiwa na taa zao. 2 Watano kati yao walikuwa na hekima, na watano walikuwa wajinga. 3 Wanawali wajinga walichukua taa zao bila ya kubeba mafuta ya ziada kwa ajili ya taa zao. 4 Wanawali wenye hekima walichukua taa zao pamoja na mafuta ya ziada kwa ajili ya taa zao katika chupa. 5 Bwana arusi alipochelewa sana, walichoka na wote wakasinzia.
6 Usiku wa manane ulipofika, ikatangazwa, ‘Bwana arusi anakuja! Njooni mumlaki!’
7 Wasichana wote waliamka. Wakatayarisha taa zao. 8 Lakini wanawali wajinga wakawaambia wanawali wenye hekima, ‘Tupeni mafuta kiasi kwa sababu mafuta katika taa zetu yamekwisha.’
9 Wanawali wenye hekima wakajibu, ‘Hapana! Mafuta tuliyonayo hayatatutosha sisi sote. Lakini nendeni kwa wauza mafuta mkanunue.’
10 Hivyo wanawali wajinga wakaenda kununua mafuta. Walipoondoka, bwana arusi akafika. Wanawali waliokuwa tayari wakaingia kwenye sherehe ya arusi pamoja na bwana arusi. Kisha mlango ukafungwa.
11 Baadaye wanawali waliokwenda kununua mafuta wakarudi. Wakasema, ‘bwana, bwana! Fungua mlango tuingie.’
12 Lakini bwana arusi akajibu, ‘Kwa hakika hapana! Wala siwajui ninyi.’
13 Hivyo iweni tayari kila wakati. Hamjui siku wala muda ambao Mwana wa Adamu atakuja.
Simulizi Kuhusu Watumishi Watatu
(Lk 19:11-27)
14 Pia, ufalme wa Mungu unafanana na mtu aliyekuwa akiondoka nyumbani kwake kusafiri safari ndefu. Aliwaita watumishi wake na kuwaweka kuwa wasimamizi wa mali zake. 15 Alimgawia kila mtumishi kiasi cha mali atakachosimamia. Alimpa mmoja talanta[a] tano. Alimpa mtumishi mwingine talanta mbili na akampa mtumishi wa tatu talanta moja. Kisha akaondoka. 16 Mtumishi aliyepewa talanta tano alikwenda akazifanyia biashara na talanta zile tano zikazaa talanta tano zingine. 17 Mtumishi aliyepewa talanta mbili alifanya vivyo hivyo. Mtumishi huyo alizifanyia biashara talanta mbili alizopewa na zikazaa talanta mbili zingine. 18 Lakini mtumishi aliyekabidhiwa talanta moja, alikwenda akachimba shimo kisha akaifukia talanta moja aliyopewa na bwana wake.
19 Baada ya muda mrefu kupita bwana wao alirudi. Aliwauliza watumishi wake walizifanyia nini talanta alizowaachia. 20 Mtumishi aliyekabidhiwa talanta tano alimletea bwana wake talanta tano alizomwachia na talanta zingine tano zaidi. Mtumishi akamwambia bwana wake, ‘Bwana, uliniamini ukaniachia talanta tano kuzitunza, hivyo nilizifanyia biashara na kupata talanta tano zaidi.’
21 Bwana wake akajibu, ‘Ulifanya vyema. Wewe ni mtumishi mwema unayeweza kuaminiwa. Ulifanya vizuri kwa kiasi kidogo hicho cha pesa. Hivyo nitakufanya kuwa msimamizi wa mambo makuu. Njoo usherehekee pamoja nami.’
22 Kisha mtumishi aliyepewa talanta mbili akaja kwa bwana wake. Akasema, ‘Bwana ulinipa talanta mbili ili nizitunze. Nilizifanyia biashara talanta hizi mbili na nimepata zingine mbili zaidi.’
23 Bwana wake akajibu, ‘Ulifanya vyema. Wewe ni mtumishi mwema unayeweza kuaminiwa. Ulifanya vizuri kwa kiasi kidogo hicho cha pesa. Hivyo nitakufanya kuwa msimamizi wa mambo makuu. Njoo usherehekee pamoja nami.’
24 Ndipo mtumishi aliyeachiwa talanta moja akaja kwa bwana wake. Akasema, ‘Bwana, nilijua wewe ni mkorofi sana. Unavuna usichopanda. Unakusanya mazao mahali ambapo hukupanda mbegu yoyote. 25 Hivyo niliogopa. Nilienda nikaificha talanta yako ardhini. Hii hapa ni ile talanta moja ya fedha uliyonipa.’
26 Bwana wao akamjibu, ‘Wewe ni mtumishi mbaya na mvivu! Unasema kwamba ulijua ninavuna nisichopanda na ninakusanya mazao ambayo sikupanda mbegu yo yote. 27 Hivyo ungeweka pesa yangu benki. Kisha, wakati nitakaporudi ningepata talanta yangu pamoja na faida ambayo ingezalishwa na talanta yangu.’
28 Hivyo bwana wao akawaambia watumishi wake wengine, ‘Mnyang'anyeni talanta moja mtumishi huyo na kumpa mtumishi mwenye talanta kumi. 29 Kila aliyezalisha faida atapata zaidi. Atakuwa na vingi kuzidi mahitaji yake. Lakini wale wasiotumia walivyonavyo kuleta faida watanyang'anywa kila kitu.’ 30 Kisha bwana wao akasema, ‘Mtupeni nje, gizani mtumishi huyo asiyefaa, ambako watu watalia na kusaga meno kwa maumivu.’
Yesu, Mwana wa Adamu Atawahukumu Watu Wote
31 Mwana wa Adamu atakuja akiwa katika utukufu wake, pamoja na malaika wote. Ataketi kwenye kiti chake cha enzi akiwa mfalme. 32 Watu wote wa ulimwenguni watakusanywa mbele zake, kisha atawagawa katika makundi mawili. Itakuwa kama mchungaji anavyowatenga kondoo kutoka katika kundi la mbuzi. 33 Atawaweka kondoo upande wake wa kuume na mbuzi upande wa kushoto.
34 Kisha mfalme atawaambia walio upande wake wa kuume, ‘Njooni, baba yangu ana baraka kuu kwa ajili yenu. Ufalme alioahidi ni wenu sasa. Uliandaliwa kwa ajili yenu tangu dunia ilipoumbwa. 35 Ni wenu kwa sababu nilipokuwa na njaa, mlinipa chakula. Nilipokuwa na kiu, mlinipa maji ya kunywa. Nilipokosa mahali pa kukaa, mlinikaribisha katika nyumba zenu. 36 Nilipokosa nguo, mlinipa mavazi ya kuvaa. Nilipokuwa mgonjwa, mlinijali. Nilipofungwa gerezani, mlikuja kunitembelea.’
37 Kisha wenye haki watajibu, ‘Bwana, ni lini tulikuona ukiwa na njaa tukakupa chakula? Lini tulikuona una kiu tukakupa maji ya kunywa? 38 Lini tulikuona huna mahali pa kukaa tukakukaribisha katika nyumba zetu? Lini tulikuona huna nguo za kuvaa na tukakuvisha? 39 Lini tulikuona unaumwa au uko gerezani tukaja kukuona?’
40 Kisha mfalme atajibu, ‘Ukweli ni kuwa, kila mlichowafanyia mmojawapo wa watu wangu hapa, hata wale walioonekana kuwa si watu wa thamani, mlinifanyia mimi pia.’
41 Kisha mfalme atawaambia walio upande wake wa kushoto, ‘Ondokeni kwangu. Mungu amekwisha amua kuwa mtaadhibiwa. Nendeni katika moto uwakao milele, moto ulioandaliwa kwa ajili ya yule Mwovu na malaika zake. 42 Ondokeni kwa sababu nilipokuwa na njaa, hamkunipa chakula nile. Nilipokuwa na kiu, hamkunipa maji ya kunywa. 43 Nilipokosa mahali pa kukaa, hamkunikaribisha katika nyumba zenu. Nilipokosa nguo za kuvaa, hamkunipa nguo za kuvaa. Nilipokuwa mgonjwa au mfungwa gerezani hamkunijali.’
44 Ndipo watu hao watajibu, ‘Bwana ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu? Lini tulikuona huna mahali pa kukaa? Au ni lini tulikuona huna nguo au mgonjwa au ukiwa gerezani? Tuliona haya yote lini na hatukukusaidia?’
45 Mfalme atajibu, ‘Ukweli ni kuwa, chochote mlichokataa kumfanyia mmojawapo wa watu wangu hapa, hata wale walioonekana kuwa si wa muhimu, mlikataa kunifanyia mimi.’
46 Ndipo watu hawa watakapondolewa ili kuadhibiwa milele. Lakini wenye haki watakwenda kuyafurahia maisha ya milele.”
Mpango wa Kumwua Yesu
(Mk 14:1-2; Lk 22:1-2; Yh 11:45-53)
26 Yesu alipomaliza akasema haya yote, akawaambia wafuasi wake, 2 “Mnajua kuwa kesho kutwa ni Pasaka. Siku hiyo Mwana wa Adamu atakabidhiwa kwa maadui zake ili auawe msalabani.”
3 Ndipo viongozi wa makuhani na wazee walikutana katika nyumba ya Kayafa kuhani mkuu. 4 Katika mkutano huo walitafuta njia ya kumkamata na kumwua Yesu kwa siri pasipo mtu yeyote kujua. 5 Wakasema, “Hatuwezi kumkamata Yesu wakati wa sherehe ya Pasaka. Hatutaki watu wakasirike na kusababisha vurugu.”
Mwanamke Ampa Yesu Heshima
(Mk 14:3-9; Yh 12:1-8)
6 Yesu alipokuwa Bethania katika nyumba ya Simoni aliyekuwa na ugonjwa mbaya sana wa ngozi. 7 Mwanamke alimwendea, akiwa na chupa yenye manukato ya thamani kubwa. Yesu akiwa anakula, mwanamke huyo akamwagia manukato hayo kichwani.
8 Wanafunzi walipomwona mwanamke akifanya hivi walimkasirikia. Walisema, “Kwa nini kuharibu manukato hayo? 9 Yangeuzwa na pesa nyingi ingepatikana, na pesa hiyo wangepewa maskini.”
10 Lakini Yesu alijua kilichokuwa kinaendelea. Akasema, “Kwa nini mnamsumbua mwanamke huyu? Amenifanyia jambo zuri sana. 11 Mtaendelea kuishi na maskini siku zote.[b] Lakini ninyi hamtakuwa nami siku zote. 12 Mwanamke huyu amenimwagia manukato. Amefanya hivi kuniandaa kwa ajili ya mazishi baada ya kufa. 13 Habari Njema itahubiriwa kwa watu wote ulimwenguni. Na ninaweza kuwathibitishia kuwa kila mahali ambako Habari Njema zitahubiriwa, jambo alilofanya mwanamke huyu litahubiriwa pia, na watu watamkumbuka.”
Yuda Akubali Kuwasaidia Adui wa Yesu
(Mk 14:10-11; Lk 22:3-6)
14 Ndipo Yuda Iskariote, mmoja wa wanafunzi kumi na wawili wa Yesu alikwenda kuzungumza na wakuu wa makuhani. 15 Akasema, “Nikimkabidhi Yesu kwenu, mtanilipa nini?” Makuhani walimpa sarafu thelathini za fedha. 16 Kuanzia siku hiyo, Yuda alianza kutafuta muda mzuri wa kumsaliti Yesu.
Karamu ya Pasaka
(Mk 14:12-21; Lk 22:7-14,21-23; Yh 13:21-30)
17 Ilipofika siku ya kwanza ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, wafuasi wake walimjia Yesu na kumwambia, “Tutaandaa kila kitu kwa ajili yako ili ule mlo wa Pasaka. Unataka tuandae wapi mlo wa Pasaka?”
18 Yesu akajibu, “Nendeni mjini kwa mtu ninayemfahamu. Mwambieni kuwa Mwalimu anasema, ‘Muda uliowekwa kwa ajili yangu umekaribia sana. Mimi na wafuasi wangu tutakula mlo wa Pasaka katika nyumba yako.’” 19 Walitii na kufanya kama Yesu alivyowaambia. Waliandaa mlo wa Pasaka.
20 Jioni ilipowadia, Yesu alikuwa ameketi mezani pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili. 21 Walipokuwa wakila Yesu akasema, “Niaminini, ninapowaambia kuwa mmoja wenu ninyi kumi na wawili atanikabidhi kwa maadui zangu.”
22 Wanafunzi walisikitika sana waliposikia hili. Kila mmoja akasema, “Bwana, hakika si mimi!”
23 Yesu akajibu, “Yeye aliyechovya mkate wake katika kikombe kile kile nilichochovya mimi ndiye atakayenisaliti. 24 Mwana wa Adamu atakiendea kifo chake kama Maandiko yanavyosema. Lakini ole wake mtu yule anayemsaliti Mwana wa Adamu ili auawe. Ni bora mtu huyo asingezaliwa.”
25 Ndipo Yuda, ambaye ndiye angemsaliti, akamwambia Yesu, “Mwalimu, hakika si mimi unayemzungumzia, ama ndiye?”
Yesu akamjibu, “hicho ndicho unachosema.”
Chakula cha Bwana
(Mk 14:22-26; Lk 22:15-20; 1 Kor 11:23-25)
26 Walipokuwa wakila, Yesu alichukua baadhi ya mikate na akamshukuru Mungu. Alimega baadhi ya vipande, akawapa wafuasi wake na akasema, “Chukueni mkate huu na mle. Ni mwili wangu.”
27 Kisha akachukua kikombe chenye divai, akamshukuru Mungu na akawapa. Akasema, “Kila mmoja wenu anywe divai iliyo katika kikombe hiki. 28 Divai hii ni damu yangu, itakayomwagika ili kusamehe dhambi za watu wengi na kuanza Agano Jipya ambalo Mungu analifanya na watu wake. 29 Ninataka mjue kuwa, hii ni mara ya mwisho nitakunywa divai mpaka siku ile nitakapokunywa divai mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu.”
30 Waliimba wimbo kwa pamoja kisha wakaenda kwenye Mlima wa Mizeituni.
Yesu Asema Wafuasi Wake Watamwacha
(Mk 14:27-31; Lk 22:31-34; Yh 13:36-38)
31 Yesu akawaambia wafuasi wake, “Usiku wa leo ninyi nyote mtapoteza imani yangu kwangu. Maandiko yanasema,
‘Nitamwua mchungaji,
na kondoo watatawanyika.’(A)
32 Lakini baada ya kuuawa, nitafufuka Kisha nitakwenda Galilaya. Nitakuwa huko kabla ninyi hamjaenda huko.”
33 Petro akajibu, “Wafuasi wengine wote wanaweza kupoteza imani juu yako. Lakini imani yangu haitatetereka.”
34 Yesu akajibu, “Ukweli ni huu, usiku wa leo utasema haunifahamu. Utanikana mara tatu kabla jogoo hajawika.”
35 Lakini Petro akajibu, “Sitasema kwamba sikufahamu! Mimi hata nitakufa pamoja nawe!” Na wafuasi wengine wote wakasema kitu hicho hicho.
Yesu Aomba Akiwa Peke Yake
(Mk 14:32-42; Lk 22:39-46)
36 Kisha Yesu akaondoka pamoja na wafuasi wake na kwenda mahali panapoitwa Gethsemane. Akawaambia, “Kaeni hapa wakati ninakwenda mahali pale kuomba.” 37 Alimwambia Petro na wana wawili wa Zebedayo waende pamoja naye. Kisha akaanza kuhuzunika na kuhangaika. 38 Yesu akamwambia Petro na wana wa Zebedayo, “Moyo wangu ni mzito na wenye huzuni hata kujisikia kana kwamba huzuni hiyo itaniua. Kaeni hapa mkeshe pamoja nami.”
39 Kisha Yesu akaenda mbele kidogo. Akainama hadi chini uso wake ukiigusa nchi akiomba na akasema, “Baba yangu, ikiwezekana, usifanye nikinywee kikombe hiki cha mateso.[c] Lakini fanya lile ulitakalo na si lile ninalolitaka mimi.” 40 Kisha akarudi walipokuwa wafuasi wake na akawakuta wamelala. Akamwambia Petro, “Je hamkuwa na uwezo wa kukesha pamoja nami hata kwa saa moja? 41 Amkeni kesheni na kuomba ili muyashinde majaribu. Roho zenu zinataka kufanya mambo sahihi, lakini miili yenu ni dhaifu.”
42 Kisha Yesu akaenda mara ya pili na akaomba akisema, “Baba yangu, ikiwa ni lazima nikinywee kikombe hiki na haiwezekani nikakwepa, basi mapenzi yako na yatimizwe.”
43 Kisha akarudi na kwenda walipokuwa wafuasi wake, akawakuta wamelala tena. Hawakuweza kukesha. 44 Hivyo akawaacha akaenda tena kuomba. Mara hii ya tatu alipokuwa anaomba akasema kama alivyosema hapo mwanzo.
45 Kisha Yesu akawarudia wafuasi wake na akasema, “Bado mnalala na kupumzika? Wakati wa Mwana wa Adamu kukabidhiwa kwa wenye dhambi umewadia. 46 Simameni! Tuondoke. Tazama yeye atakayenikabidhi anakuja.”
Yesu Akamatwa
(Mk 14:43-50; Lk 22:47-53; Yh 18:3-12)
47 Yesu alipokuwa anazungumza, Yuda mmoja wa wanafunzi wake kumi na mbili alifika akiwa na kundi kubwa la watu, waliokuwa wamebeba majambia na marungu. Walikuwa wametumwa na viongozi wa makuhani na wazee wa watu. 48 Yuda aliyekuwa amkabidhi Yesu kwao, alipanga kufanya kitu cha kuwajulisha yupi kati ya wafuasi alikuwa Yesu. Alisema, “Mtu nitakayembusu ndiye mtakayemkamata.” 49 Hivyo Yuda alikwenda kwa Yesu na kumwambia, “Salamu, Mwalimu!” Kisha akambusu.
50 Yesu akajibu, “Rafiki yangu, fanya ulilokuja kufanya.”
Kisha wale watu wakaja na kumkamata Yesu. 51 Jambo hili lilipotokea, mmoja wa wafuasi wa Yesu alichukua jambia lake na kumkata sikio mtumishi wa kuhani mkuu.
52 Yesu akamwambia, “Rudisha jambia lako mahali pake. Atumiaye jambia atauawa kwa jambia. 53 Hakika unajua kuwa ningemwomba Baba yangu yeye angenipa zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika. 54 Lakini hilo lisingekubaliana na yale Maandiko, yanayosema hivi ndivyo ilivyopasa itokee.”
55 Kisha Yesu akaliambia kundi, “Kwa nini mnakuja kunikamata mkiwa na mikuki na marungu kama vile mimi ni mhalifu? Nimekuwa nakaa eneo la Hekalu nikifundisha kila siku. Kwa nini hamkunikamata kule? 56 Lakini mambo haya yote yametokea ili kutimiza Maandiko yaliyoandikwa na manabii.” Ndipo wafuasi wake wote wakamwacha na kukimbia.
Yesu Akiwa Mbele ya Viongozi wa Kidini
(Mk 14:53-65; Lk 22:54-55,63-71; Yh 18:13-14,19-24)
57 Wale waliomkamata Yesu wakampeleka nyumbani kwa Kayafa, kuhani mkuu. Walimu wa Sheria na viongozi wazee wa Kiyahudi walikuwa wamekusanyika huko. 58 Petro alimfuata Yesu lakini alikuwa mbali kidogo. Alimfuata mpaka katika ua wa nyumba ya kuhani mkuu. Petro alienda uani na akakaa pamoja na walinzi. Alitaka kuona nini kingetokea.
59 Viongozi wa makuhani na baraza kuu walijaribu kutafuta kosa ili waweze kumwua Yesu. Walijaribu kutafuta watu ili wadanganye kuwa Yesu alifanya kosa. 60 Watu wengi walikuja na akasema uongo kuhusu Yesu. Lakini baraza lilishindwa kupata ushahidi wa kuutumia ili kumwua. Ndipo watu wawili walikuja 61 na akasema, “Mtu huyu[d] alisema, ‘Ninaweza kuliharibu Hekalu la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu.’”
62 Kisha kuhani mkuu alisimama na kumwambia Yesu, “Huna neno lolote la kujitetea dhidi ya mashtaka haya juu yako? Wanasema kweli?” 63 Lakini Yesu hakusema neno lolote.
Kisha kuhani mkuu akamwambia Yesu, “Apa mbele za Mungu aliye hai kwamba utatuambia kweli. Je, wewe ni Masihi, Mwana wa Mungu?”
64 Yesu akajibu, “Unaweza akasema hivyo, Mimi ndiye. Lakini ninawaambia, kitambo kidogo mtamwona Mwana wa Adamu akiwa amekaa upande wa kuume wa Mungu, mwenye Nguvu. Na mtamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni.”
65 Kuhani mkuu aliposikia hili, alilarua vazi lake kwa hasira. Akasema, “Mtu huyu amemtukana Mungu! Hatuhitaji mashahidi zaidi. Ninyi nyote mmesikia matusi yake. 66 Mnasemaje?”
Viongozi wa Kiyahudi wakajibu, “Ana hatia, na ni lazima afe.”
67 Na baadhi ya waliokuwa pale wakamtemea mate Yesu usoni na kumpiga makonde na wengine walimpiga makofi. 68 Wakasema, “Tuonyeshe kuwa wewe ni nabii, Masihi! Nani amekupiga!”
Petro Amkana Yesu
(Mk 14:66-72; Lk 22:56-62; Yh 18:15-18,25-27)
69 Petro alipokuwa amekaa nje uani, msichana mtumishi akamwendea. Akasema, “Ulikuwa pamoja na Yesu, yule mtu kutoka Galilaya.”
70 Lakini Petro akamwambia kila mtu aliyekuwa pale kuwa si kweli. Akasema “Sijui unachosema.”
71 Kisha akaondoka uani. Akiwa kwenye lango msichana mtumishi akamwona na akawaambia watu waliokuwa pale, “Mtu huyu alikuwa pamoja na Yesu wa Nazareti.”
72 Kwa mara nyingine tena Petro akasema hakuwa pamoja na Yesu. Akasema, “Ninaapa kwa Mungu, simfahamu mtu huyu!”
73 Baada ya muda mfupi baadaye, watu waliokuwa wamesimama pale wakamwendea Petro na kumwambia, “Tunajua wewe ni mmoja wao. Hata namna unavyoongea inaonesha wazi kuwa ndivyo hivyo.”
74 Kisha Petro akaanza kujiapiza mwenyewe ikiwa anaongopa. Akasema, “Ninaapa kwa Mungu, simfahamu mtu huyu!” Mara alipomaliza akasema hili, jogoo akawika. 75 Kisha akakumbuka maneno alivyoambiwa na Yesu kuwa: “Kabla jogoo hajawika, utakuwa umenikana mara tatu.” Kisha Petro akatoka nje na kulia kwa uchungu sana.
© 2017 Bible League International