Read the Gospels in 40 Days
Yesu ni Kama Mzabibu
15 Yesu akasema, “Mimi ndiye mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. 2 Yeye hulikata kutoka kwangu kila tawi lisilozaa matunda.[a] Pia hupunguza majani katika kila tawi linalozaa matunda ili kuliandaa liweze kuzaa matunda zaidi. 3 Ninyi mmewekwa tayari[b] kwa ajili ya kuzaa matunda[c] kutokana na mafundisho yale niliyowapa. 4 Hivyo mkae mkiwa mmeunganishwa kwangu, nami nitakaa nikiwa nimeunganishwa kwenu. Hakuna tawi linaloweza kuzaa matunda likiwa liko peke yake. Ni lazima liwe limeunganishwa katika mzabibu. Ndivyo ilivyo hata kwenu. Hamwezi kutoa matunda mkiwa peke yenu. Ni lazima muwe mmeunganishwa kwangu.
5 Mimi ni mzabibu, nanyi ni matawi. Mtatoa matunda mengi sana mkiwa mmeunganishwa kwangu, nami nimeunganishwa kwenu. Lakini mkitenganishwa mbali nami hamtaweza kufanya jambo lo lote. 6 Kama hamtaunganishwa nami, basi mtakuwa sawa na tawi lililotupwa pembeni nanyi mtakauka. Matawi yote yaliyokufa jinsi hiyo hukusanywa, hutupwa katika moto na kuchomwa. 7 Hivyo ninyi mbaki mmeunganishwa nami, na mfuate mafundisho yangu. Mkifanya hivyo, mnaweza kuomba kitu chochote mnachohitaji, nanyi mtapewa. 8 Ninyi mdhihirishe kuwa mmekuwa wafuasi wangu kwa kutoa matunda mengi. Kwani hiyo itamletea Baba utukufu.[d]
9 Mimi nimewapenda kama vile Baba alivyonipenda. Sasa mdumu katika upendo wangu. 10 Nimezitii amri za Baba yangu, naye anaendelea kunipenda. Kwa jinsi hiyo, nami nitaendelea kuwapenda mkizitii amri zangu. 11 Nimewaambia haya ili mpate furaha ya kweli kama ile niliyonayo mimi. Nami ninatamani muwe na furaha iliyo kamilifu. 12 Hii ndiyo amri yangu kwenu: Mpendane ninyi kwa ninyi kama mimi nilivyowapenda. 13 Hakuna anayeweza kuonesha pendo lolote kuu zaidi ya kuwa tayari kufa kwa ajili ya rafiki zake. Upendo wa hali ya juu unaoweza kuoneshwa na watu ni kufa badala ya rafiki zao. 14 Nanyi ni rafiki zangu mnapoyafanya yale ninayowaambia myafanye. 15 Siwaiti tena watumwa, kwa sababu watumwa hawajui yale yanayofanywa na bwana zao. Lakini sasa nawaita marafiki, kwa sababu nimewaambia yote aliyoniambia Baba yangu.
16 Ninyi hamkunichagua mimi. Bali ni mimi niliyewachagua ninyi. Nami niliwapa kazi hii: Kwenda na kutoa matunda; matunda ambayo yatadumu. Ndipo Baba atakapowapa chochote mtakachomwomba katika jina langu. 17 Hii ndiyo amri yangu: Mpendane ninyi kwa ninyi.
Yesu Awatahadharisha wafuasi Wake
18 Endapo ulimwengu utawachukia, mkumbuke kwamba umenichukia mimi kwanza. 19 Kama mngekuwa wa ulimwengu huu, ulimwengu ungewapenda kama watu wake. Lakini ulimwengu unawachukia kwa sababu ninyi siyo wa ulimwengu huu. Badala yake, mimi niliwachagua ninyi ili muwe tofauti na ulimwengu.
20 Kumbukeni somo nililowafundisha: Watumwa sio wakubwa kuliko mabwana wao. Kama watu walinitendea mimi vibaya, watawatendea vibaya hata nanyi pia. Na kama waliyatii mafundisho yangu, watayatii hata ya kwenu pia. 21 Watawatendea yale waliyonitendea mimi, kwa sababu ninyi ni wangu. Wao hawamjui yeye aliyenituma. 22 Kama nisingekuwa nimekuja na kusema na watu wa ulimwengu, basi wasingekuwa na hatia ya dhambi. Lakini sasa nimekwisha sema nao. Hivyo hawana cha kisingizio cha dhambi zao.
23 Yeyote anayenichukia mimi anamchukia na Baba pia. 24 Mimi nilifanya mambo miongoni mwa watu wa ulimwengu ambayo hayajawahi kufanywa na mtu yeyote mwingine. Kama nisingefanya mambo hayo, wao nao wasingekuwa na hatia ya dhambi. Ijapokuwa waliyaona niliyofanya, bado wananichukia mimi na Baba yangu. 25 Lakini haya yalitokea ili kuweka wazi yaliyoandikwa katika sheria zao: ‘Walinichukia bila sababu yoyote.’”[e]
26 Mimi, “Nitamtuma Msaidizi kutoka kwa Baba. Huyo Msaidizi ni Roho wa kweli anayekuja kutoka kwa Baba. Yeye atakapokuja, atasema juu yangu. 27 Nanyi pia mtawajulisha watu juu yangu, kwa sababu mmekuwa pamoja nami tangu mwanzo.
16 Nimewaambia mambo haya yote ili msipoteze imani mtakapokutana na matatizo. 2 Watu watawafukuza mtoke katika masinagogi[f] na msirudi humo tena. Hakika, unakuja wakati watapofikiri kuwa kwa kuwaua ninyi watakuwa wanatoa huduma kwa Mungu. 3 Watafanya hivyo kwa sababu hawajamjua Baba, na hawajanijua mimi pia. 4 Nimewaambia haya sasa ili kuwaandaa. Hivyo wakati wa mambo haya kutimia utakapofika, mtakumbuka kwamba niliwapa tahadhari mapema.
Kazi za Roho Mtakatifu
Sikuwaambia mambo haya tangu mwanzo, kwa sababu bado nilikuwa pamoja nanyi. 5 Sasa narudi kwake yeye aliyenituma, ingawa hakuna hata mmoja wenu anayeniuliza, ‘Unakwenda wapi?’ 6 Nanyi mmejawa na huzuni kwa vile nimewaambia mambo haya yote. 7 Hakika nawaambieni, ni kwa faida yenu mimi nikiondoka. Nasema hivi kwa sababu, nitakapoondoka nitamtuma kwenu Msaidizi. Lakini nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja.
8 Ila huyo Msaidizi atakapokuja, atawaonesha watu wa ulimwengu jinsi walivyofanya dhambi. Atawaonesha nani ana hatia ya dhambi, nani ana haki mbele za Mungu, na nani anastahili kuhukumiwa na Mungu. 9 Huyo Msaidizi atawaonesha kuwa wana hatia ya dhambi kwa sababu hawaniamini mimi. 10 Atawaonesha jinsi wasivyoelewa mtu anavyohesabiwa haki na Mungu. Hakika mimi nina kibali kwa sababu naenda kwa Baba nanyi hamtaniona tena. 11 Naye atawaonesha watu wa ulimwengu huu jinsi hukumu yao isivyo sahihi, kwa sababu mkuu wao ulimwenguni[g] amekwisha hukumiwa.
12 Ninayo mambo mengi ya kuwaeleza, lakini ni magumu kwenu kuyapokea kwa sasa. 13 Hata hivyo atakapokuja huyo Roho wa kweli, Yeye atawaongoza hadi kwenye kweli yote. Hatasema maneno yake mwenyewe bali atayasema yale tu anayosikia na atawajulisha yale yatakayotokea baadaye. 14 Roho wa kweli atanipa mimi utukufu kwa kuwaeleza ninyi yote aliyopokea kutoka kwangu. 15 Yote aliyonayo Baba ni yangu pia. Ndiyo sababu nilisema kwamba Roho atawaeleza yote anayopokea kutoka kwangu.
Huzuni Itageuzwa Kuwa Furaha
16 Baada ya kipindi kifupi hamtaniona. Kisha baada ya kipindi kingine kifupi mtaniona tena.”
17 Baadhi ya wafuasi wake wakaambiana wao kwa wao, “Ana maana gani anaposema, ‘Baada ya kipindi kifupi hamtaniona tena. Kisha baada ya kipindi kifupi kingine mtaniona tena?’ Tena ana maana gani anaposema, ‘Kwa sababu naenda kwa Baba’?” 18 Wakauliza pia, “Ana maana gani anaposema ‘Kipindi kifupi’? Sisi hatuelewi anayosema.” 19 Yesu alitambua kuwa wafuasi wake walitaka kumwuliza juu ya jambo hilo. Hivyo akawaambia, “Je, mnaulizana ninyi kwa ninyi kwamba nilikuwa na maana gani niliposema, ‘Baada ya kipindi kifupi hamtaniona. Kisha baada ya kipindi kifupi kingine mtaniona tena’? 20 Hakika nawaambia, ninyi mtapata huzuni na kulia, bali ulimwengu utakuwa na furaha. Ndio, mtapata huzuni, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha.
21 Mwanamke anapojifungua mtoto, hupata maumivu, kwa sababu wakati wake umefika. Lakini baada ya mtoto kuzaliwa, huyasahau maumivu yale. Husahau kwa sababu huwa na furaha kwa kuwa mtoto amezaliwa ulimwenguni. 22 Ndivyo ilivyo hata kwenu pia. Sasa mna huzuni lakini nitawaona tena, nanyi mtafurahi. Mtakuwa na furaha ambayo hakuna mtu atakayewaondolea. 23 Katika siku hiyo, hamtapaswa kuniuliza mimi kitu chochote. Nami kwa hakika nawaambia, Baba yangu atawapa lo lote mtakalomwomba kwa jina langu. 24 Hamjawahi kuomba lo lote kwa namna hii hapo awali. Bali ombeni kwa jina langu nanyi mtapewa. Kisha mtakuwa na furaha iliyotimia ndani yenu.
Ushindi Dhidi ya Ulimwengu
25 Nimewaambia mambo haya kwa kutumia maneno yenye mafumbo. Isipokuwa utakuja wakati ambapo sitatumia tena maneno ya jinsi hiyo kuwaeleza mambo. Nami nitasema nanyi kwa maneno ya wazi wazi juu ya Baba. 26 Kisha, mtaweza kumwomba Baba vitu kwa jina langu. Sisemi kwamba nitapaswa kumwomba Baba kwa ajili yenu. 27 Baba mwenyewe anawapenda kwa sababu ninyi mmenipenda mimi. Naye anawapenda kwa sababu mmeamini kwamba nimetoka kwa Mungu. 28 Mimi nimetoka kwa Baba kuja ulimwenguni. Sasa naondoka ulimwenguni na kurudi kwa Baba.”
29 Kisha wafuasi wake wakasema, “Tayari unaongea nasi wazi wazi. Hutumii tena maneno yanayoficha maana. 30 Sasa tunatambua kuwa unajua mambo yote. Wewe unajibu maswali yetu hata kabla hatujayauliza. Hii inatufanya tuamini kwamba ulitoka kwa Mungu.”
31 Yesu akasema, “Kwa hiyo sasa mnaamini? 32 Basi nisikilizeni! Wakati unakuja mtakapotawanywa, kila mmoja nyumbani kwake. Kwa hakika, wakati huo tayari umekwisha fika. Ninyi mtaniacha, nami nitabaki peke yangu. Lakini kamwe mimi siko peke yangu, kwa sababu Baba yupo pamoja nami.
33 Nimewaambia mambo haya ili muwe na amani ndani yangu. Katika ulimwengu huu mtapata mateso. Lakini muwe jasiri! Mimi nimeushinda ulimwengu!”
© 2017 Bible League International