Book of Common Prayer
Kusikiliza na Kutii
19 Kumbukeni hili ndugu zangu wapendwa: Kila mtu awe mwepesi wa kusikia lakini awe mzito wa kusema, na mzito kukasirika, 20 kwa sababu hasira ya mwanadamu haitoi haki inayohitajiwa na Mungu toka kwetu. 21 Hivyo acheni matendo yote machafu na kila uovu uliokaa karibu yenu, na mpokee kwa unyenyekevu mafundisho yaliyopandwa ndani ya mioyo yenu. Neno hilo, lina uwezo wa kuleta wokovu wa roho zenu.
22 Usisikilize tu kile ambacho mafundisho ya Mungu yanakisema; bali fanya yale inayosema! Ikiwa utasikiliza tu, utajidanganya mwenyewe. 23 Kwani kama mtu atasikiliza mafundisho ya Mungu, lakini asitende yanayosemwa, yuko kama mtu anayeutazama uso wake kwenye kioo. 24 Anajiangalia mwenyewe kwa haraka na anapoondoka tu husahau anavyoonekana. 25 Lakini anayetazama kwa makini katika sheria kamilifu ya Mungu, inayowaletea watu uhuru, na akaendelea kufanya hivyo asiwe msikilizaji anayesahau, bali huyatunza mafundisho katika matendo, mtu huyo atakuwa na baraka katika kila analofanya.
Njia Sahihi ya Kumwabudu Mungu
26 Kama kuna anayedhani kuwa ni mshika dini, lakini bado hauzuii ulimi wake anajidanganya mwenyewe. Dini yake mtu huyu haina manufaa. 27 Dini safi na isiyo na lawama mbele za Mungu Baba, inahusisha haya: kuwatunza yatima na wajane katika mazingira mgumu na kujilinda asichafuliwe na ulimwengu.
Yesu Afundisha Kuhusu Kutoa
6 Mnapofanya jambo jema, kuweni waangalifu msilifanye mbele za watu wengine ili wawaone. Mtakapofanya hivyo hamtapata thawabu kutoka kwa Baba yenu wa mbinguni.
2 Unapowapa maskini na wahitaji, usilipigie mbiu sana jambo hilo. Maana hivyo ndivyo wanavyofanya wanafiki kwenye makusanyiko.[a] Wao hupiga mbiu kabla ya kutoa ili watu wawaone, kwa kuwa hutaka kila mtu awasifu. Ukweli ni kuwa, hiyo ndiyo thawabu yote waliyokwishapata. 3 Hivyo unapowapa maskini, mtu yeyote asijue unachofanya.[b] 4 Kutoa kwako kunapaswa kufanyika sirini kwa kuwa Baba yako huona mambo yanayofanywa sirini, naye atakupa thawabu.
Yesu Afundisha Kuhusu Maombi
(Lk 11:2-4)
5 Mnapoomba, msiwe kama wanafiki. Wanapenda kusimama kwenye masinagogi na kwenye pembe za mitaa na kuomba kwa kupaza sauti. Wanapenda kuonwa na watu. Ukweli ni kuwa hiyo ndiyo thawabu yote watakayopata. 6 Lakini unapoomba, unapaswa kuingia katika chumba chako cha ndani na ufunge mlango. Kisha mwombe Baba yako aliye mahali pa siri. Yeye anayaona mambo yanayofanyika katika siri na hivyo atakupa thawabu.
Yesu Afundisha Kuhusu Kufunga
16 Mnapofunga, msijionyeshe kuwa na huzuni kama wanafiki wanavyofanya. Hukunja nyuso zao kwa kuonesha kuwa wana huzuni ili watu wawaone kuwa wamefunga. Ukweli ni kuwa wamekwishapata thawabu yao yote. 17 Hivyo unapofunga, nawa uso wako na ujiweke katika mwonekano mzuri, 18 ili watu wasijue kuwa umefunga, isipokuwa Baba yako, aliye nawe hata sirini. Anaweza kuona yanayofanywa sirini, naye atakupa thawabu.
© 2017 Bible League International