Book of Common Prayer
Ibada Chini ya Patano la Kale
9 Patano la kwanza lilikuwa na kanuni kwa ajili ya kuabudu na mahali pa kuabudia hapa duniani. 2 Mahali hapa palikuwa ni ndani ya hema. Eneo la kwanza ndani ya hema liliitwa Patakatifu. Katika Patakatifu kulikuwepo taa na meza iliyokuwa na mikate maalumu iliyotolewa kwa Mungu. 3 Nyuma ya pazia la pili kilikuwepo chumba kilichoitwa Patakatifu pa Patakatifu. 4 Katika Patakatifu pa Patakatifu kulikuwepo madhabahu ya dhahabu kwa ajili ya kuchoma uvumba. Pia lilikuwepo Sanduku la Agano. Sanduku lilifunikwa kwa dhahabu. Ndani ya hilo Sanduku kulikuwemo birika la mana na fimbo ya Haruni; fimbo ambayo iliwahi kuchipusha matawi. Vilevile ndani ya Sanduku yalikuwemo mawe bapa yaliyoandikwa Amri Kumi za agano la kale kwao. 5 Juu ya Sanduku walikuwepo viumbe wenye mbawa walioonesha utukufu wa Mungu. Viumbe hawa wenye mbawa walikuwa juu ya sehemu ya rehema.[a] Lakini hatuwezi kusema chochote kuhusu hili hivi sasa.
6 Kila kitu ndani ya hema kilikuwa kimewekwa tayari kwa namna nilivyoeleza. Kisha makuhani waliingia ndani ya chumba cha kwanza kila siku kutekeleza shughuli zao za ibada. 7 Lakini ni kuhani mkuu tu aliweza kuingia kwenye chumba cha pili, na aliingia mara moja tu kwa mwaka. Pia, asingeweza kuingia ndani ya chumba hicho bila kuchukua damu pamoja naye. Aliitoa damu hiyo kwa Mungu kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya dhambi walizotenda watu bila kujua kwamba walikuwa wanatenda dhambi.
8 Roho Mtakatifu hutumia vyumba hivi viwili tofauti kutufundisha kwamba njia ya kuelekea Patakatifu pa Patakatifu haikuwa wazi wakati chumba cha kwanza kilipokuwepo. 9 Huu ni mfano kwetu leo. Inaonyesha sadaka na sadaka ambazo makuhani walizitoa kwa Mungu haziwezi kufanya dhamiri za wanaoabudu ziwe safi kabisa. 10 Sadaka na sadaka hizi ni kwa ajili tu ya vyakula na vinywaji na aina maalumu ya kuoga. Ni sheria kuhusu mwili tu. Mungu alizitoa kwa watu wake wazifuate hadi wakati wa njia yake mpya.
Ibada Chini ya Patano Jipya
11 Lakini Kristo tayari amekuja awe kuhani mkuu. Yeye ni kuhani mkuu wa mambo mema tuliyonayo sasa. Lakini Kristo hatumiki ndani ya eneo kama hema ambalo makuhani wale walitumika ndani yake. Anatumika katika eneo bora zaidi. Tofauti na hema lile, hili ni kamilifu. Halikutengenezwa hapa duniani. Siyo la ulimwengu huu. 12 Kristo aliingia Patakatifu Zaidi mara moja tu; hii ilitosha kwa nyakati zote. Aliingia Patakatifu Zaidi kwa kutumia damu yake mwenyewe, siyo damu ya mbuzi au ya ng'ombe wadogo. Aliingia hapo na kutuweka huru milele kutoka katika dhambi.
13 Damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ng'ombe zilinyunyizwa juu ya wale ambao hawakuwa safi vya kutosha tena kuweza kuingia katika eneo la kuabudia. Damu na majivu viliwafanya wawe safi tena, lakini katika miili yao tu. 14 Hivyo hakika sadaka ya damu ya Kristo inaweza kufanya mambo bora zaidi. Kristo alijitoa mwenyewe kupitia Roho wa milele kama sadaka kamilifu kwa Mungu. Damu yake itatutakasa kabisa sisi kutoka katika maovu tuliyotenda. Itatupa sisi dhamiri safi ili tuweze kumwabudu Mungu aliye hai.
Yesu Amponya Mtu Bwawani
5 Baadaye, Yesu akaenda Yerusalemu kwa ajili ya sikukuu maalumu ya Wayahudi. 2 Huko Yerusalemu kulikuwa na bwawa lenye mabaraza matano. Kwa Kiaramu liliitwa Bethzatha.[a] Bwawa hili lilikuwa karibu na Lango la Kondoo. 3 Wagonjwa wengi walikuwa wamelala katika mabaraza pembeni mwa bwawa. Baadhi yao walikuwa wasiyeona, wengine walemavu wa viungo, na wengine waliopooza mwili.[b] 4 Nyakati zingine malaika wa Bwana alishuka bwawani na kuyatibua maji. Baada ya hapo, mtu wa kwanza aliyeingia bwawani aliponywa ugonjwa aliokuwa nao.[c] 5 Mmoja wa watu waliolala hapo alikuwa mgonjwa kwa muda wa miaka thelathini na minane. 6 Yesu alimwona akiwa amelala hapo na kutambua kuwa amekuwa mgonjwa kwa muda mrefu sana. Hivyo akamwuliza, “Je, unataka kuwa mzima?”
7 Yule mgonjwa akajibu, “Bwana, hakuna mtu wa kunisaidia kuingia kwenye bwawa mara maji yanapotibuliwa. Najitahidi kuwa wa kwanza kuingia majini. Lakini ninapojaribu, mtu mwingine huniwahi na kuingia majini kabla yangu.”
8 Kisha Yesu akasema, “Simama juu! Beba kirago chako na utembee.” 9 Mara hiyo, mtu huyo akapona. Akabeba kirago chake na kuanza kutembea.
Siku yalipotokea haya yote ilikuwa ni Siku ya Sabato.[d] 10 Hivyo baadhi ya Wayahudi wakamwambia yule mtu aliyeponywa, “Leo ni Sabato. Kulingana na sheria yetu wewe hauruhusiwi kubeba mkeka katika siku ya Sabato!”
11 Lakini yeye akajibu, “Yule mtu aliyeniponya aliniambia, ‘Beba mkeka wako uende.’”
12 Wakamwuliza, “Ni nani aliyekuambia kubeba mkeka wako na kutembea?”
13 Lakini yule mtu aliyeponywa hakuwa amemfahamu ni nani. Walikuwepo watu wengi hapo, na Yesu alikwisha kuondoka.
14 Baadaye, Yesu akamwona huyo mtu Hekaluni na akamwambia, “Tazama, umepona sasa. Kwa hivyo uache kutenda dhambi tena, la sivyo jambo baya zaidi laweza kukupata.” 15 Kisha huyo mtu akaondoka na kurudi kwa wale Wayahudi waliomuuliza. Naye aliwaeleza kuwa Yesu ndiye aliyemponya.
16 Yesu alikuwa anayafanya yote haya katika siku ya Sabato. Hivyo Wayahudi hao wakaanza kumsumbua asiendelee. 17 Lakini yeye akawaambia, “Baba yangu hajawahi kuacha kufanya kazi, hivyo nami pia nafanya kazi.” 18 Hili likawafanya waongeze juhudi ya kumwua. Wakasema, “Mwanzoni mtu huyu alikuwa anavunja sheria kuhusu siku ya Sabato. Kisha akasema kwamba Mungu ni Baba yake! Yeye anajifanya kuwa yuko sawa na Mungu.”
© 2017 Bible League International