Book of Common Prayer
13 Mungu aliweka ahadi kwa Ibrahimu. Na hayuko yeyote aliye mkuu kuliko Mungu, hivyo akaweka ahadi yenye kiapo kwa jina lake mwenyewe; kiapo ambacho atatimiza alichoahidi. 14 Alisema, “Hakika nitakubariki. Nitakupa wewe wazaliwa wengi.”(A) 15 Ibrahimu akangoja kwa uvumilivu hili litimie, na baadaye akapokea kile Mungu alichoahidi.
16 Mara nyingi watu hutumia jina la mtu aliye mkuu zaidi yao ili kuweka ahadi yenye kiapo. Kiapo huthibitisha kwamba walichokisema ni kweli, na hakuna haja ya kubishana juu ya hilo. 17 Mungu alitaka kuthibitisha kuwa ahadi yake ilikuwa kweli. Alitaka kuthibitisha hili kwa wale ambao wataipokea ahadi. Aliwataka waelewe kwa uwazi kwamba makusudi yake kamwe hayabadiliki. Hivyo Mungu akisema kitu fulani kingetokea, na akathibitisha aliyosema kwa kuongezea kiapo. 18 Mambo haya mawili hayawezi kubadilika: Mungu hawezi kusema uongo anaposema kitu, na hawezi kudanganya anapoweka kiapo.
Hivyo mambo yote hayo ni ya msaada mkubwa kutusaidia sisi tuliomjia Mungu kwa ajili ya usalama. Yanatuhimiza kuling'ang'ania tumaini lililo letu. 19 Tumaini hili tulilonalo ni kama nanga kwetu. Ni imara na la uhakika na hutulinda salama. Huenda hadi nyuma ya pazia[a] katika mahali patakatifu zaidi kwenye hekalu la kimbingu la Mungu. 20 Tayari Yesu amekwisha kuingia hapo na kuifungua njia kwa ajili yetu. Amefanyika kuhani mkuu milele, kama alivyokuwa Melkizedeki.
Yesu Azungumza na Mwanamke Msamaria
4 Yesu akatambua ya kwamba Mafarisayo wamesikia habari kuwa alikuwa anapata wafuasi wengi kuliko Yohana na kuwabatiza. 2 (Lakini kwa hakika, Yesu mwenyewe hakumbatiza mtu yeyote huko; bali wafuasi wake ndiyo waliowabatiza watu kwa niaba yake.) 3 Hivyo akaondoka Uyahudi na kurudi Galilaya.
4 Barabara ya kuelekea Galilaya ilimpitisha Yesu katikati ya nchi ya Samaria. 5 Akiwa Samaria Yesu akafika katika mji wa Sikari, ulio karibu na shamba ambalo Yakobo alimpa mwanawe Yusufu. 6 Mahali hapo ndipo kilikuwapo kisima cha Yakobo. Kutokana na safari yake kuwa ndefu Yesu alichoka, hivyo akakaa chini kando ya kisima. Nayo ilikuwa saa sita adhuhuri. 7 Baadaye mwanamke Msamaria akaja kisimani hapo kuchota maji, na Yesu akamwambia, “Tafadhali nipe maji ninywe.” 8 Hili lilitokea wakati wafuasi wake walipokuwa mjini kununua chakula.
9 Mwanamke yule akajibu, “Nimeshangazwa wewe kuniomba maji unywe! Wewe ni Myahudi nami ni mwanamke Msamaria!” (Wayahudi hawana uhusiano na Wasamaria.[a])
10 Yesu akajibu, “Hujui kile Mungu anachoweza kukukirimu. Na hunijui mimi ni nani, niliyekuomba maji ninywe. Kama ungejua, nawe ungekuwa umeniomba tayari, nami ningekupa maji yaletayo uzima.”
11 Mwanamke akasema, “Bwana, utayapata wapi maji yaliyo hai? Kisima hiki kina chake ni kirefu sana, nawe huna kitu cha kuchotea. 12 Je, wewe ni mkuu kumzidi baba yetu Yakobo? Yeye ndiye aliyetupa kisima hiki. Yeye alikunywa kutoka kisima hiki, na wanawe, na wanyama wake wote.”
13 Yesu akajibu, “Kila anayekunywa maji haya ataona kiu tena. 14 Bali yeyote anayekunywa maji ninayompa mimi hatapata kiu tena. Maji ninayowapa watu yatakuwa kama chemichemi inayobubujika ndani yao. Hayo yatawaletea uzima wa milele.”
15 Mwanamke akamwambia Yesu, “Bwana, nipe maji hayo. Kisha sitapata kiu na sitapaswa kuja tena hapa kuchota maji.”
© 2017 Bible League International