Book of Common Prayer
1 Salamu kutoka kwa Paulo, mtume wa Kristo Yesu.[a] Mimi ni mtume kwa sababu ndivyo Mungu alivyotaka niwe. Salamu pia kutoka kwa Timotheo ndugu yetu katika Kristo.
2 Salamu kwenu kaka na dada zetu watakatifu na walio waaminifu katika Kristo mlioko Kolosai.
Neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu ziwe pamoja nanyi.
3 Katika maombi yetu tunamshukuru Mungu daima kwa ajili yenu. Yeye ndiye Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. 4 Nasi tunamshukuru Yeye kwa sababu tumesikia kuhusu imani yenu katika Kristo Yesu na upendo wenu kwa watu wa Mungu wote. 5 Imani yenu na upendo wenu vinatokana na ufahamu kwamba mtapokea kile mnachotumaini. Hicho ambacho Mungu amekihifadhi salama mbinguni kwa ajili yenu. Hilo ni tumaini lile lile ambalo mmekuwa nalo tangu mliposikia kwa mara ya kwanza ujumbe wa kweli, yaani Habari Njema. 6 Habari Njema hii imezaa matunda na imeenea ulimwenguni kote. Na hicho ndicho kilichokuwa kikitokea tangu siku mliposikia kwa mara ya kwanza na kuelewa ukweli wa neema ya Mungu. 7 Kweli hiyo mliisikia kutoka kwa Epafra, aliye mtumwa wa Bwana pamoja nasi. Yeye anatusaidia sisi[b] kama mtumishi mwaminifu wa Kristo. 8 Naye ametueleza pia kuhusu upendo mlioupokea kutoka kwa Roho Mtakatifu.
9 Ndugu zangu tangu siku tuliposikia mambo haya juu yenu, tumeendelea kuwaombea, na haya ndiyo maombi yetu kwa ajili yenu:
Kwamba Mungu awajaze ufahamu wa mapenzi yake kwa kuwapa hekima na ufahamu wote wa kiroho mnaohitaji; 10 ili hayo yawasaidie kuishi maisha yanayomletea Bwana heshima na kumpendeza yeye katika hali zote; ili maisha yenu yazae matunda mema ya aina mbalimbali na mpate kuongezeka katika maarifa yenu ya Mungu;[c] 11 ili Mungu mwenyewe awaimarishe kwa uwezo wake mkuu, ili muwe na uvumilivu pasipo kukata tamaa mnapokutana na shida.
Ndipo nanyi mtakapofurahi, 12 na kumshukuru Mungu Baba. Kwani yeye amewastahilisha kupokea kile alichowaahidi watakatifu wake, wanaoishi katika nuru. 13 Mungu ametuweka huru kutoka katika nguvu za giza. Naye ametuingiza katika ufalme wa Mwanaye mpendwa. 14 Na huyo Mwana amelipa gharama ya kutuweka huru, kwani ndani yake tuna msamaha wa dhambi zetu.
30 Hivyo watu wakamwuliza, “Ni ishara gani utakayotufanyia? Ili nasi tutakapokuona unafanya ishara basi tukuamini? Je, utafanya nini? 31 Baba zetu walipewa mana kula jangwani. Kama Maandiko yanavyosema, ‘Aliwapa mkate wa kula kutoka mbinguni.’”(A)
32 Yesu akasema, “Naweza kuwahakikishia kwamba Musa siye aliyewapa watu wenu mkate kutoka mbinguni. Bali Baba yangu huwapa ninyi mkate halisi unaotoka mbinguni. 33 Mkate wa Mungu ni ule unaoshuka kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima.”
48 Maana mimi ni mkate unaoleta uzima. 49 Baba zenu walikula mana waliyopewa na Mungu kule jangwani, lakini haikuwazuia kufa. 50 Hapa upo mkate unaotoka mbinguni. Yeyote anayekula mkate huu hatakufa kamwe. 51 Mimi ni mkate ulio hai ulioshuka kutoka mbinguni. Yeyote atakayeula mkate huu ataishi milele. Mkate huu ni mwili wangu. Nitautoa mwili wangu ili watu wa ulimwengu huu waweze kupata uzima.”
© 2017 Bible League International