Book of Common Prayer
Uhai Wenu Mpya Miongoni Mwenu
12 Mungu amewachagua na kuwafanya ninyi kuwa watu wake walio watakatifu. Anawapenda. Hivyo, jivikeni matendo haya na muwe na huruma: wema, wanyenyekevu, wapole na wenye subira. 13 Msikasirikiane, bali msameheane. Mtu yeyote akikukosea, msamehe. Wasameheni wengine kwa sababu Bwana amewasamehe ninyi. 14 Pamoja na haya yote, vaeni upendo. Upendo ndicho kitu kinachounganisha kila kitu katika umoja mkamilifu. 15 Amani inayotoka kwa Kristo itawale fahamu zenu. Mliitwa kwa ajili ya amani ili muwe pamoja katika mwili[a] mmoja. Mwe na shukrani daima.
16 Na mafundisho ya Kristo[b] yakae kwa wingi ndani yenu. Mfundishane na mshauriane ninyi kwa ninyi kwa hekima yote, mkiimba zaburi, nyimbo za sifa na nyimbo zinaowezeshwa na roho na kumshukuru Mungu katika mioyo yenu. 17 Kila mnachosema na kutenda, mkifanye kwa ajili ya Yesu Kristo Bwana wenu huku mkimshukuru Mungu Baba kupitia Yesu Kristo.
41 Baadhi ya Wayahudi walianza kumlalamikia Yesu kwa vile alisema, “Mimi ni mkate unaoshuka kutoka mbinguni.” 42 Wakasema, “Huyu ni Yesu. Tunawajua baba na mama yake. Yeye ni mtoto wa Yusufu. Anawezaje kusema, ‘Nilishuka kutoka mbinguni’?”
43 Lakini Yesu akawaambia, “Acheni kunung'unika miongoni mwenu. 44 Baba ndiye aliyenituma, na ndiye anayewaleta watu kwangu. Nami nitawafufua siku ya mwisho. Hakuna mtu anayeweza kuja kwangu asipoletwa na Baba yangu. 45 Hii iliandikwa katika vitabu vya manabii: ‘Mungu atawafundisha wote.’(A) Watu humsikiliza Baba na hujifunza kutoka kwake. Hao ndiyo wanaokuja kwangu. 46 Sina maana kwamba yupo yeyote aliyemwona Baba. Yule pekee aliyekwisha kumwona Baba ni yule aliyetoka kwa Mungu. Huyo amemwona Baba.
47 Hakika nawaambieni kila anayeamini anao uzima wa milele.
© 2017 Bible League International