Book of Common Prayer
9 Mimi ni Yohana, mwamini mwenzenu. Tuko pamoja katika Yesu na tunashirikiana mambo haya: mateso, ufalme na uvumilivu wenye subira. Nilikuwa katika kisiwa cha Patmo[a] kwa sababu nimekuwa mwaminifu kwa ujumbe wa Mungu na kwa ajili ya kweli ya Yesu. 10 Siku ya Bwana, Roho Mtakatifu alinitawala. Nilisikia sauti kuu nyuma yangu iliyosikika kama tarumbeta. 11 Ilisema, “Yaandike kwenye kitabu yale unayoyaona na uyatume kwa makanisa saba ya Efeso, Smirna, Pergamo, Thiatira, Sardi, Filadelfia na Laodikia.”
12 Niligeuka nyuma nimwone aliyekuwa anazungumza nami. Nilipogeuka, niliona vinara saba vya taa vya dhahabu. 13 Nikamwona mmoja katikati ya vinara aliyeonekana kama Mwana wa Mtu. Alikuwa amevaa vazi refu, na mshipi wa dhahabu uliofungwa kuzunguka kifua chake. 14 Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu nyeupe kama theluji. Macho yake yalikuwa kama miali ya moto. 15 Miguu yake ilikuwa kama shaba ing'aayo inapochomwa katika tanuru. Sauti yake ilikuwa kama kelele za mafuriko ya maji. 16 Alikuwa ameshikilia nyota saba katika mkono wake wa kulia. Upanga wenye makali kuwili ulitoka kinywani mwake. Uso wake ulikuwa jua linalong'aa sana mchana.
Amri ipi ni ya Muhimu Zaidi?
(Mk 12:28-34; Lk 10:25-28)
34 Mafarisayo waliposikia kuwa Yesu amewafanya Masadukayo waonekane wajinga nao wakaacha kumwuliza maswali. Kwa hiyo Mafarisayo wakafanya mkutano. 35 Ndipo mmoja wao, aliye mtaalamu wa Sheria ya Musa, akamwuliza Yesu swali ili kumjaribu. 36 Akasema, “Mwalimu, amri ipi katika sheria ni ya muhimu zaidi?”
37 Yesu akajibu, “‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote na akili yako yote.’(A) 38 Hii ndiyo amri ya kwanza na ya muhimu zaidi. 39 Na amri ya pili ni kama ya kwanza: ‘Mpende jirani yako[a] kama unavyojipenda wewe mwenyewe.’(B) 40 Sheria yote na maandiko ya manabii yamejengwa katika amri hizi mbili.”
Je, Masihi ni Mwana wa Daudi?
(Mk 12:35-37; Lk 20:41-44)
41 Hivyo Mafarisayo walipokuwa pamoja, Yesu aliwauliza swali. 42 Akasema, “Nini mawazo yenu juu ya Masihi? Je, ni mwana wa nani?” Mafarisayo wakajibu, “Masihi ni Mwana wa Daudi.”
43 Yesu akawaambia, “Sasa ni kwa nini Daudi anamwita ‘Bwana’? Daudi alikuwa anazungumza kwa nguvu ya Roho. Aliposema,
44 ‘Bwana Mungu alimwambia Bwana Mfalme wangu:
Keti karibu nami upande wangu wa kuume,
na nitawaweka adui zako chini ya udhibiti wako.’[b](C)
45 Ikiwa Daudi anamwita Masihi ‘Bwana’. Inakuwaje Masihi ni mwana wa Daudi?”
46 Hakuna Farisayo aliyeweza kumjibu Yesu. Na baada ya siku hiyo, hakuna aliyekuwa jasiri kumwuliza maswali zaidi.
© 2017 Bible League International