Book of Common Prayer
9 Ndugu zangu tangu siku tuliposikia mambo haya juu yenu, tumeendelea kuwaombea, na haya ndiyo maombi yetu kwa ajili yenu:
Kwamba Mungu awajaze ufahamu wa mapenzi yake kwa kuwapa hekima na ufahamu wote wa kiroho mnaohitaji; 10 ili hayo yawasaidie kuishi maisha yanayomletea Bwana heshima na kumpendeza yeye katika hali zote; ili maisha yenu yazae matunda mema ya aina mbalimbali na mpate kuongezeka katika maarifa yenu ya Mungu;[a] 11 ili Mungu mwenyewe awaimarishe kwa uwezo wake mkuu, ili muwe na uvumilivu pasipo kukata tamaa mnapokutana na shida.
Ndipo nanyi mtakapofurahi, 12 na kumshukuru Mungu Baba. Kwani yeye amewastahilisha kupokea kile alichowaahidi watakatifu wake, wanaoishi katika nuru. 13 Mungu ametuweka huru kutoka katika nguvu za giza. Naye ametuingiza katika ufalme wa Mwanaye mpendwa. 14 Na huyo Mwana amelipa gharama ya kutuweka huru, kwani ndani yake tuna msamaha wa dhambi zetu.
Mwana wa Mungu yu sawa na Mungu
15 Hakuna anayeweza kumwona Mungu,
lakini Mwana anafanana kabisa na Mungu.
Anatawala juu ya kila kitu kilichoumbwa.
16 Kwa uweza wake, vitu vyote viliumbwa:
vitu vya angani na ardhini, vinavyoonekana na visivyoonekana,
watawala wote wa kiroho, wakuu, enzi, na mamlaka.
Kila kitu kiliumbwa kupitia Yeye na kwa ajili yake.
17 Mwana alikuwapo kabla ya kuumbwa kitu chochote,
na vyote vinaendelea kuwepo kwa sababu yake.
18 Yeye ni kichwa cha mwili,
yaani kanisa.
Yeye ni mwanzo wa maisha yajayo,
ni wa kwanza miongoni mwa wote watakaofufuliwa kutoka kwa wafu.[b]
Hivyo katika mambo yote yeye ni mkuu zaidi.
19 Mungu alipendezwa kwamba ukamilifu wa uungu wake
uishi ndani ya Mwana.
20 Na kupitia Yeye, Mungu alifurahi
kuvipatanisha tena vitu vyote kwake Yeye mwenyewe;
vilivyoko mbinguni na vilivyoko duniani.
Mungu alileta amani kupitia sadaka ya damu ya Mwanaye msalabani.
Yesu Atambulishwa Hekaluni
22 Muda wa kutakaswa ulimalizika, kama ilivyotakiwa na Sheria ya Musa baada ya mtoto kuzaliwa.[a] Baada ya hapo walimpeleka Yesu Yerusalemu na kumweka mbele za Bwana. 23 Kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana: Mzaliwa wa kwanza akiwa mtoto wa kiume, atolewe wakfu kwa ajili ya Bwana.[b] 24 Pia Mariamu na Yusufu walikwenda Yerusalemu kutoa dhabihu kama Sheria ya Bwana inavyosema kuwa, “Ni lazima utoe dhabihu ya jozi moja ya hua[c] au makinda mawili wa njiwa.”
Simeoni Amwona Yesu
25 Alikuwepo mtu mmoja aliyeishi katika mji wa Yerusalemu, mtu huyu aliitwa Simeoni. Alikuwa mtu mwema na mcha Mungu na Roho Mtakatifu alikuwa pamoja naye. Alikuwa akiusubiri wakati ambao Mungu angeisaidia Israeli. 26 Roho Mtakatifu alimwambia kwamba asingekufa kabla ya kumwona Masihi kutoka kwa Bwana. 27 Roho Mtakatifu alimwongoza mpaka Hekaluni. Hivyo, alikuwemo Hekaluni wakati Mariamu na Yusufu walipomleta mtoto Yesu ili wamfanyie kama ilivyotakiwa katika Sheria ya Kiyahudi. 28 Simeoni alimbeba mtoto Yesu mikononi mwake, akamshukuru Mungu na kusema,
29 “Sasa, Bwana, niruhusu mimi mtumishi wako nife kwa amani
kwa kuwa umeitimiza ahadi yako kwangu.
30 Nimeona kwa macho yangu namna utakavyowaokoa watu wako.
31 Sasa watu wote wanaweza kuuona mpango wako.
32 Yeye ni mwanga wa kuionesha njia yako kwa mataifa mengine,
na atawaletea heshima watu wako Israeli.”
33 Mariamu na Yusufu walishangazwa sana na maneno aliyosema Simeoni kuhusu Yesu. 34 Kisha Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu; “Wayahudi wengi wataanguka na wengi watainuka kwa sababu ya mtoto huyu. Atakuwa ishara kutoka kwa Mungu, lakini baadhi ya watu watamkataa. 35 Mawazo ya siri ya watu wengi yatajulikana. Na mambo yatakayotokea yatakuumiza, kama upanga unaokuchoma moyoni.”
Ana Amwona Yesu
36 Alikuwapo nabii aliyeitwa Ana binti Fanueli, kutoka katika kabila la Asheri. Alikuwa mwanamke mzee sana. Aliishi na mume wake kwa miaka saba, 37 kabla ya mume wake kufa na kumwacha peke yake. Na sasa alikuwa na umri wa miaka themanini na nne. Ana alikuwa Hekaluni daima, hakutoka. Alimwabudu Mungu kwa kufunga na kuomba usiku na mchana.
38 Simeoni alipokuwa anazungumza na Yusufu na Mariamu, Ana alikwenda walipokuwa na akaanza kumsifu Mungu na kuwaambia kuhusu Yesu watu wote waliokuwa wanasubiri Mungu kuikomboa Yerusalemu.
Yusufu, Mariamu na Yesu Warudi Nyumbani
39 Yusufu na Mariamu walipotimiza mambo yote yanayotakiwa katika sheria ya Bwana, walirudi Galilaya, katika mji wao wa Nazareti. 40 Mtoto Yesu aliendelea kukua na kuwa kijana mwenye nguvu na aliyejaa hekima nyingi. Na Mungu alikuwa anambariki.
© 2017 Bible League International