Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Mashahidi Wawili
11 Kisha nilipewa fimbo ya kupimia, ndefu kama fimbo ya kutembelea. Nikaambiwa, “Nenda ukalipime hekalu[a] la Mungu na madhabahu na uwahesabu watu wanaoabudu humo. 2 Lakini usipime eneo lililo nje ya hekalu. Liache. Eneo hilo wamepewa watu wasio wa Mungu. Wataonesha nguvu zao juu ya mji mtakatifu kwa miezi 42. 3 Nami nitawapa nguvu mashahidi wangu wawili, watatabiri kwa siku 1,260. Nao watakuwa wamevaa magunia.”
4 Mashahidi hawa wawili ni mizeituni miwili na vinara viwili vya taa vinavyosimama mbele za Bwana wa dunia. 5 Ikiwa mtu yeyote atajaribu kuwadhuru mashahidi hawa, moto utatoka katika vinywa vyao na kuwaua adui zao. Yeyote atakaye jaribu kuwadhuru atakufa. 6 Mashahidi hawa wana nguvu ya kuzuia mvua isinyeshe katika wakati ambao watakuwa wanatabiri. Pia wana uwezo wa kugeuza maji kuwa damu. Wana uwezo wa kutuma kila aina ya pigo duniani. Wanaweza kufanya hivi kadri wanavyotaka.
7 Mashahidi wawili watakapomaliza kuutangaza ujumbe wao, mnyama atokaye kuzimu atapigana nao. Atawashinda na kuwaua. 8 Miili ya mashahidi hawa wawili italala kwenye mtaa wa mji mkuu. Mji huu unaitwa Sodoma na Misri. Majina ya mji huu yana maana maalumu. Huu ni mji ambako Bwana aliuawa. 9 Watu kutoka kila asili, kabila, lugha na taifa wataiangalia miili ya mashahidi hawa wawili kwa siku tatu na nusu. Watu watakataa kuwazika. 10 Na Kila aishiye duniani atafurahi kwa sababu mashahidi hawa wawili wamekufa. Watu watafanya sherehe na kupeana zawadi kwa sababu manabii hawa wawili walileta mateso mengi kwa watu waishio duniani.
11 Lakini baada ya siku tatu na nusu, Mungu akawarudishia uhai mashahidi hawa wawili. Wakasimama kwa miguu yao. Na wale waliowaona wakajaa hofu. 12 Kisha mashahidi wakasikia sauti kuu kutoka mbinguni ikisema, “Njooni huku juu!” Na wote wawili wakaenda juu mbinguni katika wingu, adui zao wakiangalia wanavyokwenda.
13 Katika wakati huo huo kulitokea tetemeko kuu la ardhi. Sehemu ya kumi ya mji ikateketea, na watu elfu saba wakafa. Wale ambao hawakufa waliogopa sana. Wakampa utukufu Mungu wa mbinguni.
14 Kitisho cha pili kimepita. Kitisho cha tatu kinakuja haraka.
© 2017 Bible League International