Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
9 Mimi ni Yohana, mwamini mwenzenu. Tuko pamoja katika Yesu na tunashirikiana mambo haya: mateso, ufalme na uvumilivu wenye subira. Nilikuwa katika kisiwa cha Patmo[a] kwa sababu nimekuwa mwaminifu kwa ujumbe wa Mungu na kwa ajili ya kweli ya Yesu. 10 Siku ya Bwana, Roho Mtakatifu alinitawala. Nilisikia sauti kuu nyuma yangu iliyosikika kama tarumbeta. 11 Ilisema, “Yaandike kwenye kitabu yale unayoyaona na uyatume kwa makanisa saba ya Efeso, Smirna, Pergamo, Thiatira, Sardi, Filadelfia na Laodikia.”
12 Niligeuka nyuma nimwone aliyekuwa anazungumza nami. Nilipogeuka, niliona vinara saba vya taa vya dhahabu. 13 Nikamwona mmoja katikati ya vinara aliyeonekana kama Mwana wa Mtu. Alikuwa amevaa vazi refu, na mshipi wa dhahabu uliofungwa kuzunguka kifua chake. 14 Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu nyeupe kama theluji. Macho yake yalikuwa kama miali ya moto. 15 Miguu yake ilikuwa kama shaba ing'aayo inapochomwa katika tanuru. Sauti yake ilikuwa kama kelele za mafuriko ya maji. 16 Alikuwa ameshikilia nyota saba katika mkono wake wa kulia. Upanga wenye makali kuwili ulitoka kinywani mwake. Uso wake ulikuwa jua linalong'aa sana mchana.
17 Nilipomwona nilianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Aliweka mkono wake wa kulia juu yangu na kusema, “Usiogope! Mimi ni wa kwanza na wa Mwisho. 18 Mimi ndiye ninayeishi. Nilikufa, lakini tazama, niko hai milele na milele! Na ninashikilia funguo za mauti na Kuzimu.
© 2017 Bible League International