Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Roho Mtakatifu Awashukia Watu Wasio Wayahudi
44 Petro alipokuwa bado anazungumza, Roho Mtakatifu aliwashukia wote waliokuwa wanamsikiliza. 45 Waamini wa Kiyahudi waliofuatana na Petro walishangaa kwamba Roho Mtakatifu amemiminwa kama zawadi hata kwa watu wasio Wayahudi. 46 Waliwasikia wakiongea lugha mbalimbali na kumsifu Mungu. Ndipo Petro akasema, 47 “Je, mtu yeyote anawezaje kuzuia watu hawa wasibatizwe katika maji? Wamempokea Roho Mtakatifu kama sisi tulivyompokea!” 48 Hivyo Petro akawaambia wambatize Kornelio pamoja na jamaa zake na rafiki zake katika jina la Yesu Kristo. Kisha wakamwomba Petro akae nao kwa siku chache.
Watoto wa Mungu Ushindeni Ulimwengu
5 Watu wanao amini kuwa Yesu ni Masihi ni wana wa Mungu. Na kila ampendae Baba pia anawapenda watoto wa Baba. 2 Twatambuaje kuwa tunawapenda watoto wa Mungu? Twatambua kwa sababu tunampenda Mungu na tunazitii amri zake. 3 Kumpenda Mungu ni kuzitii amri zake. Na amri za Mungu si ngumu kwetu, 4 kwa sababu kila ambae ni mwana wa Mungu ana uwezo wa kushinda dhidi ya ulimwengu. Ni imani yetu iliyoshinda vita dhidi ya ulimwengu. 5 Hivyo ni nani anayeushinda ulimwengu? Ni wale tu wanaoamini kuwa Yesu ni mwana wa Mungu.
Mungu alituambia kwa Habari ya Mwanae
6 Yesu Kristo ndiye aliyekuja. Alikuja kwa maji na damu.[a] Hakuja kwa maji peke yake. Lahasha, Yesu alikuja kwa vyote maji na damu. Na Roho atuambia kuwa hili ni kweli. Roho ndiye Kweli.
9 Mimi nimewapenda kama vile Baba alivyonipenda. Sasa mdumu katika upendo wangu. 10 Nimezitii amri za Baba yangu, naye anaendelea kunipenda. Kwa jinsi hiyo, nami nitaendelea kuwapenda mkizitii amri zangu. 11 Nimewaambia haya ili mpate furaha ya kweli kama ile niliyonayo mimi. Nami ninatamani muwe na furaha iliyo kamilifu. 12 Hii ndiyo amri yangu kwenu: Mpendane ninyi kwa ninyi kama mimi nilivyowapenda. 13 Hakuna anayeweza kuonesha pendo lolote kuu zaidi ya kuwa tayari kufa kwa ajili ya rafiki zake. Upendo wa hali ya juu unaoweza kuoneshwa na watu ni kufa badala ya rafiki zao. 14 Nanyi ni rafiki zangu mnapoyafanya yale ninayowaambia myafanye. 15 Siwaiti tena watumwa, kwa sababu watumwa hawajui yale yanayofanywa na bwana zao. Lakini sasa nawaita marafiki, kwa sababu nimewaambia yote aliyoniambia Baba yangu.
16 Ninyi hamkunichagua mimi. Bali ni mimi niliyewachagua ninyi. Nami niliwapa kazi hii: Kwenda na kutoa matunda; matunda ambayo yatadumu. Ndipo Baba atakapowapa chochote mtakachomwomba katika jina langu. 17 Hii ndiyo amri yangu: Mpendane ninyi kwa ninyi.
© 2017 Bible League International