Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Yesu Azungumza Tena Kuhusu Kifo Chake
(Mt 20:17-19; Lk 18:31-34)
32 Walikuwa wote njiani wakipanda kuelekea Yerusalemu, na Yesu alikuwa akitembea mbele yao. Nao walisumbuka sana. Na wale waliowafuata walikuwa na hofu pia. Kwa mara nyingine Yesu akawachukua wale wanafunzi kumi na mbili pembeni, na akaanza kuwaeleza yale yatakayomtokea Yerusalemu. 33 “Sikilizeni! Tunaelekea hadi Yerusalemu na Mwana wa Adamu atasalitiwa na kutolewa kwa viongozi wa makuhani na walimu wa Sheria, nao watamtia hatiani na kumpa hukumu kifo, kisha watamtoa kwa wale wasio Wayahudi, 34 Nao watamdhihaki, na watamtemea mate, na watamchapa kwa viboko vya ngozi, nao watamwua. Ndipo atafufuka baada ya siku ya tatu.”
Yesu Amponya Asiyeona
(Mt 20:29-34; Lk 18:35-43)
46 Kisha wakafika Yeriko. Yesu alipokuwa akiondoka mjini na wanafunzi wake pamoja na umati wa watu, Bartimayo mwana wa Timayo, ombaomba asiyeona, alikuwa amekaa kando ya barabara. 47 Aliposikia kwamba huyo alikuwa ni Yesu wa Nazareti, alianza kupiga kelele na kusema, “Yesu Mwana wa Daudi, unihurumie!”
48 Na watu wengi walimkemea na kumwambia anyamaze kimya. Lakini yeye alipiga kelele kwa sauti kubwa zaidi na kusema, “Mwana wa Daudi, unihurumie!”
49 Kwa hiyo Yesu akasimama na kusema, “Hebu mwiteni.”
Nao wakamwita yule mtu asiyeona na kumweleza, “Jipe moyo mkuu! Inuka! Yesu anakuita.” 50 Naye akalitupa joho lake, akaruka juu, na akamwendea Yesu.
51 Naye Yesu akamwambia, “Unataka nikufanyie nini?”
Yule mtu asiyeona akamwambia, “Mwalimu, nataka kuona tena.”
52 Hivyo Yesu akamwambia, “Nenda! Imani yako imekuponya.”[a] Na mara akaweza kuona tena, na akamfuata Yesu barabarani.
© 2017 Bible League International