Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
5 Ndivyo ilivyo hata kwa Kristo. Hakujichagua mwenyewe kuwa na heshima na kuwa kuhani mkuu. Lakini Mungu alimchagua. Mungu akamwambia:
“Wewe ni mwanangu.
Leo nimekuwa baba yako.”(A)
6 Na katika sehemu nyingine ya Maandiko Mungu anasema:
“Wewe ni kuhani mkuu milele;
kama Melkizedeki alivyokuwa kuhani.”(B)
7 Yesu alipoishi duniani alimwomba Mungu, akiusihi msaada kutoka kwa yule anayeweza kumwokoa kutoka mauti. Alimwomba Mungu kwa sauti kuu na kwa machozi. Na Mungu alizisikia sala zake kwa sababu ya heshima yake kuu kwa Mungu. 8 Yesu alikuwa mwana wa Mungu, lakini aliteseka, na kwa njia ya mateso yake alijifunza kutii chochote alichosema Mungu. 9 Hili lilimfanya yeye awe kuhani mkuu mkamilifu, anayetoa njia kwa ajili ya kila mmoja anayemtii ili kuokolewa milele. 10 Mungu alimfanya yeye kuhani mkuu, kama alivyokuwa Melkizedeki.
Yesu Azungumza Juu Uzima na Kifo
20 Hapo Yerusalemu walikuwepo pia Wayunani. Hawa walikuwa ni miongoni mwa watu walioenda mjini humo kuabudu wakati wa sikukuu ya Pasaka. 21 Hao walimwendea Filipo, aliyetoka Bethsaida kule Galilaya. Wakasema, “Bwana, tunahitaji kumwona Yesu.” 22 Filipo alienda na kumwambia Andrea hitaji lao. Kisha Andrea na Filipo walienda na kumwambia Yesu.
23 Yesu akawaambia Filipo na Andrea, “Wakati umefika kwa Mwana wa Adamu kuupokea utukufu wake. 24 Ni ukweli kwamba mbegu ya ngano inapaswa kuanguka katika ardhi na kuoza kabla ya kukua na kuzaa nafaka nyingi ya ngano. Kama haitakufa, haitaongezeka zaidi ya hiyo mbegu moja. 25 Yeyote anayeyapenda maisha yake aliyonayo atayapoteza. Yeyote atakayetoa maisha yake kwa Yesu katika ulimwengu huu atayatunza. Nao wataupata uzima wa milele. 26 Kama mtu atanitumikia inampasa anifuate. Watumishi wangu watakuwa pamoja nami popote nitakapokuwa. Mtu atakayenitumikia Baba yangu atamheshimu.
Yesu Azungumza Kuhusu Kifo Chake
27 Sasa ninapata taabu sana rohoni mwangu. Nisemeje? Je, niseme, ‘Baba niokoe katika wakati huu wa mateso’? Hapana, nimeufikia wakati huu ili nipate mateso. 28 Baba yangu, ufanye yale yatakayokuletea wewe utukufu!”
Kisha sauti kutoka mbinguni ikasikika ikisema, “Tayari nimekwisha upata utukufu wangu. Nitaupata tena.”
29 Watu waliokuwa wamesimama hapo wakaisikia sauti hiyo. Wakasema ilikuwa ni ngurumo. Lakini wengine wakasema, “Malaika amesema naye!”
30 Yesu akasema, “Sauti hiyo ilikuwa ni kwa ajili yenu si kwa ajili yangu. 31 Sasa ni wakati wa ulimwengu kuhukumiwa. Sasa mtawala wa ulimwengu[a] huu atatupwa nje. 32 Nami nitainuliwa juu[b] kutoka katika nchi. Mambo hayo yatakapotokea, nitawavuta watu wote waje kwangu.” 33 Yesu alisema hili kuonesha jinsi ambavyo atakufa.
© 2017 Bible League International