Revised Common Lectionary (Semicontinuous)
Petro Azungumza na Watu
14 Ndipo Petro akasimama akiwa pamoja na mitume wengine kumi na moja. Akapaza sauti ili watu wote waweze kusikia. Alisema, “Ndugu zangu Wayahudi, nanyi nyote mnaoishi Yerusalemu. Nitawaeleza kuhusu jambo lililotokea, nisikilizeni kwa makini. 15 Watu hawa hawajalewa kwa mvinyo kama mnavyodhani; bado ni saa tatu asubuhi. 16 Lakini Nabii Yoeli aliandika kuhusu jambo hili mnaloliona likitokea hapa. Aliandika:
17 ‘Mungu anasema: Katika siku za mwisho,
nitaimimina Roho yangu kwa watu wote.
Wana wenu na binti zenu watatabiri.
Vijana wenu wataona maono,
na wazee wenu wataota ndoto.
18 Katika siku hizo nitaimimina Roho
yangu kwa watumishi wangu,
wanaume na wanawake, nao watatabiri.
19 Nitafanya maajabu juu angani.
Nitasababisha ishara chini duniani.
Kutakuwa damu, moto na moshi mzito.
20 Jua litakuwa giza,
na mwezi utakuwa mwekundu kama damu
kabla ya ile siku kuu yenye utukufu ya Bwana kuja.
21 Na kila amwombaye Bwana’[a] ataokolewa.(A)
22 Ndugu zangu Waisraeli, sikilizeni ninayowaambia: Mungu aliwaonesha wazi kuwa Yesu kutoka Nazareti alikuwa mtu wake. Mungu alilithibitisha hili kwa miujiza, maajabu na ishara alizotenda Yesu. Ninyi nyote mliyaona mambo haya, na mnajua hii ni kweli. 23 Yesu aliletwa kwenu, nanyi mkamwua. Kwa kusaidiwa na watu wasioijali sheria yetu, mlimpigilia msalabani. Lakini Mungu alijua hili lingetokea. Ulikuwa mpango wake, mpango alioutengeneza tangu mwanzo. 24 Yesu aliteseka kwa maumivu makali ya kifo, lakini Mungu alimweka huru. Akamfufua kutoka kwa wafu. Mauti ilishindwa kumshikilia.
© 2017 Bible League International