Revised Common Lectionary (Complementary)
Ibada Chini ya Patano Jipya
11 Lakini Kristo tayari amekuja awe kuhani mkuu. Yeye ni kuhani mkuu wa mambo mema tuliyonayo sasa. Lakini Kristo hatumiki ndani ya eneo kama hema ambalo makuhani wale walitumika ndani yake. Anatumika katika eneo bora zaidi. Tofauti na hema lile, hili ni kamilifu. Halikutengenezwa hapa duniani. Siyo la ulimwengu huu. 12 Kristo aliingia Patakatifu Zaidi mara moja tu; hii ilitosha kwa nyakati zote. Aliingia Patakatifu Zaidi kwa kutumia damu yake mwenyewe, siyo damu ya mbuzi au ya ng'ombe wadogo. Aliingia hapo na kutuweka huru milele kutoka katika dhambi.
13 Damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ng'ombe zilinyunyizwa juu ya wale ambao hawakuwa safi vya kutosha tena kuweza kuingia katika eneo la kuabudia. Damu na majivu viliwafanya wawe safi tena, lakini katika miili yao tu. 14 Hivyo hakika sadaka ya damu ya Kristo inaweza kufanya mambo bora zaidi. Kristo alijitoa mwenyewe kupitia Roho wa milele kama sadaka kamilifu kwa Mungu. Damu yake itatutakasa kabisa sisi kutoka katika maovu tuliyotenda. Itatupa sisi dhamiri safi ili tuweze kumwabudu Mungu aliye hai.
15 Hivyo Kristo huwaletea watu wake agano jipya kutoka kwa Mungu. Huleta agano hili ili wale walioteuliwa na Mungu waweze kuzipata baraka ambazo Mungu aliwaahidi, baraka zinazodumu milele. Hili laweza kutokea tu kwa sababu Kristo alikufa ili awaweke huru watu kutokana na dhambi zilizotendwa dhidi ya amri za agano la kwanza.
Mwanamke Ampa Yesu Heshima
(Mt 26:6-13; Mk 14:3-9)
12 Siku sita kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu alienda Bethania. Huko ndiko alikoishi Lazaro, yule mtu aliyefufuliwa na Yesu kutoka wafu. 2 Hapo walimwandalia Yesu karamu ya chakula. Naye Martha alihudumu na Lazaro alikuwa mmoja wa watu waliokuwa wakila chakula pamoja na Yesu. 3 Mariamu akaleta manukato ya thamani sana yaliyotengenezwa kwa nardo asilia kwenye chombo chenye ujazo wa nusu lita[a] hivi. Akayamwaga manukato hayo miguuni mwa Yesu. Kisha akaanza kuifuta miguu ya Yesu kwa nywele zake. Harufu nzuri ya manukato hayo ikajaa nyumba nzima.
4 Yuda Iskariote, mmoja wa wafuasi wa Yesu, naye alikuwepo hapo. 5 Yuda ambaye baadaye angemkabidhi Yesu kwa maadui zake akasema, “Manukato hayo yana thamani ya mshahara wa mwaka[b] wa mtu. Bora yangeuzwa, na fedha hizo wangepewa maskini.” 6 Lakini Yuda hakusema hivyo kwa vile alikuwa anawajali sana maskini. Alisema hivyo kwa sababu alikuwa mwizi. Naye ndiye aliyetunza mfuko wa fedha za wafuasi wa Yesu. Naye mara kadhaa aliiba fedha kutoka katika mfuko huo.
7 Yesu akajibu, “Msimzuie. Ilikuwa sahihi kwake kutunza manukato haya kwa ajili ya siku ya leo; siku ambayo maziko yangu yanaandaliwa. 8 Nyakati zote mtaendelea kuwa pamoja na hao maskini.[c] Lakini si kila siku mtakuwa pamoja nami.”
Mpango Dhidi ya Lazaro
9 Wayahudi wengi wakasikia kwamba Yesu alikuwa Bethania, Kwa hiyo walienda huko ili wakamwone. Walienda pia ili kumwona Lazaro, yule ambaye Yesu alimfufua kutoka wafu. 10 Viongozi wa makuhani nao wakafanya mpango wa kumuua Lazaro. 11 Walitaka kumwua kwa sababu, Wayahudi wengi waliwaacha makuhani hao na kumwamini Yesu.
© 2017 Bible League International