Revised Common Lectionary (Complementary)
Mfano wa Ibrahimu
4 Basi tuseme nini kuhusu Ibrahimu,[a] baba wa watu wetu? 2 Ikiwa Ibrahimu alifanywa kuwa mwenye haki kutokana na matendo yake, hicho ni kitu cha kujivunia! Lakini kama Mungu aonavyo, hakuwa na sababu ya kujivuna. 3 Hili ni wazi kama Maandiko yanavyosema, “Ibrahimu alimwamini Mungu, na kwa sababu ya kuamini kwake, Mungu alimhesabu kuwa mwenye haki.”[b]
4 Watu wanapofanya kazi, mshahara wao hautolewi kama zawadi. Ni kitu wanachopata kutokana na kazi waliyofanya. 5 Lakini watu hawawezi kufanya kazi yoyote itakayowafanya wahesabiwe kuwa wenye haki mbele za Mungu. Hivyo ni lazima wamtumaini Yeye. Kisha huikubali imani yao na kuwahesabia haki. Yeye ndiye anayewahesabia haki hata waovu. 6 Daudi alisema mambo hayo hayo alipozungumzia baraka wanazopata watu pale Mungu anapowahesabia haki pasipo kuangalia matendo yao:
7 “Ni heri kwa watu
wanaposamehewa kutokana na mabaya waliyotenda,
dhambi zao zinapofutwa!
8 Ni heri kwa watu,
Bwana anapozifuta dhambi zao kutoka katika kumbukumbu yake!”(A)
9 Je, baraka hii ni kwa ajili ya waliotahiriwa tu? Au pia ni kwa ajili ya wale wasiotahiriwa? Tumekwisha sema ya kwamba Ibrahimu alikubaliwa kuwa ni mwenye haki mbele za Mungu kutokana na imani yake. 10 Sasa katika mazingira gani hili lilitokea? Je, Mungu alimkubali Ibrahimu na kumhesabia haki kabla au baada ya kutahiriwa? Mungu alimkubali kabla ya kutahiriwa kwake. 11 Ibrahimu alitahiriwa baadaye ili kuonesha kuwa Mungu amemkubali kuwa mwenye haki. Tohara yake ilikuwa uthibitisho kwamba Mungu alimhesabia haki kwa njia ya imani hata kabla ya kutahiriwa. Hivyo Ibrahimu ni baba wa wote wanaoamini lakini hawajatahiriwa. Kama Ibrahimu, wao pia wamekubaliwa na Mungu kuwa wenye haki kwa sababu ya imani yao tu. 12 Pia Ibrahimu ni baba wa waliotahiriwa, lakini si kwa sababu ya kutahiriwa kwao. Ni baba yao kwa sababu wao nao wamemwamini Mungu vile vile kama Ibrahimu alivyofanya kabla hajatahiriwa.
© 2017 Bible League International