Revised Common Lectionary (Complementary)
12 Kwa sababu tuna tumaini hili tunatenda kwa ujasiri mkubwa. 13 Hatuko kama Musa, ambaye alifunika uso wake ili watu wa Israel wasiendelee kuona kuwa utaratibu wa zamani wa kumtumikia Mungu ulikuwa unaelekea mwisho. 14 Lakini mioyo yao ilikuwa imefungwa. Na hata leo, watu wale wanapolisoma agano la kale, fahamu zao zinakuwa zimefunikwa. Ni kwa kupitia Yesu Kristo tu agano la kale linaondolewa. 15 Ndiyo, hata leo, wanaposoma sheria ya Musa, fahamu zao zimefunikwa. 16 Lakini, kama maandiko yanavyosema juu ya Musa, “Kila anapomgeukia Bwana, ufahamu wake unafunuliwa.” 17 Katika maandiko hayo Bwana ni Roho, na palipo na Roho wa Bwana, pana uhuru. 18 Na sura zetu hazikufunikwa. Sote tunaendelea kuutazama utukufu wa Bwana, na tunabadilishwa na kufanana na mfano huo huo tunaouona. Badiliko hili linatuletea utukufu zaidi na zaidi, na linatoka kwa Bwana, ambaye ni Roho.
Hazina ya kiroho katika Vyungu vya Udongo
4 Mungu, kwa rehema zake, alitupa sisi huduma hii ili tuifanye, hivyo hatukati tamaa. 2 Lakini tumekataa mambo ya aibu ya siri. Hatumdanganyi mtu yeyote, na hatuyabadilii mafundisho ya Mungu. Tunaifundisha kweli wazi wazi. Na hivi ndivyo watu wanaweza kutambua mioyoni mwao sisi ni watu wa namna gani mbele za Mungu.
Yesu Aonekana Akiwa na Musa na Eliya
(Mt 17:1-8; Mk 9:2-8)
28 Baada ya siku kama nane tangu Yesu aseme maneno haya, aliwachukua Petro, Yohana na Yakobo, akapanda mlimani kuomba. 29 Yesu alipokuwa akiomba, uso wake ulianza kubadilika. Nguo zake zikawa nyeupe, zikang'aa. 30 Kisha watu wawili walikuwa pale, wakiongea naye. Walikuwa Musa na Eliya; 31 Wao pia walionekana waking'aa na wenye utukufu. Walikuwa wanazungumza na Yesu kuhusu kifo chake kitakachotokea Yerusalemu. 32 Petro na wenzake walikuwa wanasinzia. Lakini waliamka na kuuona utukufu wa Yesu. Waliwaona pia watu wawili waliokuwa wamesimama pamoja naye. 33 Musa na Eliya walipokuwa wanaondoka, Petro akasema, “Mkuu, ni vizuri tuko hapa. Tutajenga vibanda vitatu hapa, kimoja kwa ajili ya kukutukuza wewe, kingine kwa ajili kumtukuza Musa na kingine wa ajili ya kumtukuza Eliya.” Petro hakujua alichokuwa anasema.
34 Petro alipokuwa akisema mambo haya, wingu likaja, likawafunika wote. Petro, Yohana na Yakobo waliogopa walipofunikwa na wingu. 35 Sauti ikatoka katika wingu na kusema, “Huyu ni Mwanangu. Ndiye niliyemchagua. Mtiini yeye.”
36 Sauti hiyo ilipomalizika, Yesu peke yake ndiye alikuwa pale. Petro, Yohana na Yakobo hawakusema chochote. Na kwa muda mrefu baada ya hilo, hawakumwambia mtu yeyote yale waliyoyaona.
Yesu Amweka Huru Mvulana Kutoka Pepo Mchafu
(Mt 17:14-18; Mk 9:14-27)
37 Siku iliyofuata, Yesu, Petro, Yohana na Yakobo walitelemka kutoka mlimani. Kundi kubwa la watu likaenda kukutana naye. 38 Mtu mmoja katika umati huo alimwita Yesu akisema, “Mwalimu, tafadhali njoo umwonee mwanangu. Ni mtoto pekee niliye naye. 39 Pepo mchafu humvaa na hupiga kelele, humtia kifafa na kumtoa povu mdomoni. Huendelea kumwumiza na hamwachi kirahisi. 40 Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe pepo huyu mchafu lakini wameshindwa.”
41 Yesu akajibu, “Enyi watu msio na imani. Maisha yenu ni mabaya. Nitakaa na kuchukuliana nanyi mpaka lini?” Ndipo Yesu akamwambia yule mtu, “Mlete kijana wako hapa.”
42 Kijana alipokuwa anakwenda kwa Yesu, pepo mchafu akamwangusha chini na kumtia kifafa. Lakini Yesu akamwamuru atoke. Kijana akaponywa, na Yesu akampeleka kwa baba yake. 43 Watu wote wakaushangaa ukuu wa nguvu ya Mungu.
Yesu Azungumza Kuhusu Kifo Chake
(Mt 17:22-23; Mk 9:30-32)
Watu walipokuwa bado wanayashangaa mambo yote aliyofanya Yesu. Akawaambia wanafunzi wake,
© 2017 Bible League International