Revised Common Lectionary (Complementary)
Nguvu ya Mungu na Hekima Katika Kristo Yesu
18 Mafundisho kuhusu msalaba yanaonekana ni ya kipuuzi kwao wao wanaoelekea kwenye uharibifu. Lakini ni nguvu ya Mungu kwetu sisi tunaookolewa. 19 Kama Maandiko yanavyosema,
“Nitaiharibu hekima ya wenye hekima.
Nitaukanganya uelewa wa wenye akili.”(A)
20 Je, hii inasema nini kuhusu mwenye hekima, mtaalamu wa sheria au yeyote katika ulimwengu huu mwenye ujuzi wa kutengeneza hoja zenye nguvu? Mungu ameifanya hekima ya ulimwengu kuwa upuuzi. 21 Hii inadhihirisha wazi kuwa, Mungu katika hekima yake aliamua kuwa hawezi kupatikana kwa kutumia hekima ya ulimwengu. Hivyo Mungu aliutumia ujumbe unaoonekana kuwa upuuzi kuwaokoa wale wanaouamini.
22 Na hii ndiyo sababu Wayahudi wanataka ishara za miujiza na Wayunani wanataka hekima. 23 Lakini ujumbe tunaomwambia kila mtu unahusu Masihi aliyekufa msalabani. Ujumbe huu ni kikwazo kwa Wayahudi na kwa Wayunani ni upuuzi. 24 Lakini kwa Wayahudi na Wayunani walioteuliwa na Mungu, Masihi huyu aliyesulibiwa ni nguvu ya Mungu na hekima ya Mungu. 25 Maana upumbavu wa Mungu ni hekima zaidi ya hekima ya kibinadamu, na udhaifu wa Mungu ni nguvu zaidi ya nguvu ya kibinadamu.
26 Kaka na dada zangu, fikirini kuhusu hili kwamba Mungu aliwachagua ili muwe milki yake. Wachache wenu mlikuwa na hekima kwa namna dunia inavyoichukulia hekima. Wachache wenu mlikuwa mashuhuri na wachache wenu mnatoka katika familia maarufu. 27 Lakini Mungu aliyachagua mambo ambayo wanadamu huyachukulia kuwa ya kipumbavu ili ayaaibishe yenye hekima. Aliyachagua mambo yanayoonekana kuwa manyonge ili ayaaibishe yenye nguvu. 28 Aliwachagua wasio kitu ili ayaangamize yale ambayo ulimwengu unadhani ni muhimu. 29 Mungu alifanya hivi ili mtu yeyote asisimame mbele zake na akajisifu kuwa yeye ni bora kuliko mwingine. 30 Lakini Mungu ameyafungamanisha maisha yenu na Kristo Yesu. Yeye alifanywa kuwa hekima yetu kutoka kwa Mungu. Na kupitia kwake tumehesabiwa haki na Mungu na tumefanywa kuwa watakatifu. Kristo ndiye aliyetuokoa, akatufanya watakatifu na akatuweka huru mbali na dhambi. 31 Hivyo, kama Maandiko yanavyosema, “Kila anayejisifu, ajisifu juu ya Bwana tu.”(B)
© 2017 Bible League International