Revised Common Lectionary (Complementary)
15 Sisi ni Wayahudi kwa kuzaliwa. Hatukuzaliwa tukiwa ‘watenda dhambi’, kama vile Wayahudi wanavyowaita wale wasio Wayahudi. 16 Lakini tunajua kuwa hakuna mtu anayehesabiwa haki mbele za Mungu kwa kuifuata sheria. Ni kwa kuamini katika[a] Yesu Kristo ndiko kunamfanya mtu ahesabiwe haki mbele za Mungu. Hivyo hata nasi Wayahudi tumeiweka imani yetu katika Kristo Yesu, kwa sababu tulitaka kuhesabiwa haki mbele za Mungu. Na tumehesabiwa haki kwa imani[b] ya Yesu Kristo, siyo kwa sababu tuliifuata sheria. Naweza kusema hili kwa sababu hakuna anayeweza kuhesabiwa haki kwa kuifuata Sheria ya Musa.
17 Kwa hiyo tunaamini uhusiano wetu kwa Kristo utatufanya tuhesabiwe haki mbele za Mungu. Ikiwa hiyo inatufanya tuonekane kama ‘watenda dhambi’ wasio Wayahudi, je itakuwa na maana kuwa Kristo anasababisha dhambi kuongezeka. Kwa hakika sivyo? 18 Sheria ilijenga ukuta baina yetu Wayahudi na watu wengine wote, ukuta ambao nilijitahidi kuuvunja. Kweli nitakosea sana kuujenga tena ukuta huo. 19 Sheria yenyewe iliyafikisha mwisho maisha yangu chini ya sheria. Nikafa katika sheria hiyo na kuwa huru ili niweze kuishi kwa ajili ya Mungu. Nimepigiliwa misumari msalabani pamoja na Kristo. 20 Hivyo siyo mimi ninayeishi sasa; ni Kristo ndiye anayeishi ndani yangu. Bado naishi katika mwili wangu, lakini naishi kwa imani katika Mwana wa Mungu aliyenipenda na kujitoa mwenyewe kuniokoa mimi. 21 Si mimi ninayeikataa neema ya Mungu kama vile haina manufaa yoyote. Kwa sababu ikiwa kwa kuifuata sheria ndivyo watu wanahesabiwa haki mbele za Mungu, basi Kristo alikufa pasipo faida!”
Yesu na Mwanamke Mwenye Dhambi
36 Mmoja wa Mafarisayo alimwalika Yesu kula chakula nyumbani mwake. Yesu akaenda nyumbani kwa yule Farisayo, akaketi[a] katika nafasi yake sehemu ya kulia chakula.
37 Alikuwepo mwanamke mmoja katika mjini ule aliyekuwa na dhambi nyingi. Alipojua kuwa Yesu alikuwa anakula chakula nyumbani kwa Farisayo, alichukua chupa kubwa yenye manukato ya thamani sana. 38 Alisimama karibu na miguu ya Yesu akilia. Kisha alianza kuisafisha miguu ya Yesu kwa machozi yake na akaifuta kwa nywele zake, akaibusu mara nyingi na kuipaka manukato.
39 Farisayo aliyemwalika Yesu alipoona hili, alijisemea moyoni mwake, “Mtu huyu angekuwa nabii, angetambua kuwa mwanamke huyu anayemgusa ni mwenye dhambi.”
40 Katika kujibu kile Farisayo alichokuwa akifikiri, Yesu akasema, “Simoni nina kitu cha kukwambia.”
Simoni akajibu, “Nieleze, Mwalimu.”
41 Yesu akasema, “Kulikuwa watu wawili. Wote wawili walikuwa wanadaiwa na mkopeshaji mmoja. Mmoja alidaiwa sarafu mia tano za fedha, na wa pili sarafu hamsini za fedha. 42 Watu wale hawakuwa na fedha, hivyo hawakuweza kulipa madeni yao. Lakini mkopeshaji aliwasamehe wote wawili. Kati ya wote wawili ni yupi atakayempenda mkopeshaji zaidi?”
43 Simoni akajibu, “Nafikiri ni yule aliyekuwa anadaiwa fedha nyingi.”
Yesu akamwambia, “Umejibu sawa.” 44 Kisha akamgeukia yule mwanamke na kumwambia Simoni, “Unamwona mwanamke huyu? Nilipoingia nyumbani mwako hukunipa maji ili ninawe miguu yangu. Lakini mwanamke huyu ameniosha miguu yangu kwa machozi yake na kuikausha kwa nywele zake. 45 Wewe hukunisalimu kwa busu, lakini amekuwa akinibusu miguu yangu tangu nilipoingia. 46 Hukuniheshimu kwa mafuta kwa ajili ya kichwa changu, lakini yeye amenipaka miguu yangu manukato yanayonukia vizuri. 47 Ninakwambia kuwa dhambi zake zilizo nyingi zimesamehewa. Hii ni wazi, kwa sababu ameonesha upendo mkubwa. Watu wanaosamehewa kidogo hupenda kidogo.”
48 Kisha akamwambia mwanamke, “Dhambi zako zimesamehewa.”
49 Watu waliokaa naye sehemu ya chakula wakaanza kusema mioyoni mwao, “Mtu huyu anadhani yeye ni nani? Anawezaje kusamehe dhambi?”
50 Yesu akamwambia mwanamke, “Kwa sababu uliamini, umeokolewa kutoka katika dhambi zako. Nenda kwa amani.”
Yesu Akiwa Galilaya
8 Siku iliyofuata, Yesu alisafiri kupitia katika baadhi ya miji na vijiji. Yesu aliwahubiri watu Habari Njema kuhusu ufalme wa Mungu. Mitume kumi na wawili walikuwa pamoja naye. 2 Walikuwepo pia baadhi ya wanawake ambao Yesu aliwaponya magonjwa na pepo wabaya. Mmoja wao alikuwa Mariamu aitwaye Magdalena ambaye alitokwa na pepo saba; 3 Pia pamoja na wanawake hawa alikuwepo Yoana mke wa Kuza (msimamizi wa mali za Herode), Susana, na wanawake wengine wengi. Wanawake hawa walitumia fedha zao kuwahudumia Yesu na mitume wake.
© 2017 Bible League International