Revised Common Lectionary (Complementary)
Zakayo
19 Yesu alikuwa anasafiri kupitia katika mji wa Yeriko. 2 Katika mji wa Yeriko alikuwepo mtu aliyeitwa Zakayo. Alikuwa mtoza ushuru mkuu na alikuwa tajiri. 3 Alitaka kumwona Yesu na watu wengine wengi walitaka kumwona Yesu pia. Lakini alikuwa mfupi na hakuweza kuona juu ya watu. 4 Hivyo alikimbia akaenda mahali alipojua kuwa Yesu angepita. Kisha akapanda mkuyu ili aweze kumwona Yesu.
5 Yesu alipofika mahali alipokuwa Zakayo, alitazama juu na kumwona akiwa kwenye mti. Yesu akasema, “Zakayo, shuka upesi! Ni lazima nikae nyumbani mwako leo.”
6 Zakayo alishuka chini haraka. Alifurahi kuwa na Yesu nyumbani mwake. 7 Kila mtu aliliona hili na watu wakaanza kulalamika, wakisema, “Tazama aina ya mtu ambaye Yesu anakwenda kukaa kwake. Zakayo ni mwenye dhambi!”
8 Zakayo akamwambia Bwana, “Sikiliza Bwana nitawapa maskini nusu ya pesa zangu. Ikiwa nilimdhulumu mtu yeyote, nitamrudishia mara nne zaidi.”
9 Yesu akasema, “Leo ni siku kwa ajili ya familia hii kuokolewa kutoka katika dhambi. Ndiyo, hata mtoza ushuru huyu ni mmoja wa wateule wa Mungu.[a] 10 Mwana wa Adamu alikuja kuwatafuta na kuwaokoa watu waliopotea.”
© 2017 Bible League International