Revised Common Lectionary (Complementary)
Nani anaweza kukifungua kitabu?
5 Kisha niliona kitabu[a] katika mkono wa kulia wa aliyekaa kwenye kiti cha enzi. Kitabu hiki kilikuwa na maandishi pande zote na kilikuwa kimefungwa kwa mihuri saba. 2 Na nikamwona malaika mwenye nguvu, aliyeita kwa sauti kubwa, “Ni nani anayestahili kuivunja mihuri na kukifungua kitabu?” 3 Lakini hakukuwa yeyote mbinguni au duniani au chini ya dunia ambaye angeweza kukifungua kitabu na kutazama ndani yake. 4 Nililia sana kwa sababu hakuwepo aliyestahili kukifungua kitabu na kuangalia ndani yake. 5 Lakini mmoja wa wazee akaniambia, “Usilie! Simba[b] kutoka kabila la Yuda ameshinda. Ni mzaliwa wa Daudi. Anaweza kukifungua kitabu na mihuri yake saba.”
6 Kisha nikamwona Mwanakondoo amesimama katikati karibu na kiti cha enzi kilichozungukwa na viumbe wanne wenye uhai. Wazee pia walikuwa wamemzunguka Mwanakondoo aliyeonekana kama aliyeuawa. Alikuwa na pembe saba na macho saba, ambayo ni roho saba za Mungu zilizotumwa ulimwenguni kote. 7 Mwanakondoo alikuja na akakichukua kile kitabu kutoka katika mkono wa kulia wa yule aliyeketi kwenye kiti enzi. 8 Baada ya Mwanakondoo kukichukua kile kitabu, viumbe wenye uhai wanne na wazee ishirini na wanne wakainama mbele za Mwanakondoo. Kila mmoja wao alikuwa na kinubi. Pia walikuwa wameshikilia bakuli za dhahabu zilizojaa ubani, ambao ni maombi ya watu watakatifu wa Mungu. 9 Na wote walimwimbia wimbo mpya Mwanakondoo:
“Unastahili kukichukua kitabu
na kuifungua mihuri yake,
kwa sababu uliuawa,
na kwa sadaka ya damu yako uliwanunua watu kwa ajili ya Mungu,
kutoka kila kabila, lugha, rangi na taifa.
10 Uliwafanya kuwa ufalme na makuhani kwa ajili ya Mungu wetu.
Nao watatawala duniani.”
© 2017 Bible League International