Old/New Testament
Mwanamke Ampa Yesu Heshima
(Mt 26:6-13; Mk 14:3-9)
12 Siku sita kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu alienda Bethania. Huko ndiko alikoishi Lazaro, yule mtu aliyefufuliwa na Yesu kutoka wafu. 2 Hapo walimwandalia Yesu karamu ya chakula. Naye Martha alihudumu na Lazaro alikuwa mmoja wa watu waliokuwa wakila chakula pamoja na Yesu. 3 Mariamu akaleta manukato ya thamani sana yaliyotengenezwa kwa nardo asilia kwenye chombo chenye ujazo wa nusu lita[a] hivi. Akayamwaga manukato hayo miguuni mwa Yesu. Kisha akaanza kuifuta miguu ya Yesu kwa nywele zake. Harufu nzuri ya manukato hayo ikajaa nyumba nzima.
4 Yuda Iskariote, mmoja wa wafuasi wa Yesu, naye alikuwepo hapo. 5 Yuda ambaye baadaye angemkabidhi Yesu kwa maadui zake akasema, “Manukato hayo yana thamani ya mshahara wa mwaka[b] wa mtu. Bora yangeuzwa, na fedha hizo wangepewa maskini.” 6 Lakini Yuda hakusema hivyo kwa vile alikuwa anawajali sana maskini. Alisema hivyo kwa sababu alikuwa mwizi. Naye ndiye aliyetunza mfuko wa fedha za wafuasi wa Yesu. Naye mara kadhaa aliiba fedha kutoka katika mfuko huo.
7 Yesu akajibu, “Msimzuie. Ilikuwa sahihi kwake kutunza manukato haya kwa ajili ya siku ya leo; siku ambayo maziko yangu yanaandaliwa. 8 Nyakati zote mtaendelea kuwa pamoja na hao maskini.[c] Lakini si kila siku mtakuwa pamoja nami.”
Mpango Dhidi ya Lazaro
9 Wayahudi wengi wakasikia kwamba Yesu alikuwa Bethania, Kwa hiyo walienda huko ili wakamwone. Walienda pia ili kumwona Lazaro, yule ambaye Yesu alimfufua kutoka wafu. 10 Viongozi wa makuhani nao wakafanya mpango wa kumuua Lazaro. 11 Walitaka kumwua kwa sababu, Wayahudi wengi waliwaacha makuhani hao na kumwamini Yesu.
Yesu Anaingia Yerusalemu Kama Mfalme
(Mt 21:1-11; Mk 11:1-11; Lk 19:28-40)
12 Siku iliyofuata watu waliokuwamo Yerusalemu walisikia kwamba Yesu alikuwa anakuja huko. Hili ni kundi la watu waliokuja kusherehekea sikukuu ya Pasaka. 13 Hawa walibeba matawi ya miti ya mitende na kwenda kumlaki Yesu. Pia walipiga kelele wakisema,
“‘Msifuni[d] Yeye!’
‘Karibu! Mungu ambariki yeye
ajaye kwa jina la Bwana!’(A)
Mungu ambariki Mfalme wa Israeli!”
14 Yesu akamkuta punda njiani naye akampanda, kama vile Maandiko yanavyosema,
16 Wafuasi wa Yesu hawakuyaelewa yale yaliyokuwa yanatokea wakati huo. Lakini Yesu alipoinuliwa juu kwenye utukufu, ndipo walipoelewa kuwa haya yalitokea kama ilivyoandikwa juu yake. Kisha wakakumbuka kwamba walifanya mambo haya kwa ajili ya Yesu.
17 Siku Yesu alipomfufua Lazaro kutoka wafu na kumwambia atoke kaburini walikuwepo watu wengi pamoja naye. Hawa walikuwa wakiwaeleza wengine yale aliyoyafanya Yesu. 18 Ndiyo sababu watu wengi walienda ili kumlaki Yesu; kwa kuwa walikuwa wamesikia habari za ishara hii aliyoifanya. 19 Mafarisayo nao wakasemezana wao kwa wao, “Tazameni! Mpango wetu haufanyi kazi. Watu wote wanamfuata Yesu!”
Yesu Azungumza Juu Uzima na Kifo
20 Hapo Yerusalemu walikuwepo pia Wayunani. Hawa walikuwa ni miongoni mwa watu walioenda mjini humo kuabudu wakati wa sikukuu ya Pasaka. 21 Hao walimwendea Filipo, aliyetoka Bethsaida kule Galilaya. Wakasema, “Bwana, tunahitaji kumwona Yesu.” 22 Filipo alienda na kumwambia Andrea hitaji lao. Kisha Andrea na Filipo walienda na kumwambia Yesu.
23 Yesu akawaambia Filipo na Andrea, “Wakati umefika kwa Mwana wa Adamu kuupokea utukufu wake. 24 Ni ukweli kwamba mbegu ya ngano inapaswa kuanguka katika ardhi na kuoza kabla ya kukua na kuzaa nafaka nyingi ya ngano. Kama haitakufa, haitaongezeka zaidi ya hiyo mbegu moja. 25 Yeyote anayeyapenda maisha yake aliyonayo atayapoteza. Yeyote atakayetoa maisha yake kwa Yesu katika ulimwengu huu atayatunza. Nao wataupata uzima wa milele. 26 Kama mtu atanitumikia inampasa anifuate. Watumishi wangu watakuwa pamoja nami popote nitakapokuwa. Mtu atakayenitumikia Baba yangu atamheshimu.
© 2017 Bible League International