Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Read the New Testament in 24 Weeks

A reading plan that walks through the entire New Testament in 24 weeks of daily readings.
Duration: 168 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Mathayo 3-4

Yohana Atayarisha Njia kwa Ajili ya Yesu

(Mk 1:1-8; Lk 3:1-9,15-17; Yh 1:19-28)

Baadaye, kabla ya miaka mingi kupita, Yohana Mbatizaji alianza kuwahubiri watu ujumbe uliotoka kwa Mungu. Naye alihubiri kutokea maeneo ya nyikani huko Uyahudi. Yohana alisema, “Tubuni na kuibadili mioyo yenu, kwa sababu ufalme wa Mungu umekaribia.” Nabii Isaya alisema kuhusu habari za Yohana Mbatizaji pale aliposema,

“Kuna mtu anayeipaza sauti yake toka nyikani:
‘Tayarisheni njia kwa ajili ya Bwana;
    nyoosheni njia kwa ajili yake.’”(A)

Huyo Yohana alivaa mavazi yaliyofumwa kutokana na manyoya ya ngamia. Naye alijifunga mkanda wa ngozi kuzunguka kiuno chake, na alikula nzige na asali mbichi. Watu kutoka Yerusalemu na maeneo yote ya Uyahudi na wale kutoka maeneo yote yaliyo kando ya Mto Yordani walikwenda kwa Yohana Mbatizaji; huko waliungama matendo yao mabaya kwake naye akawabatiza katika Mto Yordani.

Mafarisayo na Masadukayo wengi walikwenda kwa Yohana ili wabatizwe. Yohana alipowaona, akasema, “Enyi ninyi nyoka! Ni nani amewaonya kuikimbia hukumu ya Mungu inayokuja? Muibadili mioyo yenu! Na muoneshe kwa vitendo kuwa mmebadilika. Ninajua mnachofikiri. Mnataka akasema kuwa, ‘lakini Ibrahimu ni baba yetu!’ Hiyo haijalishi. Ninawaambia Mungu anaweza kumzalia Ibrahimu watoto kutoka katika mawe haya. 10 Shoka limewekwa tayari kukata shina la mti katika mizizi yake. Kila mti[a] usiozaa matunda mazuri utakatwa vivyo hivyo na kutupwa motoni.

11 Mimi ninawabatiza kwa maji kuonesha kuwa mmebadilika mioyoni mwenu na pia maishani mwenu. Lakini yupo mwingine ajaye baada yangu, mwenye nguvu zaidi kuliko mimi, huyo atafanya mengi zaidi yangu. Nami niliye mtumwa wa chini kabisa sistahili hata kuinama na kufungua kamba za viatu vyake. Yeye huyo atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. 12 Naye atakuja akiwa tayari kwa ajili ya kuisafisha nafaka. Atatenganisha nafaka nzuri kutoka kwenye makapi,[b] na kisha ataiweka nafaka nzuri kwenye ghala yake. Kisha atayachoma makapi kwa moto usiozimika.”

Yohana Ambatiza Yesu

(Mk 1:9-11; Lk 3:21-22)

13 Ndipo Yesu alitoka Galilaya na kwenda Mto Yordani. Alikwenda kwa Yohana, akitaka kubatizwa. 14 Lakini Yohana alijaribu kumzuia. Yohana akamwambia Yesu, “Kwa nini unakuja kwangu ili nikubatize? Mimi ndiye ninayepaswa kubatizwa na wewe!”

15 Yesu akajibu, “Acha iwe hivyo kwa sasa. Tunapaswa kuyatimiza mapenzi ya Mungu.” Ndipo Yohana akakubali.

16 Hivyo Yesu akabatizwa. Mara tu aliposimama kutoka ndani ya maji, mbingu zilifunguka na akamwona Roho Mtakatifu akishuka kutoka mbinguni kama hua[c] na kutua juu yake. 17 Sauti kutoka mbinguni ikasema, “Huyu ni Mwanangu, nimpendaye. Ninapendezwa naye.”

Yesu Ajaribiwa na Shetani

(Mk 1:12-13; Lk 4:1-13)

Kisha Roho Mtakatifu akamwongoza Yesu hadi nyikani ili akajaribiwe na Shetani. Baada ya Yesu kufunga kwa siku arobaini mchana na usiku, akaumwa njaa sana. Mjaribu[d] akamwendea na akasema, “Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, basi yaamuru mawe haya yawe mikate.”

Yesu akajibu, “Maandiko yanasema, ‘Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila Neno linalotoka katika kinywa cha Mungu.’”(B)

Kisha Shetani alimwongoza Yesu mpaka mji mtakatifu wa Yerusalemu na akamweka juu ya mnara wa Hekalu. Akamwambia Yesu, “Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, jirushe mpaka chini! Kwani Maandiko yanasema,

‘Mungu atawaamuru malaika zake wakusaidie,
na mikono yao itakupokea,
    ili usije ukajikwaa mguu wako kwenye jiwe.’”(C)

Yesu akamjibu, “Pia, Maandiko yanasema, ‘usimjaribu Bwana Mungu wako.’”(D)

Kisha Shetani akamwongoza Yesu mpaka kwenye kilele cha mlima ulio mrefu sana na kumwonyesha falme zote za ulimwengu na vitu vya kupendeza vilivyomo ndani. Shetani akamwambia Yesu, “Ukiinama na kuniabudu, nitakupa vitu hivi vyote.”

10 Yesu akamjibu Shetani akamwambia, “Ondoka kwangu Shetani! Kwani Maandiko yanasema, ‘Umwabudu Bwana Mungu wako na umtumikie yeye peke yake!’”(E)

11 Baada ya hayo, Shetani akamwacha. Ndipo malaika wakaja kumhudumia.

Yesu Aanza Kazi yake Galilaya

(Mk 1:14-15; Lk 4:14-15)

12 Yesu aliposikia kuwa Yohana alikuwa amefungwa gerezani, alirudi katika wilaya ya Galilaya. 13 Lakini aliondoka Nazareti. Alikwenda kuishi Kapernaumu, mji ulio kando kando ya Ziwa Galilaya katika eneo la Zabuloni na Naftali. 14 Hili lilitokea ili kutimiza maneno aliyosema nabii Isaya:

15 “Sikilizeni, enyi nchi ya Zabuloni na Naftali,
    nchi iliyo kando ya barabara iendayo baharini,
    ng'ambo ya Mto Yordani!
    Galilaya, wanapokaa Mataifa.
16 Watu wanaoishi katika giza ya kiroho,
    nao wameiona nuru iliyo kuu.
Nuru hiyo imeangaza kwa ajili yao wale
    wanaoishi katika nchi yenye giza kama kaburi.”(F)

17 Tangu wakati huo Yesu alianza kuwaambia watu ujumbe wake unaosema, “Mbadili mioyo yenu na maisha yenu pia, kwa sababu Ufalme wa Mungu umewafikia.”

Yesu Achagua Baadhi ya Wafuasi

(Mk 1:16-20; Lk 5:1-11)

18 Yesu alipokuwa akitembea kando ya Ziwa Galilaya, aliwaona ndugu wawili, Simoni, aitwaye Petro na nduguye aitwaye Andrea. Ndugu hawa walikuwa wavuvi na walikuwa wanavua samaki kwa nyavu zao. 19 Yesu akawaambia, “Njooni, mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa aina nyingine. Nitawafundisha jinsi ya kukusanya watu badala ya samaki.” 20 Mara moja, Simoni na Andrea wakaziacha nyavu zao na kumfuata Yesu papo hapo.

21 Yesu akaendelea kutembea kutoka pale. Akawaona ndugu wengine wawili, Yakobo na Yohana wana wa Zebedayo. Walikuwa kwenye mashua pamoja na Zebedayo baba yao. Walikuwa wakiandaa nyavu zao za kuvulia samaki. Yesu akawaita wamfuate. 22 Mara moja wakaiacha mashua pamoja na baba yao na wakamfuata Yesu.

Yesu Afundisha na Kuponya Watu

(Lk 6:17-19)

23 Yesu alikwenda sehemu zote za Galilaya, akifundisha na akihubiri Habari Njema katika masinagogi kuhusu Ufalme wa Mungu. Aliponya magonjwa yote na madhaifu mengi ya watu. 24 Habari kuhusu Yesu zilienea katika nchi yote ya Shamu, na watu waliwaleta wale wote wenye kuteswa na magonjwa na maumivu mbalimbali. Baadhi yao walikuwa na mashetani, wengine walikuwa na kifafa na wengine walikuwa wamepooza. Yesu akawaponya wote. 25 Makundi makubwa ya watu walimfuata; watu kutoka Galilaya, na jimbo lililoitwa Miji Kumi,[e] Yerusalemu, Yuda na maeneo ng'ambo ya Mto Yordani.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International