Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

New Testament in a Year

Read the New Testament from start to finish, from Matthew to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
1 Wakorintho 7:20-40

20 Kila mmoja wenu awe katika hali aliyokuwa nayo Mungu alipomwita. 21 Usijisikie vibaya ikiwa ulipochaguliwa na Mungu ulikuwa mtumwa. Lakini ikiwa unaweza kujikomboa, basi fanya hivyo. 22 Kama ulikuwa mtumwa Bwana alipokuita, uko huru sasa katika Bwana. Wewe ni wa Bwana. Vivyo hivyo, kama ulikuwa huru ulipoitwa, wewe ni mtumwa wa Kristo sasa. 23 Mungu alilipa gharama kubwa kwa ajili yako, hivyo usiwe mtumwa kwa mtu yeyote tena. 24 Ndugu zangu, katika maisha yenu mapya pamoja na Mungu, kila mmoja wenu anapaswa kuendelea kuwa katika hali ya tohara kama alivyokuwa Mungu alipowaita.

Maswali Kuhusu Kuoa au Kuolewa

25 Sasa nitaandika kuhusu suala jingine mliloniandikia mkiuliza kuhusu watu ambao hawajaoa au kuolewa.[a] Sina amri kutoka kwa Bwana kuhusu hili, lakini haya ni maoni yangu. Na ninaweza kuaminiwa kwa sababu Bwana amenipa rehema. 26 Huu ni wakati mgumu. Hivyo nadhani ni vyema mtu akikaa kama alivyo. 27 Ikiwa umefungwa kwa mke, usijaribu kufunguliwa. Ikiwa hujaoa, usijaribu kuoa. 28 Lakini si dhambi ukiamua kuoa. Lakini waliooa watapata dhiki katika maisha haya, nami ninataka msiipitie dhiki hiyo.

29 Kaka zangu nina maana ya kuwa muda uliosalia ni mchache, wale waliooa waishi kama vile hawajaoa.[b] 30 Wale wanaolia wawe kama wasiolia, wenye furaha wawe kama hawana furaha na wale wanaonunua vitu wawe kama hawavimiliki vitu hivyo. 31 Vitumieni vitu vya ulimwengu pasipo kuviruhusu viwe vya muhimu kwenu. Hivi ndivyo mnapaswa kuishi, kwa sababu ulimwengu huu kwa namna ulivyo sasa, unapita.

32 Nataka msisumbuke. Mwanaume ambaye hajaoa hujishughulisha na kazi ya Bwana naye hujitahidi kumpendeza Bwana. 33 Lakini mwanaume aliyeoa hujishughulisha na mambo ya ulimwengu, ili ampendeze mke wake. 34 Ni lazima afikirie mambo mawili; kumpendeza mke wake na kumpendeza Bwana. Mwanamke ambaye hajaolewa au msichana ambaye hajawahi kuolewa hujishughulisha na kazi ya Bwana. Hutaka kuutoa mwili na roho yake kikamilifu kwa Bwana. Lakini mwanamke aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya ulimwengu ili ampendeze mume wake. 35 Ninasema hili ili niwasaidie. Si kuwawekea vikwazo, lakini ninataka mwishi katika njia sahihi. Na ninataka mjitoe kikamilifu kwa Bwana pasipo kuchukuliwa katika mambo mengine.

36 Mwanaume anaweza kudhani kuwa hamtendei haki mchumba wake. Mchumba wake huyo anaweza kuwa ameshapita umri mzuri wa kuolewa.[c] Hivyo mwanaume anaweza kujisikia kuwa anapaswa kumwoa mchumba wake huyo. Basi na afanye anachotaka. Si dhambi kwao wakioana. 37 Lakini mwanaume mwingine anaweza kuwa na uhakika akilini mwake ya kuwa hakuna haja ya ndoa, hivyo yuko huru kufanya anachotaka. Ikiwa ameamua moyoni mwake kutomwoa mchumba wake, anafanya jambo sahihi. 38 Hivyo mwanaume anayemwoa mchumba wake anafanya jambo jema, na mwanaume asiyeoa anafanya vyema zaidi.

39 Mwanamke anapaswa kuishi na mume wake kipindi chote mumewe anapokuwa hai. Lakini mume akifa, mwanamke anakuwa huru kuolewa na mwanaume yeyote. Lakini mwanaume huyo lazima awe yule wa Bwana. 40 Ikiwa atabaki kuwa mjane, atakuwa na furaha sana. Haya ni maoni yangu, na ninaamini yanatoka kwa Roho wa Mungu.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International