New Testament in a Year
Uzima Katika Roho
8 Hivyo mtu yeyote aliye wa Kristo Yesu hana hukumu ya kifo. 2 Hiyo ni kwa sababu kwa njia ya Kristo Yesu sheria ya Roho inayoleta uzima imewaweka ninyi[a] huru kutoka katika sheria inayoleta dhambi na kifo. 3 Ndiyo, sheria haikuwa na nguvu ya kutusaidia kwa sababu ya udhaifu wetu wa kibinadamu. Lakini Mungu akafanya kile ambacho sheria haikuweza kufanya: Alimtuma Mwanaye duniani akiwa na mwili ule ule tunaoutumia kutenda dhambi. Mungu alimtuma ili awe njia ya kuiacha dhambi. Alitumia maisha ya mwanadamu ili kuipa dhambi hukumu ya kifo. 4 Mungu alifanya hivi ili tuweze kuishi kama sheria inavyotaka. Sasa tunaweza kuishi hivyo kwa kumfuata Roho na si kwa jinsi ya udhaifu wa kibinadamu.
5 Watu wanaoishi kwa kufuata udhaifu wa kibinadamu[b] huyafikiri yale wanayoyataka tu. Lakini wale wanaoishi kwa kumfuata Roho huyafikiri yale Roho anayotaka wafanye. 6 Ikiwa fikra zenu zinaongozwa na udhaifu wa kibinadamu, kuna kifo cha kiroho. Lakini ikiwa fikra zenu zinaongozwa na Roho, kuna uhai na amani. 7 Je, hili ni kweli? Kwa sababu kila mtu ambaye fikra zake zinaongozwa na udhaifu wa kibinadamu yuko kinyume na Mungu maana hukataa kuitii sheria ya Mungu. Na kwa hakika hawawezi kutii. 8 Wale wanaotawaliwa na udhaifu wa kibinadamu hawawezi kumpendeza Mungu.
9 Lakini ninyi hamtawaliwi na udhaifu wenu wa kibinadamu, bali mnatawaliwa na Roho, ikiwa Roho huyo wa Mungu anakaa ndani yenu. Na mtu yeyote asiye na Roho wa Kristo, huyo si wa Kristo. 10 Miili yenu inaelekea kifo kwa sababu ya dhambi. Lakini ikiwa Kristo anaishi ndani yenu, basi Roho anawapa uzima kwa sababu ya uaminifu wa wema wa Mungu.[c] 11 Mungu alimfufua Yesu kutoka kwa wafu. Na ikiwa Roho wa Mungu anaishi ndani yenu, ataifanya hai tena miili yenu inayokufa. Ndiyo, Mungu ndiye aliyemfufua Kristo kutoka kwa wafu, naye atawafufua ninyi na kuwapa uzima kupitia Roho wake anayeishi ndani yenu.
12 Hivyo, kaka na dada zangu, ni lazima tusitawaliwe na udhaifu wa kibinadamu kwa kufuata tamaa zake. 13 Ikiwa mtayatumia maisha yenu kufanya yale ambayo udhaifu wenu wa kibinadamu unataka, mtakufa kiroho. Lakini ikiwa mtaupokea msaada wa Roho na mkaacha kutenda mambo mabaya mnayotenda na miili yenu, mtakuwa na uzima wa kweli.
14 Watoto wa kweli wa Mungu ni wale wanaokubali kuongozwa na Roho wa Mungu. 15 Roho tuliyempokea si roho anayetufanya kuwa watumwa tena na kutusababisha tuwe na hofu. Roho tuliye naye hutufanya tuwe watoto waliochaguliwa na Mungu. Na kwa Roho huyo twalia “Aba,[d] yaani Baba.” 16 Na Roho mwenyewe huzungumza na roho zetu na kutuhakikishia kuwa sisi ni watoto wa Mungu. 17 Nasi kwa kuwa ni watoto wa Mungu, basi sisi ni warithi, warithi wa Mungu na warithi pamoja na Kristo. Mungu atatupa yale yote aliyompa Kristo. Sisi tunaoteseka sasa kama Kristo alivyoteseka tutashiriki katika utukufu wake.
Wakati Wetu wa Utukufu Unakuja
18 Nanayachukulia mateso ya sasa kuwa si kitu ukilinganisha na utukufu mkuu tunaoutarajia. 19 Hata uumbaji una shauku kuu, ukisubiri kwa hamu wakati ambapo atawadhihirisha “watoto halisi wa Mungu”[e] kuwa ni na. 20 Kila alichokiumba Mungu kiliruhusiwa kuwa na mapungufu kana kwamba hakitafikia utimilifu wake. Hilo halikuwa kwa matakwa ya viumbe, lakini Mungu aliruhusu hayo yatokee kwa mtazamo wa tumaini hili: 21 kwamba uumbaji ungewekwa huru mbali na uharibifu, na kwamba kila alichokiumba Mungu kiwe na uhuru na utukufu ule ule ulio wa watoto wa Mungu.
© 2017 Bible League International