Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

New Testament in a Year

Read the New Testament from start to finish, from Matthew to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Warumi 11:1-18

Mungu Hajawakataa Watu wake

11 Hivyo ninauliza, “Je, Mungu aliwakataa watu wake?” Hapana! Mimi mwenyewe ni Mwisraeli, wa ukoo wa Ibrahimu, katika kabila la Benjamini. Mungu aliwachagua Waisraeli wawe watu wake kabla hawajazaliwa. Na hajawakataa. Hakika mnajua Maandiko yanavyosema kuhusu Eliya anapomwomba Mungu dhidi ya watu wa Israeli. Anasema, “Bwana, wamewaua manabii wako na kuharibu madhabahu zako. Mimi ndiye nabii pekee niliyebaki hai, na sasa wanajaribu kuniua mimi pia.”(A) Lakini ni jibu gani Mungu alilompa Eliya? Mungu alisema, “Nimejihifadhia watu elfu saba wasiomwabudu Baali.”(B)

Ndivyo ilivyo sasa. Mungu amewachagua watu wachache kwa neema yake. Na kama aliwachagua kwa neema yake, hivyo si kwa sababu ya matendo yao yaliyowafanya wawe watu wake. Kama wangefanywa kuwa watu wake kutokana na matendo yao, zawadi yake ya neema isingekuwa zawadi halisi.

Hivyo hivi ndivyo ilivyotokea: Watu wa Israeli wanazitaka sana baraka za Mungu, lakini si wote waliozipata. Watu aliowachagua walipata baraka zake, lakini wengine wakawa wagumu na wakakataa kumsikiliza. Kama Maandiko yanavyosema,

“Mungu aliwafanya watu walale usingizi.”(C)
“Mungu aliyafumba macho yao ili wasione,
    na aliyaziba masikio yao ili wasisikie.
Hili linaendelea hata sasa.”(D)

Na Daudi anasema,

“Watu hawa na wakamatwe na kunaswa
    katika tafrija wanazofurahia.
Nyakati hizo nzuri ziwasababishe waanguke
    ili wapate adhabu wanayoistahili.
10 Yapofushe macho yao ili wasiweze kuona.
    Ipindishe migongo yao kwa mzigo wa matatizo.”(E)

11 Hivyo nauliza: Pale watu wa Mungu walipojikwaa na kuanguka, Je, hawakuweza kuinuka tena? Hakika hapana! Lakini kujikwaa kwao katika mwendo kulileta wokovu kwa wale wasio Wayahudi. Kusudi la hili lilikuwa kuwafanya Wayahudi wapate wivu. 12 Kosa lao na hasara yao vilileta baraka za utajiri kwa ulimwengu kwa wasio Wayahudi. Hivyo fikirini ni kwa kiasi gani baraka hizi zitakuwa kubwa kwa ulimwengu pale idadi ya kutosha ya Wayahudi watakapokuwa watu wa aina ile anayoitaka Mungu.

13 Nasema na ninyi watu msio Wayahudi. Kwa vile mimi ndiye ambaye Mungu ameniteua niwe mtume kwa wale wasio Wayahudi, nitafanya kwa bidii yote kuiheshimu huduma hii. 14 Natarajia kuwafanya watu wangu wawe na wivu. Kwa njia hiyo, labda naweza kuwasaidia baadhi yao waweze kuokolewa. 15 Mungu aliwaacha kwa muda. Hilo lilipotokea, akawa rafiki wa watu wengine ulimwenguni. Hivyo anapowakubali Wayahudi, ni sawa na kuwafufua watu baada ya kifo. 16 Kama sehemu ya kwanza ya mkate inatolewa kwa Mungu, basi mkate mzima unakuwa umetakaswa. Kama mizizi ya mti ni mitakatifu, matawi ya mti huo pia ni matakatifu.

17 Ni kama vile baadhi ya matawi ya mzeituni yamevunjwa, na tawi la mzeituni mwitu limeunganishwa katika ule mti wa kwanza. Ikiwa wewe si Myahudi, uko sawa na tawi la mzeituni mwitu, na sasa unashiriki nguvu na uhai wa mti wa kwanza. 18 Lakini msienende kama mlio bora kuliko matawi yale yaliyovunjwa. Hamna sababu ya kujivuna, kwa sababu hamleti uhai katika mzizi. Mzizi ndiyo huleta uhai kwenu.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International