Beginning
Yesu Ajaribiwa na Shetani
(Mt 4:1-11; Mk 1:12-13)
4 Akiwa amejaa Roho Mtakatifu, Yesu akarudi kutoka Mto Yordani. Kisha Roho Mtakatifu akamwongoza mpaka nyikani 2 kwa muda wa siku arobaini, alikojaribiwa na Ibilisi. Katika muda wote huo hakula chakula chochote na baadaye akahisi njaa sana.
3 Ibilisi akamwambia, “Kama wewe ni Mwana wa Mungu, liambie jiwe hili liwe mkate.”
4 Yesu akamjibu, “Maandiko yanasema, ‘Watu hawataishi kwa mkate tu.’”(A)
5 Kisha mwovu akamchukua Yesu na kwa muda mfupi akamwonyesha falme zote za ulimwengu. 6 Mwovu akamwambia, “Nitakufanya uwe mfalme wa sehemu zote hizi. Utakuwa na mamlaka juu yao, na utapata utukufu wote. Yote yametolewa kwangu. Ninaweza kumpa yeyote kadri ninavyopenda. 7 Nitakupa vyote hivi, ikiwa utaniabudu tu.”
8 Yesu akajibu, “Maandiko yanasema, ‘Ni lazima umwabudu Bwana Mungu wako, na umtumikie yeye peke yake.’”(B)
9 Ndipo Shetani akamwongoza Yesu mpaka Yerusalemu na kumweka mahali palipo juu katika mnara wa Hekalu. Akamwambia, “Kama wewe ni Mwana wa Mungu, jirushe! 10 Kwani Maandiko yanasema,
‘Mungu atawaamuru
malaika zake wakulinde.’(C)
11 Pia imeandikwa kuwa,
‘Mikono yao itakudaka,
ili usijikwae mguu wako kwenye mwamba.’”(D)
12 Yesu akajibu, “Pia, Maandiko yanasema: ‘Usimjaribu Bwana Mungu wako.’”(E)
13 Shetani alipomaliza kumjaribu Yesu katika namna zote, alimwacha akaenda zake hadi wakati mwingine.
Yesu Aanza Kazi yake Galilaya
(Mt 4:12-17; Mk 1:14-15)
14 Yesu alirudi Galilaya akiwa na nguvu za Roho Mtakatifu. Habari zake zilisambaa katika eneo lote lililozunguka Galilaya. 15 Alianza kufundisha katika masinagogi na kila mtu alimsifu.
Yesu Aenda Kwenye Mji wa Kwao
(Mt 13:53-58; Mk 6:1-6)
16 Yesu alisafiri akaenda katika mji aliokulia wa Nazareti. Siku ya Sabato alikwenda kwenye sinagogi kama alivyokuwa akifanya. Alisimama ili asome. 17 Akapewa gombo la nabii Isaya. Akalivingirisha kulifungua na akapata mahali palipoandikwa haya:
18 “Roho wa Bwana yu juu yangu,
amenichagua ili
niwahubiri maskini habari njema.
Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao
na kuwaambia wasiyeona
kuwa wanaweza kuona tena.
Amenituma kuwapa uhuru wale wanaoteswa
19 na kutangaza kuwa wakati wa Bwana
kuonesha wema wake umefika.”(F)
20 Yesu akalivingirisha gombo akalifunga, akalirudisha kwa msaidizi na kuketi chini. Kwa kuwa kila mtu ndani ya sinagogi alimwangalia kwa makini, 21 Alianza kuzungumza nao. Akasema, “Maandiko haya yametimilika mlipokuwa mnanisikia nikiyasoma!”
22 Kila mtu pale akasema alipenda namna ambavyo Yesu alizungumza. Walishangaa kumsikia akisema maneno haya ya ajabu. Wakaulizana, “Inawezekanaje? Huyu si mwana wa Yusufu?”
23 Yesu akawaambia, “Ninafahamu mtaniambia mithali hii ya zamani: ‘Daktari, jitibu mwenyewe.’ Mnataka kusema ‘Tulisikia mambo yote uliyotenda Kapernaumu. Yatende pia hapa katika mji wako mwenyewe!’” 24 Lakini Yesu akasema, “Ukweli ni huu, nabii hakubaliki katika mji wa kwao.
25-26 Wakati wa Eliya mvua haikunyesha katika Israeli kwa miaka mitatu na nusu. Chakula hakikuwepo mahali popote katika nchi yote. Palikuwa wajane wengi katika Israeli wakati huo. Lakini Eliya hakutumwa kwenda kwa mmoja wa wajane waliokuwa katika Israeli bali kwa mjane aliyekuwa katika mji wa Sarepta, jirani na Sidoni.
27 Na, palikuwa wenye ugonjwa mbaya wa ngozi wengi walioishi katika Israeli wakati wa nabii Elisha, lakini hakuna aliyeponywa isipokuwa Naamani, aliyetoka katika nchi ya Shamu, siyo Israeli.”
28 Watu wote waliposikia hili, walikasirika sana. 29 Wakasimama na kumlazimisha Yesu atoke nje ya mji. Mji wao ulijengwa juu ya kilima. Wakamchukua Yesu mpaka ukingo wa kilima ili wamtupe. 30 Lakini alipita katikati yao na kwenda zake.
Yesu Amweka Huru Mtu Kutoka Pepo Mchafu
(Mk 1:21-28)
31 Yesu akashuka kwenda Kapernaumu, mji uliokuwa Galilaya. Siku ya Sabato aliwafundisha watu. 32 Nao walishangaa sana namna alivyokuwa akifundisha kwa sababu mafundisho yake yalikuwa na mamlaka.
33 Ndani ya sinagogi alikuwepo mtu aliyekuwa na roho chafu, kutoka kwa yule Mwovu, ndani yake. Akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, “Aiii! 34 Unataka nini kwetu Yesu wa Nazareti? Umekuja kutuangamiza? Ninajua wewe ni nani; Wewe ni Mtakatifu wa Mungu.” 35 Lakini Yesu akamkemea yule pepo na kumwambia, “Nyamaza kimya! Umtoke mtu huyu!” Ndipo pepo akamtupa yule mtu chini mbele ya watu, akamtoka bila kumjeruhi sehemu yoyote ya mwili wake.
36 Watu wakashangaa. Wakasemezana wao kwa wao, “Hii inamaanisha nini? Kwa mamlaka na uwezo anaamuru pepo wachafu na wanatoka!” 37 Hivyo habari kuhusu Yesu zikaenea kila mahali katika eneo lote.
Yesu Amponya Mkwewe Petro
(Mt 8:14-17; Mk 1:29-34)
38 Yesu akatoka katika sinagogi, akaenda nyumbani kwa Simoni.[a] Mama mkwe wa Simoni alikuwa mgonjwa sana. Alikuwa na homa kali. Nao walimwomba Yesu amsaidie. 39 Yesu alisimama karibu yake na kuiamuru homa kuondoka. Homa ikamwacha, naye akasimama na kuanza kuwahudumia.
Yesu Aponya Wengine Wengi
40 Jua lilipokuchwa, watu wote waliwaleta kwa Yesu jamaa na rafiki zao walioumwa na wenye magonjwa mengi tofauti. Yesu aliweka mikono yake juu ya kila mgonjwa na kuwaponya wote. 41 Pepo nao waliwatoka watu wengi. Mapepo yalipiga kelele yakisema “Wewe ni Mwana wa Mungu.” Lakini Yesu alitoa amri yenye nguvu kwa mapepo yasiseme, kwa sababu yalijua alikuwa ni Masihi.
Yesu Aenda Katika Miji Mingine
(Mk 1:35-39)
42 Siku iliyofuata Yesu alijitenga na kwenda mahali ili awe peke yake. Watu wakawa wakimtafuta. Walipompata, walijaribu kumzuia asiondoke. 43 Lakini akawaambia, “Ni lazima nihubiri Habari Njema kuhusu Ufalme wa Mungu katika miji mingine pia, kwa sababu nilitumwa kufanya hivyo.”
44 Kisha Yesu akahubiri Habari Njema katika masinagogi ya Uyahudi.
Yesu Achagua Baadhi ya Wafuasi
(Mt 4:18-22; Mk 1:16-20)
5 Yesu aliposimama ukingoni mwa Ziwa Galilaya[b] kundi la watu lilimsogelea ili wasikie mafundisho kuhusu Mungu. 2 Yesu aliona mashua mbili zikiwa kando ya ziwa. Wavuvi walikuwa wametoka katika mashua zao na walikuwa wanaosha nyavu zao. 3 Yesu aliingia kwenye mashua ya Simoni. Akamwomba Simoni aisogeze mbali kidogo na ufukwe wa ziwa. Kisha akaketi ndani ya mashua na akawafundisha watu waliokuwa ufukweni mwa ziwa.
4 Yesu alipomaliza kufundisha, alimwambia Simoni, “Ipeleke mashua mpaka kwenye kilindi cha maji kisha mshushe nyavu zenu majini na mtapata samaki.”
5 Simoni akamjibu, “Bwana, tumejitahidi usiku kucha kuvua samaki na hatukupata chochote. Lakini kwa kuwa unasema nishushe nyavu majini, nitafanya hivyo.” 6 Walipofanya hivi, nyavu zao zilijaa samaki wengi mpaka zikaanza kuchanika. 7 Waliwaita rafiki zao waliokuwa katika mashua nyingine ili waje wawasaidie. Rafiki zao walikuja kuwasaidia, na mashua zote mbili zilijaa samaki kiasi cha kutaka kuzama.
8-9 Wavuvi wote walistaajabu kwa sababu ya wingi wa samaki waliovua. Simoni Petro alipoona hili, akapiga magoti mbele ya Yesu na akasema, “Nenda mbali nami Bwana, mimi ni mwenye dhambi!” 10 Yakobo na Yohana wana wa Zebedayo, walishangaa pia. (Yakobo na Yohana walikuwa wanavua pamoja na Simoni.)
Yesu akamwambia Simoni, “Usiogope. Kuanzia sasa kazi yako haitakuwa kuvua samaki bali kukusanya watu!”
11 Wakaziendesha mashua zao mpaka pwani, kisha wakaacha kila kitu na kumfuata Yesu.
Yesu Amponya Mgonjwa
(Mt 8:1-4; Mk 1:40-45)
12 Wakati mmoja Yesu alikuwa katika mji ambao mwanaume mmoja mgonjwa alikuwa anaishi. Mwanaume huyo alikuwa na ugonjwa mbaya sana wa ngozi mwili wake wote. Alipomwona Yesu, alimsujudia na kumsihi akisema, “Bwana, ikiwa unataka una uwezo wa kuniponya.”
13 Yesu akasema, “Hakika ninataka kukuponya, upone!” Kisha akamgusa, na ugonjwa ukatoweka papo hapo. 14 Yesu akamwambia, “Usimwambie mtu yeyote kilichotokea. Lakini nenda kwa kuhani akakuchunguze.[c] Na umtolee Mungu sadaka ambazo Musa aliamuru watu wanaoponywa watoe, ili iwe ushahidi kwa watu kwamba umepona.”
15 Lakini habari kuhusu Yesu zilizidi kuenea zaidi. Watu wengi walikuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. 16 Mara nyingi Yesu alikwenda sehemu zingine zisizokuwa na watu na akaomba huko.
Yesu Amponya Aliyepooza
(Mt 9:1-8; Mk 2:1-12)
17 Siku moja Yesu alikuwa anawafundisha watu. Mafarisayo na walimu wa sheria walikuwa wameketi hapo pia. Walitoka katika kila mji wa Galilaya, na Uyahudi, na Yerusalemu. BWANA alimpa Yesu uwezo wa kuponya watu. 18 Alikuwepo mtu aliyepooza na baadhi ya watu walikuwa wamembeba kwenye machela. Walijaribu kumwingiza ndani ili wamweke mbele ya Yesu. 19 Lakini walishindwa kufika alipokuwa Yesu kwa sababu kulikuwa na watu wengi sana. Hivyo walikwenda juu ya paa ya nyumba na kumshusha aliyepooza chini kupitia tundu kwenye dari. Waliishusha machela alimokuwa aliyepooza kwa usawa kiasi kwamba akawa amelala mbele ya Yesu. 20 Yesu alipoona imani waliyokuwa nayo, akamwambia yule mgonjwa: “Rafiki yangu, dhambi zako zimesamehewa!”
21 Walimu wa sheria na Mafarisayo wakaanza kuhojiana wao kwa wao wakisema: “Huyu mtu ni nani kiasi cha kuthubutu kusema hivi? Si anamtukana Mungu! Mungu peke yake ndiye anayesamehe dhambi.”
22 Lakini Yesu alijua walichokuwa wanawaza, akawaambia: “Kwa nini mna maswali haya mioyoni mwenu? 23-24 Wakati akiwa duniani Mwana wa Adamu anayo mamlaka ya kusamehe dhambi. Lakini nitawezaje kulithibitisha hili kwenu? Pengine mnafikiri ilikuwa rahisi kwangu kumwambia mtu huyu aliyepooza, ‘Dhambi zako zimesamehewa.’ Kwa sababu hilo haliwezi kuthibitishwa kwamba hakika limetokea. Lakini vipi nikimwambia, mtu huyu, beba machela yako na utembee? Hapo ndipo mtakapoweza kuona kama kweli ninayo mamlaka hayo ama sina.” Kwa hiyo Yesu akamwambia mtu yule aliyepooza, “Nitalithibitishaje hili kwako? Ninakwambia hivi, Inuka! Beba machela yako uende nyumbani!”
25 Yule mtu akasimama saa ile ile mbele ya kila mtu. Akaubeba machela yake na kwenda nyumbani kwake, akimsifu Mungu. 26 Kila mtu alishangaa na kuanza kumsifu Mungu. Wakajawa na hofu kuu baada ya kuiona nguvu ya Mungu. Wakasema, “Leo tumeona mambo ya kushangaza!”
Lawi (Mathayo) Amfuata Yesu
(Mt 9:9-13; Mk 2:13-17)
27 Baada ya hayo Yesu alitoka nje akamwona mtoza ushuru amekaa sehemu yake ya kukusanyia ushuru. Jina lake aliitwa Lawi. Yesu akamwambia, “Nifuate!” 28 Lawi akasimama, akaacha kila kitu na kumfuata Yesu.
29 Lawi akaandaa chakula cha usiku nyumbani kwake kwa kumheshimu Yesu. Mezani walikuwepo watoza ushuru wengi na baadhi ya watu wengine. 30 Lakini Mafarisayo na wale wanaofundisha sheria kwa ajili ya Mafarisayo wakaanza kulalamika kwa wafuasi wa Yesu wakisema, “Kwa nini mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi wengine?”
31 Yesu akawajibu, “Wagonjwa ndiyo wanaohitaji daktari, si wenye afya njema. 32 Sikuja kuwaambia wenye haki wabadilike, bali wenye dhambi.”
Swali Kuhusu Kufunga
(Mt 9:14-17; Mk 2:18-22)
33 Baadhi ya watu wakamwambia Yesu, “Wafuasi wa Yohana hufunga na kuomba mara kwa mara, vivyo hivyo wafuasi wa Mafarisayo. Lakini wafuasi wako hula na kunywa kila wakati.”
34 Yesu akawaambia, “Kwenye harusi huwezi kuwaambia marafiki wa bwana harusi wafunge wakati bwana harusi bado yuko pamoja nao. 35 Lakini muda ukifika na bwana harusi akaondolewa kwao. Watakuwa na huzuni, na watafunga.”
36 Yesu akawaambia mfano huu: “Hakuna anayekata kiraka kwenye vazi jipya na kukishona kwenye vazi la zamani. Ataharibu vazi jipya, na kiraka kutoka vazi jipya hakitakuwa sawa na vazi la zamani. 37 Pia hakuna mtu anayeweka divai mpya[d] katika viriba vya zamani. Divai mpya itavipasua, divai itamwagika, na viriba vitaharibika. 38 Daima mnaweka divai mpya kwenye viriba vipya. 39 Hakuna mtu ambaye baada ya kunywa divai ya zamani hutaka divai mpya. Kwa sababu husema, ‘Divai ya zamani ni nzuri.’”
© 2017 Bible League International