Beginning
Yesu Aenda Kwenye Mji wa Kwao
(Mt 13:53-58; Lk 4:16-30)
6 Yesu akaondoka pale, na kwenda katika mji wa kwao; na wanafunzi wake wakamfuata. 2 Sabato ilipofika, alianza kufundisha katika sinagogi. Watu wengi walishangazwa walipomsikiliza. Wakasema, “Mtu huyu alipata wapi mambo haya? Alipata wapi hekima hii? Na anaifanyaje miujiza hii inayofanyika kwa mikono yake? 3 Je, yeye si yule seremala? Je, yeye si mwana wa Maria? Je, yeye si kaka yake Yakobo, Yusufu, Yuda, na Simoni? Je, dada zake hawaishi hapa katika mji wetu?” Kulikuwa na vikwazo vilivyowazuia wasimkubali.
4 Yesu akawaambia, “kila mtu humheshimu nabii isipokuwa watu wa mji wa kwao mwenyewe, jamaa zake mwenyewe na wale wa nyumbani mwake mwenyewe.” 5 Yesu hakuweza kufanya miujiza ya aina yoyote pale, isipokuwa aliweka mikono juu ya wagonjwa wachache na kuwaponya. 6 Naye akashangazwa na jinsi watu wa mji wa kwao mwenyewe walivyokosa kuwa na imani. Kisha Yesu alizunguka vijijini akiwafundisha watu.
Yesu Awatuma Kazi Mitume Wake
(Mt 10:1,5-15; Lk 9:1-6)
7 Akawaita kwake wanafunzi wake kumi na wawili, na akaanza kuwatuma wawili wawili. Akawapa uwezo wa kuwaweka huru watu kutoka pepo wachafu. 8 Akawapa amri kuwa wasichukue kitu chochote kwa ajili ya safari yao isipokuwa fimbo; hawakupaswa kuchukua mkate, mfuko, hata kubeba fedha kwenye mikanda yao. 9 Aliwaruhusu kuvaa makobazi lakini wasichukue kanzu ya pili. 10 Naye akawambia, “ikiwa mtu atawapa mahali pa kuishi mkae katika nyumba hiyo kwa muda wote mtakapokuwa katika mji ule msihamehame kutoka nyumba moja hadi nyingine. 11 Ikiwa hamtakaribishwa ama kusikilizwa katika mji wowote au mahali popote, kwa kuwaonya kunguteni mavumbi toka miguuni mwenu.”
12 Kwa hiyo mitume wakatoka na kuhubiri ili watu watubu. 13 Mitume wakafukuza mashetani wengi na kuwapaka mafuta ya mizeituni[a] wagonjwa wengi na kuwaponya.
Herode Adhani Yesu ndiye Yohana Mbatizaji
(Mt 14:1-12; Lk 9:7-9)
14 Mfalme Herode alisikia habari hii kwani umaarufu wa Yesu ulikuwa umeenea mahali pote. Watu wengine walisema, “Yohana Mbatizaji amefufuka kutoka wafu, ndiyo maana ana uwezo wa kufanya miujiza.”
15 Wengine wakasema, “Yeye ni Eliya.”
Wengine walisema, “Yeye ni nabii kama mmoja wa manabii wa zamani.”
16 Lakini Herode aliyasikia haya na kusema, “Yohana, yule mtu niliyemkata kichwa, amefufuka kutoka kifo.”
Yohana Mbatizaji Alivyouawa
17 Kwa kuwa Herode mwenyewe alikuwa ametoa amri ya kumkamata Yohana na kumweka gerezani. Alifanya hivi kwa sababu ya Herodia, mkewe Filipo kaka yake ambaye Herode alikuwa amemwoa. 18 Kwani Yohana alizidi kumwambia Herode, “Si halali kwako kisheria kumwoa mke wa kaka yako.” 19 Herodia alikuwa na kisa na Yohana. Hivyo alitaka auwawe, lakini hakuweza kumshawishi Herode kumuua Yohana. 20 Hii ni kwa sababu Herode alimhofu Yohana. Herode pia alifahamu ya kuwa Yohana alikuwa ni mtu mtakatifu na mwenye haki, hivyo akamlinda. Herode alimpomsikia Yohana, alisumbuka sana; lakini alifurahia kumsikiliza.
21 Lakini muda maalumu ukafika; katika siku ya kuzaliwa kwake. Herode aliandaa sherehe ya chakula cha jioni kwa maafisa mashuhuri wa baraza lake, maafisa wake wa kijeshi, na watu maarufu wa Galilaya. 22 Binti ya Herodia alipowasili ndani ya ukumbi alicheza na kumpendeza Herode na wageni aliowaalika katika sherehe hiyo.
Mfalme Herode akamwambia yule msichana, “Uniombe chochote unachotaka, nami nitakupa.” 23 Akamuahidi: “Nitakupa chochote utakachoniomba, hata nusu ya ufalme wangu!”
24 Naye akatoka na kumwambia mama yake, “Niombe kitu gani?”
Mama yake akasema, “Omba kichwa cha Yohana Mbatizaji.”
25 Yule msichana mara moja aliharakisha kuingia ndani kwa mfalme na kuomba: “Nataka unipe sasa hivi kichwa cha Yohana Mbatizaji katika sinia.”
26 Mfalme alisikitika sana. Lakini kwa sababu ya viapo vyake alivyovifanya mbele ya wageni wake chakulani hakutaka kumkatalia ombi lake. 27 Kwa hiyo mfalme mara moja akamtuma mwenye kutekeleza hukumu za kifo akiwa na amri ya kukileta kichwa cha Yohana. Kisha akaenda kukikata kichwa cha Yohana, 28 na kukileta katika sinia na kumpa yule msichana, na msichana akampa mama yake. 29 Wanafunzi wa Yohana waliposikia haya walikuja na kuchukua mwili na kuuweka ndani ya kaburi.
Yesu Awalisha Watu Zaidi ya 5,000
(Mt 14:13-21; Lk 9:10-17; Yh 6:1-14)
30 Mitume walikusanyika kumzunguka Yesu, na wakamweleza yote waliyofanya na kufundisha. 31 Kisha Yesu akawaambia, “Njooni mnifuate peke yenu hadi mahali patulivu na palipo mbali na watu wengine ili mpumzike kidogo”, kwani pale walikuwepo watu wengi wakija na kutoka, nao hawakuwa na nafasi ya kula.
32 Kwa hiyo wakaondoka na mtumbwi kuelekea mahali patulivu na mbali na watu wakiwa peke yao. 33 Lakini watu wengi waliwaona wakiondoka na waliwafahamu wao ni kina nani; kwa hiyo walikimbilia pale kwa njia ya nchi kavu kutoka vitongoji vyote vilivyolizunguka eneo hilo wakafika kabla ya Yesu na wanafunzi wake. 34 Alipotoka katika mashua, Yesu aliona kundi kubwa, na akawahurumia, kwa sababu walikuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji, Kwa hiyo akaanza kuwafundisha mambo mengi.
35 Kwa sasa ilikuwa imekwisha kuwa jioni sana. Kwa hiyo wanafunzi wake walimwijia na kusema, “Hapa ni mahali palipojitenga na sasa hivi saa zimeenda. 36 Uruhusu watu waende zao, ili kwamba waende kwenye mashamba na vijiji vinavyozunguka na waweze kujinunulia kitu cha kula.”
37 Lakini kwa kujibu aliwaambia, “Ninyi wenyewe wapeni kitu cha kula.”
Wao Wakamwambia, “Je, twende kununua mikate yenye thamani ya mshahara wa mtu mmoja[b] wa miezi minane na kuwapa wale?”
38 Yesu akawambia, “Ni mikate mingapi mliyonayo? Nendeni mkaone.”
Walienda kuhesabu, wakarudi kwa Yesu na kusema, “Tunayo mikate mitano na samaki wawili.”
39 Kisha akawaagiza wakae chini kila mmoja kwenye majani mabichi kwa vikundi. 40 Nao wakakaa kwa vikundi vya watu mia na mmoja na vya watu hamsini.
41 Akachukua ile mikate mitano na samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akashukuru na akaimega. Akawapa wanafunzi wake ili wawape watu. Pia aligawanya samaki wawili miongoni mwao wote.
42 Wakala na wote wakatosheka. 43 Wakachukua mabaki ya vipande vya mikate na samaki na kujaza vikapu kumi na viwili. 44 Na idadi ya wanaume waliokula ile mikate ilikuwa 5,000.
Yesu Atembea Juu ya Maji
(Mt 14:22-33; Yh 6:16-21)
45 Mara Yesu akawafanya wafuasi wake wapande kwenye mashua na wamtangulie kwenda Bethsaida upande wa pili wa ziwa, wakati yeye akiliacha lile kundi liondoke. 46 Baada ya Yesu kuwaaga wale watu, alienda kwenye vilima kuomba.
47 Ilipotimia jioni, mashua ilikuwa katikati ya ziwa, na Yesu alikuwa peke yake katika nchi kavu. 48 Naye akawaona wanafunzi wake wakihangaika kupiga makasia, kwani upepo uliwapinga. Kati ya saa tisa na saa kumi na mbili asubuhi Yesu aliwaendea akitembea juu ya ziwa. Yeye akiwa karibu kuwapita, 49 wanafunzi wake wakamwona akitembea juu ya ziwa,[c] na wakafikiri kuwa alikuwa ni mzimu, ndipo walipopiga kelele. 50 Kwa kuwa wote walimwona, na wakaogopa. Mara tu alizungumza nao na kuwaambia, “Jipeni moyo! Ni mimi. Usiogope.” 51 Kisha alipanda kwenye mtumbwi pamoja nao, na upepo ukatulia. Wakashangaa kabisa, 52 kwa kuwa walikuwa bado hawajauelewa ule muujiza wa mikate. Kwani fahamu zao zilikuwa zimezibwa.
Yesu Awaponya Watu Wengi Wagonjwa
(Mt 14:34-36)
53 Walipolivuka ziwa, walifika Genesareti na wakaifunga mashua. 54 Walipotoka katika mashua, watu wakamtambua Yesu, 55 Wakakimbia katika lile jimbo lote na kuanza kuwabeba wagonjwa katika machela na kuwapeleka pale waliposikia kuwa Yesu yupo. 56 Na kila alipoenda vijijini, mijini na mashambani, waliwaweka wagonjwa kwenye masoko, na wakamsihi awaache waguse pindo la koti lake. Na wote walioligusa walipona.
Sheria ya Mungu na Desturi za Kibinadamu
(Mt 15:1-20)
7 Mafarisayo na baadhi ya walimu wa Sheria waliokuja kutoka Yerusalemu walikusanyika mbele zake. 2 Hao wakawaona baadhi ya wanafunzi wake wakila chakula chao kwa mikono michafu (yaani bila kuosha mikono yao). 3 Kwani Mafarisayo na Wayahudi wengineo wote hawawezi kula isipokuwa wameosha mikono yao kwa njia maalumu, kulingana na desturi ya wazee. 4 Na wanaporudi kutoka sokoni, hawali chakula kwanza mpaka wamenawa. Na zipo desturi nyingi wanazozishika, kama vile kuosha vikombe, magudulia na mitungi ya shaba.[d]
5 Kwa hiyo Mafarisayo na walimu wa Sheria wakamwuliza Yesu, “Kwa nini wanafunzi wako hawafuati desturi za wazee, badala yake wanakula chakula chao kwa mikono isiyo safi?”
6 Yesu akawaambia, “Isaya alikuwa sahihi alipotoa unabii juu yenu enyi wanafiki, kama ilivyoandikwa:
‘Watu hawa huniheshimu kwa midomo yao,
lakini mioyo yao iko mbali nami.
7 Ibada wanayonitolea haifai,
kwa sababu wanawafundisha watu amri
zilizotungwa na wanadamu kana kwamba ndizo itikadi zao.’(A)
8 Mmezipuuza amri za Mungu, na mnashikilia desturi za binadamu.”
9 Yesu akawaambia, “Ninyi ni wazuri katika kuzikataa amri za Mungu ili kuanzisha desturi yenu. 10 Kwa mfano Musa alisema, ‘Mheshimu baba yako na mama yako,’(B) na yule mtu atakayesema maneno mabaya juu ya ‘mama au baba yake itampasa auwawe.’(C) 11 Lakini ikiwa mtu atamwambia baba au mama yake, ‘Nilikuwa na kitu ambacho ningekupa kikusaidie, lakini nimeahidi kukitoa wakfu kwa Mungu, nacho sasa ni kurbani.[e]’ 12 Kisha, anasema, hivyo hawezi kufanya kitu chochote kwa ajili ya kumsaidia baba au mama yake. 13 Kwa hiyo unalifanya neno la Mungu kuwa batili kwa desturi mlizozirithishana. Na mnafanya mambo mengi mengine yanayofanana na hayo.”
14 Yesu akaliita lile kundi kwake na kuwaambia, “Kila mmoja anisikilize na kunielewa. 15 Hakuna kitu kilicho nje ya mtu kinachoweza kumchafua kwa kumwingia. Lakini vitu vinavyotoka ndani ya mtu ndivyo vinavyomchafua.” 16 [f]
17 Na alipoliacha lile kundi na kuingia ndani ya nyumba, wanafunzi wake wakamwuliza juu ya fumbo lile. 18 Na akawaambia, “Hata nanyi hamuelewi pia? Je, hamuelewi ya kuwa hakuna kinachomwingia mtu kutoka nje kinachoweza kumchafua mtu? 19 Kwa sababu hakiingii ndani ya moyo wake bali kinaenda tumboni mwake na kasha kinatoka na kwenda chooni.” Kwa kuyasema hayo alivifanya vyakula vyote kuwa safi.
20 Na Yesu akasema, “Ni kile kinachotoka ndani ya mtu ndicho kinachomchafua. 21 Kwani mambo hayo yote mabaya hutoka ndani ya moyo wa mwanadamu; yaani mawazo mabaya na uasherati, wizi, mauaji, 22 zinaa, ulafi, kufanya mabaya kwa watu, udanganyifu, kufanya uhuni, wivu, kutukana, kujivuna, na ujinga. 23 Mambo haya yote yanatoka ndani ya mtu nayo ndiyo yanayomfanya asikubalike kwa Mungu.”
Yesu Amsaidia Mwanamke Asiye Myahudi
(Mt 15:21-28)
24 Yesu akaondoka mahali pale na kuenda katika eneo lililozunguka Tiro. Aliingia katika nyumba na hakutaka mu yeyote ajue hilo, lakini hakuweza kufanya siri kuwepo kwake. 25 Mwanamke mmoja ambaye binti yake alikuwa na pepo mchafu mara moja akasikia juu ya Yesu hivyo alimwijia na kuanguka chini yake. 26 Mwanamke huyo alikuwa ni Mgiriki na siyo Myahudi, na alikuwa amezaliwa Foeniki ya Shamu. Yeye alimsihi amfukuze pepo yule kutoka kwa binti yake.
27 Yesu akamwambia, “Kwanza waache watoto watosheke, kwani sio haki kuwanyanganya watoto mkate wao na kuwapa mbwa.”
28 Lakini yeye akajibu, “Bwana hata mbwa walio chini ya meza wanakula mabaki ya chakula cha watoto.”
29 Kisha Yesu akamwambia, “kwa majibu haya unaweza kwenda nyumbani kwa amani: pepo mbaya amekwisha mtoka binti yako.”
30 Kwa hiyo akaenda nyumbani na akamkuta amelala akipumzika kitandani, na yule pepo tayari amekwisha mtoka.
Yesu Amponya Asiyesikia
31 Yesu akarudi kutoka katika eneo kuzunguka jiji la Tiro na akapita katika jiji la Sidoni hadi Ziwa Galilaya akipita katika jimbo la Dekapoli. 32 Pale watu wengine wakamletea mtu asiyeweza kusikia na tena aliyesema kwa shida. Nao wakamwomba Yesu amwekee mikono yake na kumponya.
33 Yesu akamchukua pembeni, kutoka katika kundi, na akaweka vidole vyake ndani ya masikio yake. Kisha Yesu akatema mate na kuugusa ulimi wa yule mtu. 34 Akaangalia juu mbinguni, akapumua na kumwambia “Efatha” yaani, “Funguka!” 35 Mara masikio ya mtu yule yakafunguka, na ulimi wake ukawa huru, na akaanza kuzungumza, vizuri.
36 Lakini kadiri jinsi alivyowaamuru wasimwambie mtu ndivyo walivyozidi kueneza habari hiyo. 37 Na watu wakashangazwa kabisa na kusema, “Yesu amefanya kila kitu vyema. Kwani amewafanya wale wasiosikia kusikia na wasiosema kusema.”
© 2017 Bible League International