Beginning
Simulizi Kuhusu Mkulima Aliyepanda Mbegu
(Mk 4:1-9; Lk 8:4-8)
13 Siku hiyo hiyo Yesu alitoka nje ya nyumba na kukaa kando ya ziwa. 2 Kundi kubwa wakakusanyika kumzunguka. Hivyo akapanda mtumbwini na kuketi. Watu wote wakabaki ufukweni. 3 Kisha Yesu akatumia simulizi kuwafundisha mambo mengi. Akawaambia simulizi hii:
“Mkulima alitoka kwenda kupanda mbegu. 4 Alipokuwa anatawanya mbegu, baadhi ziliangukia njiani. Ndege wakaja na kuzila zote. 5 Mbegu zingine ziliangukia kwenye ardhi yenye mawe, ambako hakukuwa na udongo wa kutosha. Zikakua haraka pale, kwa sababu udongo haukuwa na kina. 6 Lakini jua lilipowaka, likaichoma mimea. Mimea ikafa kwa sababu haikuwa na mizizi mirefu. 7 Baadhi ya mbegu ziliangukia katikati ya miiba. Miiba ikakua na kusababisha mimea mizuri kuacha kukua. 8 Lakini baadhi ya mbegu ziliangukia kwenye udongo wenye rutuba. Hapo zikakua na kuzaa nafaka. Baadhi ya mimea ikazaa nafaka mara mia zaidi, baadhi mara sitini na baadhi mara thelathini zaidi. 9 Ninyi watu mnaoweza kunisikia, nisikilizeni!”
Kwa nini Yesu Alitumia Simulizi Kufundisha
(Mk 4:10-12; Lk 8:9-10)
10 Wafuasi wake wakamwendea Yesu na kumuuliza, “Kwa nini unatumia simulizi hizi kuwafundisha watu?”
11 Yesu akawajibu, “Mungu amewapa ninyi ujuzi wa kuelewa siri za ufalme wa Mungu, lakini hajawapa watu hawa wengine ujuzi huu. 12 Kisha akawaambia, ‘Zingatieni kwa makini kile mnachokisikia. Kwani jinsi mnavyosikiliza kwa makini, ndivyo mtakavyoelewa na kuzidi kuelewa. Kwa kuwa kila aliye na uelewa kidogo ataongezewa zaidi. Lakini wale wasiosikiliza kwa makini watapoteza hata ule uelewa mdogo walio nao.’ 13 Ndiyo sababu ninatumia simulizi hizi kuwafundisha watu: Wanaona, lakini hakika hawaoni. Wanasikia, lakini hakika hawasikii au kuelewa. 14 Hiyo inathibitisha alichosema nabii Isaya kuhusu wao kuwa kweli:
‘Ninyi watu mtasikia na kusikia,
lakini hamtaelewa.
Mtatazama na kutazama,
lakini hakika hamtaona.
15 Ndiyo, akili za watu hawa sasa zimefungwa.
Wana masikio, lakini hawasikii vizuri.
Wana macho, lakini wameyafumba.
Iwapo akili zao zisingekuwa zimefungwa,
wangeona kwa macho yao;
wangesikia kwa masikio yao;
Iwapo wangeelewa kwa akili zao.
Kisha wangenigeukia na kuponywa.’(A)
16 Bahati gani mliyonayo ninyi. Mnaelewa mnachokiona kwa macho yenu. Na mnaelewa mnachosikia kwa masikio yenu. 17 Ninaweza kuwathibitishia, manabii na watakatifu wengi walitaka kuona mnayoyaona. Lakini hawakuyaona. Walitaka kusikia mnayosikia sasa. Lakini hawakuyasikia.
Yesu Afafanua Simulizi Kuhusu Mbegu
(Mk 4:13-20; Lk 8:11-15)
18 Hivyo sikilizeni maana ya simulizi hiyo kuhusu mkulima:
19 Vipi kuhusu mbegu zilizoangukia njiani? Hizo zinafanana na watu wanaosikia mafundisho kuhusu ufalme wa Mungu lakini hawauelewi. Mwovu huja na kuyachukua yaliyopandwa katika mioyo yao.
20 Na vipi kuhusu mbegu zilizoangukia kwenye udongo wenye mawe? Hizo zinafanana na watu wanaosikia mafundisho haraka na kwa furaha huyapokea. 21 Lakini hawaruhusu mafundisho kutawala maisha yao. Huyatunza kwa muda mfupi. Mara tatizo au mateso yanapokuja kwa sababu ya mafundisho waliyoyapokea, wanaacha kuyafuata.
22 Na vipi kuhusu mbegu zilizoanguka katikati ya miiba? Hizo zinafanana na watu wanaosikia mafundisho lakini huyaruhusu mahangaiko ya maisha na kutaka utajiri, hufanya mafundisho yasikue. Hivyo mafundisho hayazai mazao mazuri katika maisha yao.
23 Lakini vipi kuhusu mbegu zilizoanguka kwenye udongo wenye rutuba? Hizo ni sawa na watu wanaosikia mafundisho na kuyaelewa. Hukua na kuzaa mazao mazuri, wakati mwingine mara mia, wakati mwingine mara sitini, na wakati mwingine mara thelathini zaidi.”
Simulizi Kuhusu Ngano na Magugu
24 Kisha Yesu akatumia simulizi nyingine kuwafundisha. Yesu akasema, “Ufalme wa Mungu unafanana na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake. 25 Usiku ule, kila mtu alipokuwa amelala, adui wa yule mtu akaja na kupanda magugu katikati ya ngano kisha akaondoka. 26 Baadaye, ngano ikakua na vichwa vya nafaka vikaota juu ya mimea. Kisha mtumishi akayaona magugu. 27 Watumwa wa mwenye shamba wakaja na akasema, ‘Bwana ulipanda mimea mizuri kwenye shamba lako. Magugu yametoka wapi?’
28 Yule mtu akajibu, ‘Adui alipanda magugu.’
Wale watumwa wakauliza, ‘Je, unataka twende na kung'oa magugu?’
29 Akajibu, ‘Hapana, kwa sababu mtakapokuwa mnang'oa magugu, mtaweza pia kung'oa ngano. 30 Yaacheni magugu na ngano vikue pamoja mpaka wakati wa mavuno. Wakati wa mavuno nitawaambia wafanyakazi hivi: Kwanza, yakusanyeni magugu na kuyafunga pamoja ili myachome. Kisha kusanyeni ngano na kuileta ghalani mwangu.’”
Simulizi Nyingine ya Ufalme
(Mk 4:30-34; Lk 13:18-21)
31 Kisha Yesu akawaambia watu simulizi nyingine: “Ufalme wa Mungu unafanana na mbegu ya mharadali ambayo mtu alipanda katika shamba lake. 32 Ni mbegu ndogo sana kuliko mbegu zote. Lakini unapokua, ni kubwa kuliko mimea yote ya bustanini. Unakuwa mti mkubwa unaotosha ndege kuja na kutengeneza viota kwenye matawi yake.”
33 Kisha Yesu akawaambia simulizi nyingine: “Ufalme wa Mungu unafanana na chachu ambayo mwanamke huichanganya katika bakuli kubwa la unga ili atengeneze mkate. Chachu hufanya kinyunya chote kiumuke.”
34 Yesu alitumia simulizi akasema mambo yote haya kwa watu. Daima alitumia simulizi kuwafundisha. 35 Hii ilikuwa kuweka wazi maana halisi kama manabii walivyosema:
“Nitazungumza kwa kutumia simulizi;
Nitayasema mambo ambayo yamekuwa siri
tangu ulimwengu ulipoumbwa.”(B)
Yesu Afafanua Simulizi Kuhusu Magugu
36 Kisha Yesu akawaacha watu na kuingia katika nyumba. Wafuasi wake wakamwendea na akasema, “Tufafanulie maana ya simulizi kuhusu magugu ndani ya shamba.”
37 Akajibu, “Mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba ni Mwana wa Adamu. 38 Shamba ni ulimwengu. Mbegu nzuri ni watoto katika ufalme wa Mungu. Magugu ni watu wa Yule Mwovu. 39 Na adui aliyepanda mbegu mbaya ni ibilisi. Mwisho wa nyakati ndiyo wakati wa mavuno. Wafanyakazi wanaokusanya ni malaika wa Mungu.
40 Magugu hung'olewa na kuchomwa motoni. Itakuwa vivyo hivyo nyakati za mwisho. 41 Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watawatafuta watu wanaosababisha dhambi na wale wote watendao maovu. Malaika watawatoa watu hao katika ufalme wa Mungu. 42 Watawatupia katika tanuru la moto. Huko watu watakuwa wakilia na kusaga meno kwa maumivu. 43 Kisha wenye haki watang'aa kama jua. Watakuwa katika ufalme wa baba yao. Ninyi watu, mlio na masikio, sikilizeni!
Simulizi Kuhusu Hazina na Lulu
44 Ufalme wa Mungu unafanana na hazina iliyofichwa shambani. Siku moja mtu alipoiona aliificha tena; na kwa sababu alikuwa na furaha sana alikwenda kuuza kila kitu alichonacho na kulinunua shamba.
45 Pia, ufalme wa Mungu unafanana na mchuuzi anayetafuta lulu safi. 46 Siku moja alipoipata, alikwenda na akauza kila kitu alichokuwa nacho ili kuinunua.
Simulizi Kuhusu Wavu wa Kuvulia Samaki
47 Pia, ufalme wa Mungu unafanana na nyavu kubwa iliyowekwa katika ziwa. Nyavu ile ikavua aina nyingi tofauti ya samaki. 48 Ikajaa, hivyo wavuvi wakaivuta mpaka pwani. Wakakaa chini na kutoa samaki wote wazuri na kuwaweka kwenye kikapu. Kisha wakawatupa samaki wabaya. 49 Itakuwa hivyo wakati wa mwisho. Malaika watakuja na kuwatenganisha waovu na watakatifu. 50 Watawatupa waovu katika tanuru la moto. Huko watu watalia na kusaga meno yao kwa sababu ya maumivu.”
51 Kisha Yesu akawauliza wafuasi wake, “Mnaelewa mambo yote haya?”
Wakasema, “Ndiyo, tunaelewa.”
52 Kisha Yesu akawaambia wafuasi wake, “Hivyo kila mwalimu wa sheria aliyejifunza kuhusu ufalme wa Mungu ana baadhi ya vitu vizuri vya kufundisha. Ni kama mmiliki wa nyumba, aliye na vitu vipya na vya zamani nyumbani mwake. Na huvitoa nje vipya na vya zamani.”
Yesu Aenda Kwenye Mji wa Kwao
(Mk 6:1-6; Lk 4:16-30)
53 Yesu alipomaliza kufundisha kwa simulizi hizi, aliondoka pale. 54 Alikwenda katika mji wa kwao. Aliwafundisha watu katika sinagogi lao, nao walishangaa. Walisema, “Mtu huyu alipata wapi hekima na nguvu hii ya kutenda miujiza? 55 Je, yeye si mwana wa seremala tunayemfahamu? Je, jina la mamaye si Mariamu na wadogo zake ni Yakobo, Yusufu, Simoni na Yuda? 56 Na dada zake bado wanaishi hapa katika mji huu? Anawezaje kutenda mambo haya?” 57 Hivyo wakawa na mashaka kumpokea.
Lakini Yesu akawaambia, “Watu kila mahali huwaheshimu manabii, lakini katika mji wake au katika nyumba yake nabii hapati heshima yoyote.” 58 Yesu hakufanya miujiza mingi huko, kwa sababu watu hawakumwamini.
Herode Adhani Yesu ndiye Yohana Mbatizaji
(Mk 6:14-29; Lk 9:7-9)
14 Katika wakati huo, Herode, mtawala wa Galilaya, alisikia ambacho watu walikuwa wanasema kuhusu Yesu. 2 Hivyo akawaambia watumishi wake, “Nadhani hakika mtu huyu ni Yohana Mbatizaji. Lazima amefufuka kutoka kwenye kifo, na ndiyo sababu anaweza kutenda miujiza hii.”
Kifo cha Yohana Mbatizaji
3 Kabla ya wakati huu, Herode alimkamata Yohana. Akamfunga kwa minyororo na kumweka gerezani. Alimkamata Yohana kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, kaka yake Herode. 4 Yohana alikuwa amemwambia, “Si sahihi kwako kumwoa Herodia.” 5 Herode alitaka kumwua, lakini aliwaogopa watu. Waliamini kuwa Yohana alikuwa nabii.
6 Siku ya kuzaliwa Herode, bintiye Herodia[a] alicheza mbele yake na kundi lake. Herode alifurahishwa naye sana. 7 Hivyo aliapa kuwa atampa kitu chochote atakachotaka. 8 Herodia alimshawishi binti yake kitu cha kuomba. Hivyo bintiye akamwambia Herode, “Nipe hapa kichwa cha Yohana Mbatizaji kwenye sahani kubwa.”
9 Mfalme Herode alihuzunika sana. Lakini alikuwa ameahidi kumpa binti kitu chochote alichotaka. Na watu waliokuwa wakila pamoja na Herode walikuwa wamesikia ahadi yake. Hivyo Herode aliamuru kitu ambacho alikuwa ameomba apatiwe. 10 Akawatuma wanaume gerezani, ambako walikikata kichwa cha Yohana. 11 Na watu wakakileta kichwa cha Yohana kwenye sahani kubwa na kumpa yule msichana. Kisha yeye akakipeleka kichwa kwa mama yake, Herodia. 12 Wafuasi wa Yohana wakaja na kuuchukua mwili wa Yohana na kuuzika. Kisha wakaenda na kumwambia Yesu kilichotokea.
Yesu Awalisha Watu Zaidi ya 5,000
(Mk 6:30-44; Lk 9:10-17; Yh 6:1-14)
13 Yesu aliposikia kilichotokea kwa Yohana, aliondoka kwa kutumia mtumbwi. Alikwenda peke yake mpaka mahali ambapo hakuna aliyekuwa akiishi. Lakini watu walisikia kuwa Yesu alikuwa ameondoka. Hivyo waliondoka katika miji na kumfuata. Walikwenda mahali alikokwenda kupitia nchi kavu. 14 Yesu alipotoka katika mtumbwi, aliwaona watu wengi. Akawahurumia, na kuwaponya waliokuwa wagonjwa.
15 Baadaye mchana huo, wafuasi walimwendea Yesu na kusema, “Hakuna anayeishi katika eneo hili. Na tayari muda umepita, hivyo waage watu ili waende katika miji na kujinunulia chakula.”
16 Yesu akasema, “Watu hawahitaji kuondoka. Wapeni ninyi chakula wale.”
17 Wafuasi wakajibu, “Lakini tuna mikate mitano na samaki wawili tu.”
18 Yesu akasema, “Leteni kwangu mikate na samaki.” 19 Kisha akawaambia watu waketi chini kwenye nyasi. Akaichukua mikate mitano na samaki wawili. Akatazama mbinguni na akamshukuru Mungu kwa ajili ya chakula. Kisha akaivunja mikate katika vipande, akawapa wafuasi wake nao wakawapa watu chakula. 20 Kila mmoja alikula mpaka akashiba. Walipomaliza kula, wafuasi walijaza vikapu kumi na mbili vya vipande vilivyosalia. 21 Walikuwepo wanaume 5,000, pamoja na wanawake na watoto waliokula.
Yesu Atembea Juu ya Maji
(Mk 6:45-52; Yh 6:16-21)
22 Mara baada ya hili Yesu akawaambia wafuasi wake wapande kwenye mtumbwi. Akawaambia waende upande mwingine wa ziwa. Aliwaambia angekuja baadaye, alikaa pale ili kuwaaga watu. 23 Baada ya Yesu kuwaaga watu, alikwenda kwenye vilima peke yake kuomba. Ikawa jioni na alikuwa pale peke yake. 24 Wakati huu mtumbwi ilikuwa mbali kutoka pwani. Kwa kuwa upepo ulikuwa unavuma kinyume na mtumbwi, mtumbwi ulikuwa unapata msukosuko kwa sababu ya mawimbi.
25 Kati ya saa tisa na saa kumi na mbili asubuhi, wafuasi wa Yesu walikuwa bado ndani ya mtumbwi. Yesu akaenda kwao akitembea juu ya maji. 26 Iliwatisha walipomwona anatembea juu ya maji. Wakapiga kelele kwa woga “Ni mzuka!”
27 Lakini haraka Yesu akawaambia, “Msihofu! Ni mimi! Msiogope.”
28 Petro akasema, “Bwana, ikiwa hakika ni wewe, niambie nije kwako juu ya maji.”
29 Yesu akasema, “Njoo, Petro.”
Kisha Petro akauacha mtumbwi na kutembea juu ya maji kumwelekea Yesu. 30 Lakini Petro alipokuwa anatembea juu ya maji, aliyaona mawimbi na upepo. Aliogopa na kuanza kuzama katika maji. Akapiga kelele, “Bwana, niokoe!”
31 Haraka Yesu akamshika Petro kwa mkono wake. Akasema, “Imani yako ni ndogo. Kwa nini ulisita?”
32 Baada ya Petro na Yesu kuingia kwenye mtumbwi, upepo ukakoma. 33 Kisha wafuasi wakamwabudu Yesu na kusema, “Hakika wewe ni Mwana wa Mungu.”
Yesu Awaponya Watu Wengi Wagonjwa
(Mk 6:53-56)
34 Baada ya kuvuka ziwa, wakafika pwani katika eneo la Genesareti. 35 Baadhi ya watu pale wakamwona Yesu na wakamtambua kuwa ni nani. Hivyo wakatuma ujumbe kwa watu wengine katika eneo lote kuwa Yesu amekuja. Watu wakawaleta wagonjwa wao wote kwake. 36 Walimsihi Yesu awaruhusu waguse tu upindo wa vazi lake ili waponywe. Na wagonjwa wote waliogusa vazi lake waliponywa.
© 2017 Bible League International