Print Page Options
Previous Prev Day Next DayNext

Beginning

Read the Bible from start to finish, from Genesis to Revelation.
Duration: 365 days
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)
Version
Mathayo 9-10

Yesu Amponya Aliyepooza

(Mk 2:1-12; Lk 5:17-26)

Yesu akapanda katika mashua na akasafiri kwa kukatisha ziwa kurudi kwenye mji wake. Baadhi ya watu wakamletea mtu aliyepooza akiwa amelala kwenye machela. Yesu alipoona imani waliyokuwa nayo, alimwambia yule mtu aliyepooza, “Changamka mtoto wangu! Dhambi zako zimesamehewa.”

Baadhi ya walimu wa sheria walisikia alichosema Yesu. Wakaambizana wao kwa wao, “Si anamtukana Mungu mtu huyu akasema hivyo!”

Yesu alipotambua walichokuwa wanafikiri, akasema, “Kwa nini mna mawazo maovu kama hayo mioyoni mwenu? Wakati akiwa duniani Mwana wa Adamu anayo mamlaka ya kusamehe dhambi. Lakini nitawezaje kulithibitisha hili kwenu? Pengine mnafikiri ilikuwa rahisi kwangu kumwambia mtu huyu aliyepooza, ‘Dhambi zako zimesamehewa.’ Kwa sababu hilo haliwezi kuthibitishwa kwamba hakika limetokea. Lakini vipi nikimwambia mtu huyu, ‘Simama! Beba kitanda chako na utembee’? Hapo ndipo mtakapoweza kuona kama kweli ninayo mamlaka hayo ama sina.” Kwa hiyo Yesu akamwambia mtu yule aliyepooza, “Nitalithibitishaje hili kwako? Ninakwambia hivi, ‘Inuka! Beba kitanda chako uende nyumbani!’”

Mtu yule akasimama na kwenda nyumbani. Watu walipoliona tukio hili wakashangaa. Wakamsifu Mungu kwa kuwapa watu mamlaka hii.

Mathayo Amfuata Yesu

(Mk 2:13-17; Lk 5:27-32)

Yesu alipokuwa anaondoka, alimwona mtu aliyeitwa Mathayo amekaa mahali pa kukusanyia ushuru. Yesu akamwambia, “Nifuate.” Hivyo Mathayo akasimama na kumfuata Yesu.

10 Baadaye Yesu alikula chakula nyumbani kwa Mathayo. Watoza ushuru wengi na watu wenye sifa mbaya walikuja na kula chakula pamoja na Yesu pamoja na wafuasi wake. 11 Mafarisayo walipoona kuwa Yesu anakula pamoja na watu hao, wakawauliza wanafunzi wake, “Kwa nini mwalimu wenu anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi wengine?”

12 Yesu alipowasikia wakisema hili, akawaambia, “Wagonjwa ndiyo wanaohitaji daktari si wenye afya. 13 Nendeni mkajifunze andiko hili linamaanisha nini: ‘Sihitaji dhabihu ya mnyama; Ninataka ninyi mwoneshe wema kwa watu.’(A) Sikuja kuwaalika wema kujiunga nami, bali wenye dhambi.”

Swali Kuhusu Kufunga

(Mk 2:18-22; Lk 5:33-39)

14 Kisha wafuasi wa Yohana wakamjia Yesu na kusema, “Sisi na Mafarisayo tunafunga mara kwa mara, lakini wafuasi wako hawafungi. Kwa nini?”

15 Yesu akajibu, “Kwenye harusi marafiki wa bwana harusi hawana huzuni anapokuwa pamoja nao, hivyo hawawezi kufunga. Lakini wakati unakuja ambao bwana harusi ataondolewa kwao. Ndipo watakuwa na huzuni kisha watafunga.

16 Mtu anaposhona kiraka kwenye vazi la zamani, atatumia kiraka chakavu. Akitumia kiraka kipya vazi lake litachanika kwa sababu ya kusinyaa kwa kiraka hicho kipya. Kisha tundu litakuwa baya zaidi. 17 Pia, watu hawawaweki divai mpya kwenye viriba[a] vya zamani. Wakifanya hivyo viriba vitapasuka, na divai itamwagika na viriba vitaharibika. Daima watu huweka divai mpya katika viriba vipya, ambavyo haviwezi kupasuka, na divai huwa salama.”

Yesu Anampa Uhai Msichana Aliyekufa na Kumponya Mwanamke Mgonjwa

(Mk 5:21-43; Lk 8:40-56)

18 Yesu alipokuwa bado anaongea, kiongozi wa sinagogi akamwendea. Kiongozi akainama chini mbele yake na akasema, “Binti yangu amekufa sasa hivi. Lakini ikiwa utakuja na kumgusa kwa mkono wako, atafufuka.”

19 Hivyo Yesu na wafuasi wake wakaenda na mtu huyo.

20 Wakiwa njiani, alikuwepo mwanamke aliyekuwa akitokwa damu kwa miaka kumi na mbili. Alimwendea Yesu kwa nyuma na akagusa sehemu ya chini ya vazi lake. 21 Aliwaza, “Ikiwa nitagusa tu joho lake, nitapona.”

22 Yesu aligeuka na kumwona mwanamke. Akasema, “Uwe na furaha, mwanamke. Imani yako imekuponya.” Kisha yule mwanamke akapona saa ile ile.

23 Yesu aliendelea kwenda na kiongozi wa Kiyahudi na kuingia nyumbani kwake. Aliwaona watu wapigao muziki kwa ajili ya mazishi pale. Na aliliona kundi la watu waliohuzunika sana. 24 Yesu akasema, “Ondokeni. Msichana hajafa. Amelala tu.” Lakini watu wakamcheka. 25 Baada ya watu kutolewa nje ya nyumba, Yesu aliingia kwenye chumba cha msichana. Aliushika mkono wa msichana na msichana akasimama. 26 Habari kuhusu jambo hili ilienea kila mahali katika eneo lile.

Yesu Awaponya Watu Watatu

27 Yesu alipokuwa anaondoka kutoka pale, wasiyeona wawili walimfuata. Walisema kwa sauti, “Mwana wa Daudi, uwe mwema kwetu.”

28 Baada ya Yesu kuingia ndani, wasiyeona wakamwendea. Akawauliza, “Mnaamini kuwa ninaweza kuwafanya muone?” Wakajibu, “Ndiyo, Bwana, tunaamini.”

29 Kisha Yesu akayagusa macho yao na akasema, “Kwa kuwa mnaamini kuwa ninaweza kuwafanya muone, hivyo itatokea.” 30 Ndipo wakaweza kuona. Yesu akawaonya kwa nguvu. Akasema, “Msimwambie yeyote kuhusu hili.” 31 Lakini waliondoka na kutawanya habari kuhusu Yesu kila mahali katika eneo lile.

32 Watu hawa wawili walipokuwa wanaondoka, baadhi ya watu walimleta mtu mwingine kwa Yesu. Mtu huyu alikuwa haongei kwa sababu alikuwa na pepo ndani yake. 33 Yesu akamtoa nje pepo na mtu yule aliweza kuongea. Watu walishangaa na akasema, “Hakuna mtu yeyote aliyewahi kuona kitu kama hiki katika Israeli.”

34 Lakini Mafarisayo walisema, “Mtawala wa mashetani ndiye anayempa nguvu ya kuyatoa mashetani.”

Mwombeni Mungu Atume Watenda Kazi Zaidi

35 Yesu alisafiri akipita katika miji yote na vijiji. Alifundisha katika masinagogi yao na kuwaeleza watu Habari Njema kuhusu ufalme wa Mungu. Aliponya kila aina ya magonjwa na udhaifu. 36 Yesu aliona watu wengi na kuwahurumia kwa sababu walikuwa wanakandamizwa na hawakuwa na tumaini; kama kondoo bila mchungaji wa kuwaongoza. 37 Yesu akawaambia wafuasi wake, “Kuna mavuno mengi ya watu ya kuleta. Lakini kuna wafanyakazi wachache wa kusaidia kuwavuna. 38 Mungu anamiliki mavuno. Mwombeni atume wafanyakazi wengi zaidi wa kusaidia kukusanya mavuno yake.”

Yesu Awatuma Kazi Mitume Wake

(Mk 3:13-19; 6:7-13; Lk 6:12-16; 9:1-6)

10 Yesu aliwaita pamoja wafuasi wake kumi na mbili. Akawapa uwezo juu ya pepo wabaya ili waweze kuwafukuza na pia kuponya kila aina ya magonjwa na maradhi. Haya ni majina ya mitume kumi na wawili:

Simoni (ambaye pia aliitwa Petro),

Andrea, kaka yake Petro,

Yakobo, mwana wa Zebedayo,

Yohana, kaka yake Yakobo,

Filipo,

Bartholomayo,

Thomaso,

Mathayo, mtoza ushuru,

Yakobo, mwana wa Alfayo,

Thadayo,

Simoni Mzelote,

Yuda Iskariote (yule ambaye baadaye alimsaliti Yesu).

Yesu aliwatuma mitume hawa kumi na wawili pamoja na maelekezo haya: “Msiende kwa watu wasio Wayahudi. Na msiingie katika miji ambako Wasamaria wanaishi. Lakini nendeni kwa watu wa Israeli. Wako kama kondoo waliopotea. Mtakapokwenda, waambieni hivi: ‘Ufalme wa Mungu umekaribia.’ Waponyeni wagonjwa. Fufueni waliokufa. Waponyeni watu wenye magonjwa mabaya sana ya ngozi. Na toeni mashetani kwa watu. Ninawapa nguvu hii bure, hivyo wasaidieni wengine bure. Msibebe pesa pamoja nanyi; dhahabu au fedha au shaba nyekundu. 10 Msibebe mikoba. Chukueni nguo na viatu mlivyovaa tu. Na msichukue fimbo ya kutembelea. Mfanyakazi anastahili kupewa anachohitaji.

11 Mnapoingia katika mji, tafuteni kwa makini hadi mumpate mtu anayefaa na mkae katika nyumba yake mpaka mtakapoondoka mjini. 12 Mtakapoingia katika nyumba hiyo, semeni, ‘Amani iwe kwenu.’ 13 Ikiwa watu katika nyumba hiyo watawakaribisha, wanastahili amani yenu. Wapate amani mliyowatakia. Lakini ikiwa hawatawakaribisha, hawastahili amani yenu. Ichukueni amani mliyowatakia. 14 Na ikiwa watu katika nyumba au mji watakataa kuwapokea au kuwasikiliza, basi ondokeni mahali hapo na mkung'ute mavumbi kutoka katika miguu yenu. 15 Ninaweza kuwathibitishia kuwa siku ya hukumu itakuwa vibaya sana kwa mji huo kuliko watu wa Sodoma na Gomora.[b]

Yesu Aonya Kuhusu Matatizo

(Mk 13:9-13; Lk 21:12-17)

16 Sikilizeni! Ninawatuma, nanyi mtakuwa kama kondoo katikati ya mbwa mwitu. Hivyo muwe na akili kama nyoka. Lakini pia muwe kama njiwa na msimdhuru yeyote. 17 Muwe waangalifu! Wapo watu watakaowakamata na kuwapeleka ili kuwashitaki mbele ya mabaraza ya mijini. Watawachapa ndani ya masinagogi yao. 18 Mtasimamishwa mbele ya magavana na wafalme. Watu watawafanyia ninyi hivi kwa sababu mnanifuata. Mtakuwa mashahidi wangu mbele za wafalme na magavana hao na kwa watu wa mataifa mengine. 19 Mtakapokamatwa, msisumbuke kuhusu nini mtakachosema au namna gani mtakavyosema. Katika wakati huo mtapewa maneno ya kusema. 20 Si ninyi mtakaoongea; Roho wa Baba Mungu wenu atakuwa anaongea kupitia ninyi.

21 Ndugu watakuwa kinyume cha ndugu zao wenyewe na kuwapeleka kwenda kuuawa. Baba watawapeleka watoto wao wenyewe kuuawa. Watoto watapigana kinyume na wazazi wao na watawapeleka kuuawa. 22 Kila mtu atawachukia kwa sababu mnanifuata mimi. Lakini atakayekuwa mwaminifu mpaka mwisho ataokolewa. 23 Mnapotendewa vibaya katika mji mmoja, nendeni katika mji mwingine. Ninawaahidi kuwa hamtamaliza kwenda katika miji ya Israeli kabla Mwana wa Adamu hajarudi.

24 Wanafunzi si wazuri kuliko mwalimu wao. Watumwa si wazuri kuliko bwana wao. 25 Inatosha kwa wanafunzi kuwa kama walimu wao na watumwa kuwa kama bwana wao. Iwapo watu hao wananiita ‘mtawala wa pepo’, na mimi ni kiongozi wa familia, basi ni dhahiri kwa kiasi gani watawatukana ninyi, mlio familia yangu!

Mwogopeni Mungu, Siyo Watu

(Lk 12:2-7)

26 Hivyo msiwagope watu hao. Kila kitu kilichofichwa kitaoneshwa. Kila kilicho siri kitajulikana. 27 Ninayowaambia ninyi faraghani myaseme hadharani. Kila ninachowanong'oneza nawataka mkiseme kwa sauti kila mtu asikie.

28 Msiwaogope watu. Wanaweza kuua mwili, lakini hawawezi kuiua roho. Mnapaswa kumwogopa Mungu, anayeweza kuuharibu mwili na roho jehanamu. 29 Ndege wanapouzwa, ndege wawili wadogo hugharimu senti moja tu. Lakini hakuna hata mmoja wa ndege hao wadogo anaweza kufa bila Baba yenu kufahamu. 30 Mungu anafahamu idadi ya nywele katika vichwa vyenu. 31 Hivyo msiogope. Mna thamani kuliko kundi kubwa la ndege.

Msiionee Haya Imani Yenu

(Lk 12:8-9)

32 Iwapo mtawaambia watu wengine kuwa mnaniamini, nitamwambia Baba yangu aliye mbinguni kuwa ninyi ni wangu. 33 Lakini ikiwa mtasimama mbele ya wengine na kusema kuwa hamniamini, nitamwambia Baba yangu aliye mbinguni kuwa ninyi si wangu.

Kumfuata Yesu Kunaleta Matatizo

(Lk 12:51-53; 14:26-27)

34 Msidhani kuwa nilikuja duniani kuleta amani. Sikuja kuleta amani. Nilikuja kuleta vita. 35 Nimekuja ili hili litokee:

‘Mwana atamgeuka baba yake.
    Binti atamgeuka mama yake.
Binti mkwe atamgeuka mama mkwe wake.
36     Hata watu wa familia zenu watakuwa adui zenu.’(B)

37 Wale wanaowapenda baba zao au mama zao kuliko wanavyonipenda mimi hawana thamani kwangu. Na wale wanaowapenda wana wao au binti zao kuliko wanavyonipenda mimi hawastahili kuwa wafuasi wangu. 38 Wale ambao hawataupokea msalaba waliopewa wanaponifuata hawastahili kuwa wanafunzi wangu na kunifuata. 39 Wale wanaojaribu kuyatunza maisha waliyonayo, watayapoteza. Lakini wale wanaoyaacha maisha yao kwa ajili yangu watapata uzima halisi.

Mungu Atawabariki Wanaowakaribisha Ninyi

(Mk 9:41)

40 Yeyote anayewakubali ninyi ananikubali mimi. Na yeyote anayenikubali anamkubali yule aliyenituma. 41 Yeyote anayemkubali nabii kwa sababu ni nabii atapata ujira wa nabii. Na yeyote anayemkubali mwenye haki kwa sababu ni mwenye haki atapata ujira anaoupata mwenye haki. 42 Yeyote anayemsaidia mmoja wa wafuasi wangu hawa wanyenyekevu kwa sababu ni wafuasi wangu hakika atapata ujira, hata ikiwa wanawapa tu kikombe cha maji baridi.”

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi (TKU)

© 2017 Bible League International