Beginning
Mjane Aonesha Jinsi Ulivyo Utoaji wa Kweli
(Mk 12:41-44)
21 Yesu alitazama na kuwaona matajiri wakimtolea Mungu sadaka zao katika sanduku la sadaka ndani ya Hekalu. 2 Kisha akamwona mjane maskini akiweka sarafu mbili za shaba kwenye sanduku. 3 Akasema, “Mjane huyu maskini ametoa sarafu mbili tu. Lakini ukweli ni kuwa, ametoa zaidi ya hao matajiri wote. 4 Wale wanavyo vingi, na wametoa vile ambavyo hawavihitaji. Lakini mwanamke huyu ni maskini sana, lakini ametoa vyote alivyokuwa akitegemea ili aishi.”
Yesu Aonya Kuhusu Wakati Ujao
(Mt 24:1-14; Mk 13:1-13)
5 Baadhi ya watu walikuwa wanazungumza kuhusu uzuri wa Hekalu lililojengwa kwa mawe safi na kupambwa kutokana na matoleo mbalimbali ambayo watu humtolea Mungu ili kutimiza nadhili zao.
6 Lakini Yesu akasema, “Wakati utafika ambao yote mnayoyaona hapa yatateketezwa. Kila jiwe katika majengo haya litatupwa chini. Hakuna jiwe litakaloachwa juu ya jingine.”
7 Baadhi ya watu wakamwuliza Yesu, “Mwalimu, mambo hayo yatakuwa lini? Dalili ipi itatuonyesha kwamba ni wakati wa mambo haya kutokea?”
8 Yesu akasema, “Iweni waangalifu, msije mkarubuniwa. Watu wengi watakuja wakitumia jina langu, watasema, ‘Mimi ndiye Masihi,’[a] na ‘Wakati sahihi umefika!’ Lakini msiwafuate. 9 Mtakaposikia kuhusu vita na machafuko, msiogope. Mambo haya lazima yatokee kwanza. Lakini mwisho hautakuja haraka.”
10 Kisha Yesu akawaambia, “Mataifa yatapigana na mataifa mengine. Falme zitapigana na falme zingine. 11 Kutakuwa matetemeko makubwa, kutakuwa njaa na magonjwa ya kutisha sehemu nyingi. Mambo ya kutisha yatatokea, na mambo ya kushangaza yatatokea kutoka mbinguni ili kuwaonya watu.
12 Lakini kabla ya mambo haya yote kutokea, watu watawakamata ninyi na kuwatesa. Watawahukumu katika masinagogi yao na kuwafunga gerezani. Mtalazimishwa kusimama mbele ya wafalme na magavana. Watawatendea mambo haya yote kwa sababu ninyi ni wafuasi wangu. 13 Lakini hili litawapa ninyi fursa ya kuhubiri juu yangu. 14 Msihofu namna mtakavyojitetea, 15 Nitawapa hekima kusema mambo ambayo adui zenu watashindwa kuyajibu. 16 Hata wazazi wenu, ndugu zenu, jamaa, na marafiki watawageuka. Watawaua baadhi yenu. 17 Kila mtu atawachukia kwa sababu mnanifuata mimi. 18 Lakini hakuna hata unywele mmoja wa vichwa vyenu utakaopotea. 19 Mtayaokoa maisha yenu ikiwa mtaendelea kuwa imara katika imani mnapopita katika mambo haya yote.
Kuharibiwa Kwa Mji wa Yerusalemu
(Mt 24:15-21; Mk 13:14-19)
20 Mtakapoona majeshi yameuzunguka mji wa Yerusalemu, ndipo mtajua kuwa wakati wa kuharibiwa kwake umefika. 21 Watu walioko katika Uyahudi wakati huo wakimbilie milimani. Mtu yeyote atakaye kuwa Yerusalemu wakati huo aondoke haraka. Ikiwa utakuwa karibu na mji, usiingie mjini! 22 Manabii waliandika mambo mengi kuhusu wakati ambao Mungu atawaadhibu watu wake. Wakati ninaouzungumzia ni wakati ambao mambo haya yote lazima yatokee. 23 Wakati huu utakuwa mgumu kwa wanawake wenye mimba au wanaonyonyesha watoto wadogo, kwa sababu mambo mabaya yatakuja katika nchi hii. Mungu atawaadhibu watu wake kwa sababu wamemkasirisha. 24 Baadhi ya watu watauawa, wengine watafanywa watumwa na kuchukuliwa katika nchi mbalimbali. Mji mtakatifu wa Yerusalemu utatekwa na kuwekwa chini ya utawala wa wageni mpaka wakati ulioruhusiwa wao kufanya hivi utakapokwisha.
Msiogope
(Mt 24:29-31; Mk 13:24-27)
25 Mambo ya kushangaza yatatokea kwenye jua, mwezi na nyota na watu katika dunia yote wataogopa na kuchanganyikiwa kutokana na kelele za bahari na mawimbi yake. 26 Watazimia kwa hofu na kuogopa watakapoona mambo yanayoupata ulimwengu. Kila kitu katika anga kitabadilishwa. 27 Kisha watu watamwona Mwana wa Adamu akija katika wingu mwenye nguvu na utukufu mwingi. 28 Mambo haya yakianza kutokea, simameni imara na msiogope. Jueni kuwa wakati wa Mungu kuwaweka huru umekaribia!”
Maneno Yangu Yataishi Milele
(Mt 24:32-35; Mk 13:28-31)
29 Kisha Yesu akawaambia mfano huu: “Tazameni miti yote. Mtini ni mfano mzuri. 30 Unapochipua majani mnatambua kwamba majira ya joto yamekaribia. 31 Kwa namna hiyo hiyo, mtakapoona mambo haya yote yanatokea, mtajua kwamba ufalme wa Mungu umekaribia kuja.
32 Ninawahakikishia kwamba, wakati mambo haya yote yatakapotokea, baadhi ya watu wanaoishi sasa watakuwa hai bado. 33 Ulimwengu wote, dunia yote na anga vitapita, lakini maneno yangu yataishi milele.
Kuweni Tayari Wakati Wote
34 Iweni waangalifu, msiutumie muda wenu katika sherehe za ulevi na kuhangaikia maisha haya. Mkifanya hivyo, hamtaweza kufikiri vyema na mwisho unaweza kuja mkiwa hamjajiandaa. 35 Mwisho utakuja kwa kushitukiza kwa kila mtu duniani. 36 Hivyo, iweni tayari kila wakati. Ombeni ili muepuke mambo haya yote yatakayotokea na mweze kusimama kwa ujasiri mbele za Mwana wa Adamu.”
37 Wakati wa mchana Yesu aliwafundisha watu katika eneo la Hekalu. Usiku alitoka nje ya mji na kukaa usiku kucha kwenye kilima kinachoitwa Mlima wa Mizeituni. 38 Kila asubuhi watu wote waliamka mapema kwenda kumsikiliza Yesu katika Hekalu.
Mpango wa Kumwua Yesu
(Mt 26:1-5; Mk 14:1-2; Yh 11:47-53)
22 Ilikuwa karibu ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, inayoitwa Pasaka. 2 Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walitaka kumwua Yesu kwa siri kwa sababu waliogopa kile ambacho watu wangefanya.
Yuda Akubali Kuwasaidia Adui wa Yesu
(Mt 26:14-16; Mk 14:10-11)
3 Mmoja wa mitume kumi na wawili wa Yesu aliitwa Yuda Iskariote. Shetani alimwingia Yuda, 4 akaondoka, akaenda kuongea na viongozi wa makuhani na baadhi ya wakuu wa askari walinzi wa Hekalu. Aliongea nao kuhusu namna ya kumkabidhi Yesu kwao. 5 Makuhani walifurahia sana hili. Wakaahidi kumlipa Yuda pesa ikiwa angefanya hivi. 6 Akakubali, kisha alianza kusubiri muda mzuri wa kumkabidhi Yesu kwao. Alitaka kumkabidhi Yesu kwao wakati hakuna kundi la watu ambao wangeona.
Karamu ya Pasaka
(Mt 26:17-25; Mk 14:12-21; Yh 13:21-30)
7 Siku ya Mikate Isiyotiwa Chachu[b] ilifika. Hii ni siku ambayo Wayahudi daima walichinja kondoo kwa ajili ya Pasaka. 8 Yesu aliwaambia Petro na Yohana, “Nendeni mkaandae mlo wa Pasaka ili tule.”
9 Wakamwambia, “Unataka tukauandae wapi?”
Akawaambia, 10 “Mtakapokuwa mnaingia mjini, mtakutana na mtu amebeba mtungi wa maji. Mfuateni. Ataingia katika nyumba. 11 Mwambieni mmiliki wa nyumba, ‘Mwalimu anakuomba tafadhali utuoneshe chumba ambacho yeye na wafuasi wake wanaweza kulia mlo wa Pasaka.’ 12 Mmiliki atawaonesha chumba kikubwa ghorofani kilicho tayari kwa ajili yetu. Andaeni mlo humo.”
13 Hivyo Petro na Yohana wakaondoka. Kila kitu kilitokea kama Yesu alivyosema. Na hivyo wakauandaa mlo wa Pasaka.
Chakula cha Bwana
(Mt 26:26-30; Mk 14:22-26; 1 Kor 11:23-25)
14 Wakati ulifika kwa wao kula mlo wa Pasaka. Yesu na mitume walikuwa wamekaa pamoja kuzunguka meza ya chakula. 15 Yesu akawaambia, “Nilitaka sana kula mlo huu wa Pasaka pamoja nanyi kabla sijafa. 16 Sitakula mlo mwingine wa Pasaka mpaka itakapopewa maana yake kamili katika ufalme wa Mungu.”
17 Kisha Yesu akachukua kikombe kilichokuwa na divai. Akamshukuru Mungu, na akasema, “Chukueni kikombe hiki na kila mmoja anywe. 18 Sitakunywa divai tena mpaka Ufalme wa Mungu utakapokuja.”
19 Kisha akaichukua baadhi ya mkate na akamshukuru Mungu. Akaigawa vipande vipande, akawapa vipande mitume na kusema, “Mkate huu ni mwili wangu ninaoutoa kwa ajili yenu. Kuleni kwa kunikumbuka.” 20 Katika namna ile ile, baada ya kula chakula, Yesu akachukua kikombe chenye divai na akasema, “Divai hii inawakilisha Agano Jipya kutoka kwa Mungu kwa watu wake. Litaanza pale damu yangu itakapomwagika kwa ajili yenu.”[c]
Nani Atamsaliti Yesu?
21 Yesu akasema, “Lakini hapa mezani kuna mkono wa yule atakayenisaliti kwa adui zangu. 22 Mwana wa Adamu atakufa kama Mungu alivyoamua. Lakini ole wake mtu yule atakayemsaliti Mwana wa Adamu ili auawe.”
23 Ndipo mitume wakaulizana, “Ni nani miongoni mwetu atafanya hivyo?”
Iweni Kama Mtumishi
24 Baadaye, mitume wakaanza kubishana kuhusu nani miongoni mwao alikuwa mkuu. 25 Lakini Yesu akawaambia, “Wafalme wa mataifa wanawatawala watu kama watumwa wao, na wenye mamlaka juu ya wengine wanataka kuitwa, ‘Wafadhili Wakuu’. 26 Lakini ni lazima msiwe hivyo. Aliye na mamlaka zaidi miongoni mwenu lazima awe kama asiye na mamlaka. Anayeongoza anapaswa kuwa kama anayetumika. 27 Nani ni mkuu zaidi: Yule anayetumika au yule aliyekaa mezani na kuhudumiwa? Kila mtu hudhani ni yule aliyekaa mezani akihudumiwa, sawa? Lakini nimekuwa pamoja nanyi kama ninayetumika.
28 Na ninyi ndiyo mliobaki pamoja nami katika mahangaiko mengi. 29 Hivyo ninawapa mamlaka kutawala pamoja nami katika ufalme ambao Baba yangu amenipa. 30 Mtakula na kunywa mezani pangu katika ufalme huo. Mtakaa katika viti vya enzi na kuwahukumu makabila kumi na mbili ya Israeli.
Petro Atajaribiwa na Kushindwa
(Mt 26:31-35; Mk 14:27-31; Yh 13:36-38)
31 Shetani ameomba ili awapepete kwa nguvu kama mkulima anavyopepeta ngano kwenye ungo ili mwanguke. Simoni, Simoni,[d] 32 nimekuombea ili usipoteze imani yako! Wasaidie ndugu zako kuwa imara utakaponirudia.”
33 Lakini Petro akamwambia Yesu, “Bwana, niko tayari kufungwa gerezani pamoja nawe. Hata kufa pamoja nawe!”
34 Lakini Yesu akasema, “Petro, asubuhi kabla jogoo hajawika, utakuwa umenikana mara tatu.”
Iweni Tayari kwa Matatizo
35 Kisha Yesu akawaambia mitume, “Kumbukeni nilipowatuma bila pesa, mkoba, wala viatu. Je, mlipungukiwa chochote?”
Mitume wakajibu, “Hapana.”
36 Yesu akawaambia, “Lakini sasa kama una pesa au mkoba, uchukue pamoja nawe. Kama huna upanga, uza koti lako ukanunue. 37 Maandiko yanasema, ‘Alidhaniwa kuwa mhalifu.’(A) Maandiko haya lazima yatimizwe. Yaliyoandikwa kuhusu mimi yanatimilika sasa.”
38 Wafuasi wakasema, “Tazama Bwana, hapa kuna panga mbili.”
Yesu akawaambia, “Nyamazeni, acheni mazungumzo ya namna hiyo!”
Yesu Aomba Akiwa Peke Yake
(Mt 26:36-46; Mk 14:32-42)
39-40 Yesu akaondoka mjini akaenda Mlima wa Mizeituni. Wafuasi wake wakaenda pamoja naye. (Alikuwa akienda huko mara kwa mara.) Akawaambia wafuasi wake, “Ombeni ili mtiwe nguvu msije mkajaribiwa.”
41 Kisha Yesu akaenda kama hatua hamsini mbali nao. Akapiga magoti na akaomba akisema, 42 “Baba, ukiwa radhi, tafadhali usinifanye ninywe katika kikombe[e] hiki. Lakini fanya unalotaka wewe, siyo ninalotaka mimi.” 43 Kisha malaika kutoka mbinguni akaja akamtia nguvu. 44 Yesu aliomba kwa nguvu zaidi na kustahimili zaidi kama mpiganaji wa mieleka akiwa katika mapambano makali. Jasho kama matone ya damu likadondoka kutoka kwenye uso wake.[f] 45 Alipomaliza kuomba, alikwenda kwa wafuasi wake. Akawakuta wamelala, wamechoka kwa sababu ya huzuni. 46 Yesu akawaambia, “Kwa nini mnalala? Amkeni, ombeni mtiwe nguvu msije mkajaribiwa.”
Yesu Akamatwa
(Mt 26:47-56; Mk 14:43-50; Yh 18:3-11)
47 Yesu alipokuwa anaongea, kundi likaja. Lilikuwa linaongozwa na Yuda, mmoja wa mitume kumi na wawili. Akamwendea Yesu ili ambusu.
48 Lakini Yesu akamwambia, “Yuda unatumia busu la urafiki kumsaliti Mwana wa Adamu kwa adui zake?” 49 Wafuasi wa Yesu walikuwa wamesimama pale pia. Walipoona kilichokuwa kinatokea, wakamwambia Yesu, “Bwana, tutumie panga zetu?” 50 Na mmoja wao akautumia upanga wake. Akakata sikio la kulia la mtumishi wa kuhani mkuu.
51 Yesu akasema, “Acha!” Kisha akaligusa sikio la mtumishi na akamponya.
52 Yesu akaliambia lile kundi lililokuja kumkamata. Walikuwa viongozi wa makuhani, viongozi wa wazee wa Kiyahudi na askari walinzi wa Hekalu. Akawaambia, “Kwa nini mmekuja hapa mkiwa na mapanga na marungu? Mnadhani mimi ni mhalifu? 53 Nilikuwa pamoja nanyi kila siku katika eneo la Hekalu. Kwa nini hamkujaribu kunikamata pale? Lakini sasa ni wakati wenu, wakati ambao giza linatawala.”
Petro Amkana Yesu
(Mt 26:57-58,69-75; Mk 14:53-54,66-72; Yh 18:12-18,25-27)
54 Walimkamata Yesu na kumpeleka nyumbani kwa kuhani mkuu. Petro alimfuata Yesu lakini alikaa nyuma kwa mbali. 55 Baadhi ya watu walikoka moto katikati ya ua kisha wakaketi pamoja. Petro naye aliketi pamoja nao. 56 Kutokana na mwanga wa moto, mtumishi wa kike alimwona Petro amekaa pale. Akamtazama Petro usoni kwa makini. Kisha akasema, “Huyu pia alikuwa na yule mtu.”
57 Lakini Petro akasema si kweli. Akasema, “Mwanamke, simfahamu mtu huyo!” 58 Muda mfupi baadaye, mtu mwingine akamwona Petro na akasema, “Wewe pia ni mmoja wa lile kundi!”
Lakini Petro akasema, “Wewe, mimi si mmoja wao!”
59 Baada ya kama saa moja baadaye, mtu mwingine akasema, “Ni kweli, nina uhakika mtu huyu alikuwa pamoja naye, kwa sababu yeye pia anatoka Galilaya.”
60 Lakini Petro akasema, “Wewe, wala sijui unazungumza kuhusu nini!”
Alipokuwa bado anazungumza, jogoo aliwika. 61 Bwana aligeuka akamtazama Petro kwenye macho yake. Kisha Petro akakumbuka Bwana alivyokuwa amesema ya kwamba, “Kabla ya jogoo kuwika asubuhi, utakuwa umenikana mara tatu.” 62 Kisha Petro akatoka nje na kulia kwa uchungu.
Walinzi Wamdhalilisha Yesu
(Mt 26:67-68; Mk 14:65)
63 Walinzi waliokuwa wanamlinda Yesu walimfanyia mizaha na kumpiga. 64 Wakayafunika macho yake ili asiwaone. Kisha wakampiga na wakasema, “Tabiri, tuambie nani amekupiga!” 65 Walimtukana pia matusi ya kila aina.
Yesu Akiwa Mbele ya Viongozi wa Kidini
(Mt 26:59-66; Mk 14:55-64; Yh 18:19-24)
66 Alfajiri, viongozi wazee wa watu, viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walikusanyika. Walimpeleka Yesu kwenye baraza lao kuu. 67 Wakamwambia, “Tuambie ikiwa wewe ni Masihi.”
Yesu akawaambia, “Hamtaniamini ikiwa nitawaambia kuwa mimi ni Masihi. 68 Na ikiwa nitawauliza swali, hakika mtakataa kunijibu. 69 Lakini kuanzia sasa, Mwana wa Adamu atakaa upande wa kuume wa Mungu Mwenye Nguvu.”
70 Wote wakasema, “Kwa hiyo wewe ni Mwana wa Mungu?” Akawajibu, “Mnaweza kusema kuwa mimi ni Mwana wa Mungu.”
71 Wakasema, “Je, tunahitaji mashahidi wengine zaidi? Sote tumesikia alichosema yeye mwenyewe!”
© 2017 Bible League International