Beginning
Yesu Awatuma Kazi Mitume Wake 72
10 Baada ya hili, Bwana alichagua wafuasi sabini na wawili[a] zaidi. Aliwatuma watangulie katika kila mji na kila mahali alipokusudia kwenda wakiwa wawili wawili. 2 Aliwaambia, “Kuna mavuno mengi ya watu wa kuwaingiza katika Ufalme wa Mungu. Lakini watenda kazi wa kuwaingiza katika ufalme wa Mungu ni wachache. Mungu anamiliki mavuno. Mwombeni ili atume watenda kazi wengi ili wasaidie kuyaingiza mavuno yake.
3 Mnaweza kwenda sasa. Lakini sikilizeni! Ninawatuma na mtakuwa kama kondoo katikati ya mbwa mwitu. 4 Msibebe mfuko wowote, wala pesa au viatu. Msisimame kusalimiana na watu njiani. 5 Kabla ya kuingia katika nyumba, mseme, ‘Amani iwemo katika nyumba hii.’ 6 Ikiwa watu wanaoishi katika nyumba hiyo wanapenda amani, baraka yenu ya amani itakaa nao. Lakini kama siyo, baraka yenu ya amani itawarudia. 7 Kaeni katika nyumba inayopenda amani. Kuleni na kunywa chochote watakachowapa kwa maana mfanyakazi anastahili ujira. Msihame kutoka katika nyumba hiyo na kwenda kukaa katika nyumba nyingine.
8 Mkiingia katika mji wowote na watu wakawakaribisha, kuleni vyakula watakavyowapa. 9 Waponyeni wagonjwa wanaoishi katika mji huo, na waambieni Ufalme wa Mungu umewafikia![b]
10 Lakini mkiingia katika mji wowote na watu wasiwakaribishe, nendeni katika mitaa ya mji huo na mseme, 11 ‘Tunafuta mavumbi ya mji wenu yaliyogandamana katika miguu yetu! Lakini kumbukeni kwamba: Ufalme wa Mungu umewafikia!’ 12 Ninawaambia, siku ya hukumu itakuwa vibaya sana kwa watu wa mji huo kuliko watu wa Sodoma.
Maonyo Kwa Wanaomkataa Yesu
(Mt 11:20-24)
13 Ole wako, Korazini! Ole wako Bethsaida![c] Watu wenu wameniona nikifanya miujiza mingi ndani yenu, lakini hamkubadilika. Miujiza hiyo hiyo ingefanyika katika miji ya Tiro na Sidoni,[d] watu katika miji hiyo wangelikwisha badili mioyo na maisha yao siku nyingi. Wangelikwisha vaa nguo za magunia na kukaa kwenye majivu kuonesha kusikitika na kutubu dhambi zao. 14 Lakini itakuwa rahisi kwa miji ya Tiro na Sidoni siku ya hukumu kuliko ninyi. 15 Nawe Kapernaumu, Je! Utatukuzwa mpaka mbinguni? Hapana, utatupwa chini hadi mahali pa kifo.
16 Mtu yeyote akiwasikiliza ninyi wafuasi wangu, hakika ananisikiliza mimi. Lakini mtu yeyote akiwakataa ninyi, hakika ananikataa mimi. Na mtu yeyote akinikataa mimi anamkataa Yule aliyenituma.”
Shetani Aangushwa
17 Wale wafuasi sabini na wawili waliporudi kutoka katika safari yao, walikuwa na furaha sana. Walisema, “Bwana, hata pepo walitutii tulipotumia jina lako!”
18 Yesu akawaambia, “Nilimwona Shetani akianguka kama mwanga wa radi kutoka mbinguni! 19 Yeye ndiye adui, lakini tambueni kuwa nimewapa mamlaka zaidi yake. Nimewapa mamlaka ya kuponda nyoka na nge zake kwa miguu yenu. Hakuna kitakachowadhuru. 20 Ndiyo, hata pepo wanawatii. Na mnaweza kufurahi, lakini si kwa sababu mna mamlaka hii. Furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.”
Yesu Aomba Kwa Baba
(Mt 11:25-27; 13:16-17)
21 Ndipo Yesu akajisikia furaha kwa uweza wa Roho Mtakatifu, akasema, “Ninakusifu wewe, Baba, BWANA wa mbingu na nchi. Ninashukuru kwamba umewaficha mambo haya wenye hekima na akili nyingi. Lakini umeyafunua kwa watu walio kama watoto wadogo. Ndiyo, Baba, umefanya hivi kwa sababu hakika ndivyo ulitaka kufanya.
22 Baba yangu amenipa vitu vyote. Hakuna anayejua Mwana ni nani, Baba peke yake ndiye anayejua. Na Mwana peke yake ndiye anayejua Baba ni nani. Watu pekee watakaojua kuhusu Baba ni wale ambao Mwana amechagua kuwaambia.”
23 Wafuasi walikuwa na Yesu peke yao na Yesu aliwageukia akasema, “Ni baraka kubwa kwenu kuyaona mnayoyaona sasa! 24 Ninawaambia, Manabii wengi na wafalme walitamani kuyaona mambo haya mnayoyaona ninyi, lakini hawakuyaona, na walitamani kuyasikia mnayoyasikia ninyi lakini hawakuweza.”
Simulizi Kuhusu Msamaria Mwema
25 Kisha mwanasheria mmoja alisimama ili amjaribu Yesu. Akasema, “Mwalimu, ninatakiwa nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?”
26 Yesu akamwambia, “Imeandikwa nini katika torati? Unaielewaje?”
27 Yule mwana sheria akajibu, “‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote.’(A) Pia ‘Mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe.’”(B)
28 Yesu akasema, “Jibu lako ni sahihi. Fanya hivi nawe utaupata uzima wa milele.”
29 Lakini mwanasheria alitaka kuonesha kuwa alikuwa mwenye haki na aliishi kwa usahihi. Hivyo akamwuliza Yesu, “Lakini si kila mtu aliye jirani yangu, au unasemaje?”
30 Katika kujibu swali hili, Yesu akasema, “Mtu mmoja alikuwa anasafiri kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko. Akiwa njiani alivamiwa na majambazi, wakamchania nguo na kumpiga. Kisha wakamwacha amelala chini akiwa katika hali ya kufa.
31 Ikatokea kuwa kuhani mmoja alikuwa anasafiri kupitia njia hiyo hiyo. Alipomwona, hakusimama ili amsaidie, alikwenda zake. 32 Kisha Mlawi[e] alipokaribia na kumwona yule mtu, alipita upande mwingine. Hakusimama ili amsaidie, Alikwenda zake.
33 Ndipo Msamaria[f] mmoja aliyekuwa anasafiri kupitia njia ile ile, alipofika mahali ambapo mtu aliyejeruhiwa alikuwa amelala, alipomwona alimhurumia. 34 Alimkaribia ili amsaidie, akamsafisha majeraha kwa mafuta ya zeituni na divai,[g] kisha akayafunga majeraha yake. Msamaria alikuwa na punda. Akampandisha juu ya punda wake na kumpeleka mpaka kwenye nyumba ya wageni. Akamhudumia huko. 35 Siku iliyofuata, Msamaria alitoa sarafu mbili za fedha na kumpa mtunza nyumba ya wageni, akamwambia, ‘Mtunze mtu huyu aliyejeruhiwa. Ukitumia pesa nyingi zaidi kwa kumhudumia, nitakulipa nitakapokuja tena.’”
36 Kisha Yesu akasema, “Ni yupi kati ya hawa watu watatu unadhani hakika alikuwa jirani wa yule mtu aliyepigwa na majambazi?”
37 Mwanasheria akajibu, “Ni yule aliyemsaidia.”
Yesu akasema, “Basi nenda ukafanye kama alivyofanya.”
Maria na Martha
38 Yesu na wafuasi wake walipokuwa wanasafiri, walifika katika kijiji kimoja. Mwanamke aitwaye Martha alimkaribisha nyumbani kwake. 39 Alikuwa na mdogo wake aliyeitwa Mariamu. Mariamu alikuwa amekaa karibu na Yesu akimsikiliza anavyofundisha. 40 Lakini Martha dada yake Mariamu alikuwa anashughulisha na shughuli mbalimbali zilizotakiwa kufanywa. Martha aliingia ndani na akasema, “Bwana, hujali kuona mdogo wangu ameniacha nifanye kazi zote peke yangu? Mwambie aje kunisaidia.”
41 Lakini Bwana akamjibu, “Martha, Martha, unasumbuka na kuhangaika kwa shughuli nyingi. 42 Lakini kitu kimoja tu ndicho cha lazima. Mariamu amefanya uchaguzi sahihi na kamwe hautachukuliwa kutoka kwake.”
Yesu Afundisha Kuhusu Maombi
(Mt 6:9-15)
11 Siku moja Yesu alitoka akaenda mahali fulani kuomba. Alipomaliza, mmoja wa wafuasi wake akamwambia, “Yohana aliwafundisha wafuasi wake namna ya kuomba. Bwana, tufundishe nasi pia.”
2 Yesu akawaambia wafuasi wake, “Hivi ndivyo mnapaswa kuomba:
‘Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe daima.
Tunaomba Ufalme wako uje.
3 Utupe chakula tunachohitaji kila siku.
4 Utusamehe dhambi zetu,
kama tunavyomsamehe kila mtu anayetukosea.
Na usiruhusu tukajaribiwa.’”
Mwombeni Mungu Kile Mnachohitaji
(Mt 7:7-11)
5-6 Kisha Yesu akawaambia, “Chukulia mmoja wenu angekwenda kwa rafiki yake usiku na kumwambia, ‘Rafiki yangu aliyekuja mjini amekuja kunitembelea. Lakini sina chakula cha kumpa ili ale. Tafadhali nipe mikate mitatu.’ 7 Rafiki yako ndani ya nyumba akajibu, ‘Nenda zako! Usinisumbue! Mlango umefungwa. Mimi na watoto wangu tumeshapanda kitandani kulala. Siwezi kuamka ili nikupe kitu chochote kwa sasa.’ 8 Ninawaambia, urafiki unaweza usimfanye aamke akupe kitu chochote. Lakini hakika ataamka ili akupe unachohitaji ikiwa utaendelea kumwomba. 9 Hivyo ninawaambia, Endeleeni kuomba na Mungu atawapa. Endeleeni kutafuta na mtapata. Endeleeni kubisha milangoni, na milango itafunguliwa kwa ajili yenu. 10 Ndiyo, kila atakayeendelea kuomba atapokea. Kila atakayeendelea kutafuta atapata. Na kila atakayeendelea kubisha mlangoni, mlango utafunguliwa kwa ajili yake. 11 Je, kuna mmoja wenu aliye na mwana? Utafanya nini ikiwa mwanao atakuomba samaki? Je, kuna baba yeyote anayeweza kumpa nyoka? 12 Au akiomba yai, utampa nge? Hakika hakuna baba wa namna hivyo. 13 Ikiwa ninyi waovu mnajua namna ya kuwapa watoto wenu vitu vizuri. Vivyo hivo, hakika Baba yenu aliye mbinguni anajua namna ya kuwapa Roho Mtakatifu wale wanao mwomba?”
Nguvu ya Yesu Inatoka kwa Mungu
(Mt 12:22-30; Mk 3:20-27)
14 Wakati mmoja Yesu alikuwa akitoa pepo aliyemfanya mtu ashindwe kuzungumza. Ikawa, pepo alipotoka, yule mtu akaanza kuongea, umati wa watu walishangaa. 15 Lakini baadhi ya watu walisema, “Anatumia nguvu za Shetani kuwatoa pepo. Shetani[h] ni mtawala wa pepo wachafu.”
16 Baadhi ya watu wengine waliokuwa pale walitaka kumjaribu Yesu, walimwomba afanye muujiza kama ishara kutoka kwa Mungu. 17 Lakini alijua walichokuwa wanafikiria, hivyo akawaambia, “Kila ufalme unaopigana wenyewe huteketezwa; na familia yenye magomvi husambaratika. 18 Hivyo, ikiwa Shetani anapigana yeye mwenyewe, ufalme wake utasimamaje? Ninawauliza hivi kwa kuwa mnasema kwamba ninatoa pepo kwa kutumia nguvu za Shetani. 19 Lakini ikiwa ninatoa pepo kwa kutumia nguvu za Shetani, watu wenu wanatumia nguvu gani wanapotoa pepo? Hivyo watu wenu wenyewe watathibitisha kuwa ninyi ni waovu. 20 Lakini, ninatumia nguvu za Mungu kutoa pepo. Hii inaonesha kuwa Ufalme wa Mungu umekuja kwenu sasa.
21 Mwenye nguvu aliye na silaha nyingi anapoilinda nyumba yake, vitu vilivyomo ndani ya nyumba yake huwa salama. 22 Lakini chukulia kuwa mwenye nguvu zaidi kuliko yeye akimshambulia na kumshinda, yule mwenye nguvu zaidi humnyang'anya silaha zake zote alizokuwa akizitegemea kuilinda nyumba yake. Ndipo mwenye nguvu zaidi atavitumia vitu vya yule mtu wa kwanza kadri anavyotaka.
23 Mtu yeyote asiye pamoja nami, yuko kinyume nami. Na mtu yeyote asiyefanya kazi pamoja nami anafanya kinyume nami.
Hatari ya Kuwa Mtupu
(Mt 12:43-45)
24 Mtu anapotokwa na roho chafu, roho hiyo husafiri sehemu zilizo kavu, ikitafuta mahali ili ipumzike. Lakini hukosa mahali pa kupumzika. Hivyo husema, ‘Nitarudi kwenye nyumba nilikotoka.’ 25 Inaporudi hukuta nyumba imesafishwa na kupangwa vizuri. 26 Ndipo roho hiyo chafu huenda ikachukua roho wengine saba, walio waovu kuliko yenyewe. Na kwa pamoja roho zote hizo huingia na kuishi ndani ya mtu huyo, na mtu huyo hupata matatizo mengi kuliko ya kwanza.”
Watu Wanaobarikiwa na Mungu
27 Yesu alipokuwa akisema mambo haya, mwanamke mmoja katika kundi la watu akapaza sauti akamwambia “Amebarikiwa na Mungu mwanamke aliyekuzaa na kukunyonyesha!”
28 Lakini Yesu akasema, “Wamebarikiwa zaidi wanaosikia na kuyatii mafundisho ya Mungu.”
Baadhi ya Watu Wawa na Mashaka na Mamlaka ya Yesu
(Mt 12:38-42; Mk 8:12)
29 Baada ya kundi la watu kuongezeka na kumzunguka, Yesu alisema, “Ninyi watu mnaoishi sasa ni waovu. Mnaomba muujiza kama ishara kutoka kwa Mungu. Lakini hakuna muujiza utakaofanyika ili kuwathibitishia jambo lolote. Ishara pekee mtakayopata ni kile kilichompata Yona.[i] 30 Yona alikuwa ishara kwa watu walioishi katika mji wa Ninawi. Ni sawasawa na Mwana wa Adamu atakavyokuwa ishara kwa watu wa wakati huu.
31 Siku ya hukumu, ninyi watu mnaoishi sasa, mtalinganishwa na Malkia wa Kusini,[j] naye pia, atakuwa shahidi atakayeonyesha namna mlivyo waovu. Kwa nini ninasema haya? Kwa sababu alisafiri kutoka mbali, mbali sana ili ayasikilize mafundisho yenye hekima ya Suleimani. Na ninawaambia mkuu[k] kuliko Suleimani yupo hapa, lakini hamnisikilizi!
32 Siku ya hukumu, ninyi watu mnaoishi sasa mtafananishwa pia na watu wa Ninawi, nao watakuwa mashahidi watakaoonyesha makosa yenu. Ninasema hivi kwa sababu Yona alipowahubiri, walibadili mioyo na maisha yao. Na sasa mnamsikia mtu aliye mkuu kuliko Yona, Lakini hamtaki kubadilika!
Iweni Mwanga kwa Ajili ya Ulimwengu
(Mt 5:15; 6:22-23)
33 Hakuna mtu anayechukua taa na kuiweka mahali palipofichika au kuifunika. Badala yake huiweka mahali palipo wazi, ili wanaoingia ndani waweze kuiona nuru yake. 34 Namna unavyowatazama watu inaonesha kwa hakika jinsi ulivyo. Unapowatazama watu katika hali isiyo ya ubinafsi, inaonesha wazi kuwa umejaa nuru. Lakini unapowatazama watu katika namna ya uchoyo, ni wazi kuwa umejaa giza.[l] 35 Hivyo iweni waangalifu ili nuru iliyo ndani yenu usiwe giza! 36 Ikiwa umejaa nuru na hakuna sehemu yenye giza ndani yako, basi utang'aa, kama nuru ya kwenye taa.”
Yesu Awakosoa Viongozi wa Kidini
(Mt 23:1-36; Mk 12:38-40; Lk 20:45-47)
37 Baada ya Yesu kumaliza kuzungumza, Farisayo mmoja alimwalika Yesu kula pamoja naye. Hivyo Yesu alikwenda na kuketi sehemu ya kulia chakula. 38 Lakini Farisayo alishangaa alipoona Yesu hakunawa[m] mikono yake kwanza kabla ya kuanza kula. 39 Bwana akamwambia, “Usafi mnaoufanya ninyi Mafarisayo ni kama kusafisha kikombe au sahani kwa nje tu. Lakini ndani yenu mna nini? Mnataka kuwadanganya na kuwaumiza watu tu. 40 Ninyi ni wajinga! Aliyeumba kilicho nje ndiye aliumba kilicho ndani. 41 Hivyo, jalini vilivyo ndani. Wapeni vitu wenye uhitaji. Ndipo mtakuwa wasafi kikamilifu.
42 Lakini, ole wenu ninyi Mafarisayo! Mnampa Mungu sehemu ya kumi ya vyakula mnavyopata, hata mnanaa, na hata kila mmea mdogo katika bustani[n] zenu. Lakini mnapuuzia kuwatendea haki wengine na kumpenda Mungu. Haya ni mambo mnayotakiwa kufanya. Na endeleeni kufanya mambo hayo mengine.
43 Ole wenu ninyi Mafarisayo, kwa sababu mnapenda kupata viti vya heshima katika masinagogi. Na mnapenda kusalimiwa na watu kwa kuheshimiwa sehemu za masoko. 44 Ole wenu, kwa kuwa mnafanana na makaburi ya zamani yasiyoonekana, ambayo watu hupita juu yake na kuyakanyaga bila kuyatambua.”
45 Mmoja wa wanasheria akamwambia Yesu, “Mwalimu, unaposema mambo haya kuhusu Mafarisayo unatukosoa hata sisi pia.”
46 Yesu akamjibu, “Ole wenu, enyi wanasheria! Mnatunga sheria kali ambazo ni vigumu watu kuzitii.[o] Mnawalazimisha wengine kuzitii sheria zenu. Lakini ninyi wenyewe hamthubutu hata kujaribu kufuata mojawapo ya sheria hizo. 47 Ole wenu kwa kuwa mnajenga makaburi ya manabii. Lakini hawa ni manabii wale wale ambao mababu zenu waliwaua. 48 Na sasa mnawaonesha watu wote kwamba mnakubaliana na mambo ambayo baba zenu walifanya. Waliwaua manabii, nanyi mnasherehekea mauaji hayo kwa kujenga makaburi ya manabii! 49 Hii ndiyo sababu ambayo kwa Hekima yake Mungu alisema, ‘Nitawatuma manabii na mitume[p] kwao. Baadhi ya manabii na mitume wangu watauawa na watu waovu. Wengine watateswa sana.’
50 Hivyo ninyi watu mnaoishi sasa mtaadhibiwa kwa sababu ya vifo vya manabii wote waliouawa tangu mwanzo wa ulimwengu. 51 Mtachukuliwa wenye hatia kutokana na vifo hivyo vyote, tangu kuuawa kwa Habili mpaka kuuawa kwa nabii Zakaria,[q] aliyeuawa kati ya madhabahu na Hekalu. Ndiyo ninawaambia, kizazi hiki kitaadhibiwa kwa sababu yao wote.
52 Ole wenu, ninyi wanasheria, mmechukua ufunguo wa kujifunza kuhusu Mungu. Ninyi wenyewe hamtaki kujifunza na mmewazuia wengine wasijifunze pia.”
53 Yesu alipotoka humo, walimu wa sheria na Mafarisayo walianza kumpinga sana. Walianza kumjaribu ili awajibu maswali kuhusu mambo mengi, 54 ili Yesu akisema jambo isivyo sahihi waweze kupata sababu ya kumkosoa.
© 2017 Bible League International