Book of Common Prayer
15 Hivyo Kristo huwaletea watu wake agano jipya kutoka kwa Mungu. Huleta agano hili ili wale walioteuliwa na Mungu waweze kuzipata baraka ambazo Mungu aliwaahidi, baraka zinazodumu milele. Hili laweza kutokea tu kwa sababu Kristo alikufa ili awaweke huru watu kutokana na dhambi zilizotendwa dhidi ya amri za agano la kwanza.
16 Mtu anapofariki na akaacha usia, ni lazima uwepo uthibitisho kwamba yule aliyeandika usia amefariki. 17 Usia haumaanishi chochote wakati aliyeuandika bado yuko hai. Unaweza kutumika mara tu baada ya kifo cha mtu huyo. 18 Ndiyo sababu ili kuthibitisha kifo damu ilihitajika ili kuanza agano la kwanza baina ya Mungu na watu wake. 19 Kwanza, Musa aliwaeleza watu kila agizo katika sheria. Kisha akachukua damu ya ndama dume[a] na kuichanganya na maji. Alitumia sufu nyekundu na tawi la hisopo kunyunyiza damu na maji katika kitabu cha sheria na kwa watu. 20 Kisha akasema, “Hii ni damu inayoweka agano liwe zuri agano ambalo Mungu aliwaagiza mlifuate.”(A) 21 Kwa jinsi hiyo hiyo, Musa alinyunyiza damu katika Hema Takatifu. Aliinyunyiza damu juu ya kila kitu kilichotumika katika ibada. 22 Sheria inasema kwamba karibu kila kitu kinapaswa kutakaswa kwa damu. Dhambi haziwezi kusamehewa bila sadaka ya damu.
Yesu Kristo ni Dhabihu yetu kwa Ajili ya Dhambi
23 Mambo haya ni nakala ya mambo halisi yaliyoko mbinguni. Nakala hizi zinapaswa kutakaswa kwa sadaka ya wanyama. Lakini mambo halisi yaliyoko mbinguni yanapaswa kuwa na sadaka zilizo bora zaidi. 24 Kristo alienda katika Patakatifu pa Patakatifu. Lakini hapakuwa mahali palipotengenezwa na mwanadamu, ambapo ni nakala tu ya ile iliyo halisi. Alienda katika mbingu, na yuko huko sasa mbele za Mungu ili atusaidie sisi.
25 Kuhani mkuu huingia katika Patakatifu pa Patakatifu mara moja tu kila mwaka. Huchukua pamoja naye damu ya sadaka. Lakini hatoi damu yake kama alivyofanya Kristo. Kristo alienda mbinguni, lakini siyo kujitoa mwenyewe mara nyingi kama ambavyo kuhani mkuu hutoa damu tena na tena. 26 Kama Kristo alijitoa mwenyewe mara nyingi, basi angehitaji kuteseka mara nyingi tangu wakati dunia ilipoumbwa. Lakini alikuja kujitoa mwenyewe mara moja tu. Na mara hiyo moja inatosha kwa nyakati zote. Alikuja katika wakati ambao ulimwengu unakaribia mwisho. Alikuja kuchukua dhambi zote kwa kujitoa mwenyewe kama sadaka.
27 Kila mtu atakufa mara moja tu. Baada ya hapo ni kuhukumiwa. 28 Hivyo Kristo alitolewa kama sadaka mara moja kuchukua dhambi za watu wengi. Na atakuja mara ya pili, lakini siyo kujitoa mwenyewe kwa ajili ya dhambi. Atakuja mara ya pili kuleta wokovu kwa wale wanaomngojea.
Yesu Anayo Mamlaka ya Mungu
19 Lakini Yesu akajibu, “Hakika nawaambieni kuwa Mwana hawezi kufanya chochote peke yake. Bali hufanya tu yale anayoona Baba yake anayafanya. Kwa maana Mwana hufanya mambo ambayo Baba huyafanya. 20 Baba anampenda Mwana na humwonesha kila kitu anachofanya. Pia Baba atamwonesha Mwana mambo makuu ya kufanya kuliko hili. Kisha nyote mtashangazwa. 21 Baba huwafufua wafu na kuwapa uzima. Kwa njia hiyo hiyo, Mwana pia huwapa uzima wale anaowataka.”
22 “Vile vile, Baba hamhukumu mtu. Bali amempa Mwana nguvu ya kufanya hukumu zote. 23 Mungu alifanya hivi ili watu wote waweze kumheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Mtu yeyote asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba. Kwani Baba ndiye aliyemtuma Mwana.
24 Kwa hakika nawaambia, yeyote anayesikia ninayosema na kumwamini yule aliyenituma anao uzima wa milele. Hawa hawatahukumiwa kuwa na hatia. Kwani tayari wameshaivuka mauti na kuingia ndani ya uzima. 25 Mniamini, wakati muhimu sana unakuja. Wakati huo tayari upo ambapo watu waliokufa wataisikia sauti ya Mwana wa Mungu. Na hao watakaoisikia watafufuka na kuwa hai. 26 Uzima huja kutoka kwa Baba mwenyewe. Na pia Baba amemruhusu Mwana kutoa uzima. 27 Na Baba amempa Mwana mamlaka ya kuwahukumu watu wote kwa sababu yeye ndiye Mwana wa Adamu.
28 Ninyi msishangazwe na hili. Wakati unakuja ambapo watu wote waliokufa na kuwamo makaburini mwao wataisikia sauti yake. 29 Kisha watatoka nje ya makaburi yao. Wale waliotenda mema watafufuka na kupata uzima wa milele. Lakini wale waliotenda maovu watafufuka na kuhukumiwa kwa kuwa na hatia.
© 2017 Bible League International