Book of Common Prayer
4 Na bado tunayo ahadi ambayo Mungu aliwapa watu wake. Ahadi hiyo ni kwamba tuweze kuingia katika sehemu ya pumziko. Hivyo tunapaswa kuwa waangalifu ili asiwepo atakayeikosa ahadi hiyo. 2 Ndiyo, habari njema kuhusu hilo zilielezwa kwetu kama ilivyokuwa kwao. Lakini ujumbe waliousikia haukuwasaidia. Waliusikia lakini hawakuupokea kwa imani. 3 Ni sisi tu tunaoamini tunaoweza kuingia katika sehemu ya pumziko ya Mungu. Kama Mungu alivyosema:
“Nilikasirika na nikaweka ahadi:
‘Hawataingia kamwe kwenye sehemu yangu ya pumziko.’”(A)
Lakini kazi ya Mungu ilikamilika tangu wakati ule alipoumba ulimwengu. 4 Ndiyo, mahali fulani katika Maandiko alizungumza juu ya siku ya saba ya juma. Alisema, “Hivyo katika siku ya saba, Mungu alipumzika kazi zake zote.”(B) 5 Lakini katika Maandiko ya hapo juu Mungu alisema, “Hawataingia kamwe katika sehemu yangu ya pumziko.”
6 Hivyo fursa bado ipo kwa baadhi kuingia na kufurahia pumziko la Mungu. Lakini waliosikia kwanza habari njema juu yake hawakuweza kuingia, kwa sababu hawakutii. 7 Hivyo Mungu akapanga siku nyingine maalumu. Inaitwa “leo.” Alizungumza juu ya siku hiyo kupitia kwa Daudi siku nyingi zilizopita kutumia maneno tuliyonukuu mwanzoni:
“Kama leo mtaisikia sauti ya Mungu,
msiifanye migumu mioyo yenu.”(C)
8 Tunajua kuwa Yoshua hakuwaongoza watu hadi sehemu ya pumziko ambayo Mungu aliwaahidi. Tunalijua hili kwa sababu Mungu alisema baadaye kuhusu siku ya pumziko. 9 Hii inaonesha kuwa pumziko la siku ya saba[a] kwa watu wa Mungu bado linakuja. 10 Mungu alipumzika alipokamilisha kazi yake. Hivyo kila mmoja anayeingia katika sehemu ya pumziko ya Mungu vilevile atapata pumziko kutoka katika kazi yake kama Mungu alivyofanya. 11 Hivyo hebu na tujitahidi tuwezavyo kuingia katika sehemu ya pumziko ya Mungu. Tunapaswa kujitahidi ili asiwepo miongoni mwetu atakayepotea kwa kufuata mfano wa wale waliokataa kumtii Mungu.
12 Neno la Mungu[b] liko hai na linatenda kazi. Lina ukali kupita upanga ulio na makali sana na hukata hadi ndani yetu. Hukata ndani hadi sehemu ambayo nafsi na roho huwa zimeunganishwa pamoja. Neno la Mungu hukata hadi katikati ya maungio na mifupa yetu. Linahukumu mawazo na hisia ndani ya mioyo yetu. 13 Hakuna chochote ulimwenguni mwote kinachoweza kufichika mbele za Mungu. Anaweza kuviona vitu vyote kwa uwazi kabisa. Kila kitu kiko wazi mbele zake. Na kwake tutapaswa kujieleza jinsi tulivyoishi.
Yesu Asafisha Eneo la Hekalu
(Mt 21:12-13; Mk 11:15-17; Lk 19:45-46)
13 Kipindi hicho wakati wa kusherehekea Pasaka ya Wayahudi ulikaribia, hivyo ikampasa Yesu kwenda Yerusalemu. 14 Katika eneo la Hekalu aliwaona watu wakiuza ng'ombe, mbuzi na njiwa. Aliwaona wengine wakikalia meza na kufanya biashara ya kubadili fedha za watu. 15 Yesu akatengeneza kiboko kwa kutumia vipande vya kamba. Kisha akawafukuza watu wote, kondoo na ng'ombe watoke katika eneo la Hekalu. Akazipindua meza za wafanya biashara wa kubadilisha fedha na kuzitawanya fedha zao. 16 Baada ya hapo akawaambia wale waliokuwa wanauza njiwa, “Viondoeni humu vitu hivi! Msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa mahali pa kununua na kuuza!”
17 Haya yaliwafanya wafuasi wake kukumbuka maneno yaliyoandikwa kwenye Maandiko: “Upendo wangu mkuu kwa Hekalu lako utaniangamiza.”(A)
18 Baadhi ya Wayahudi wakamwambia Yesu, “Tuoneshe muujiza mmoja kama ishara kutoka kwa Mungu. Thibitisha kwamba unayo haki ya kufanya mambo haya.”
19 Yesu akajibu, “Bomoeni hekalu hili nami nitalijenga tena kwa muda wa siku tatu.” 20 Wakajibu, “Watu walifanya kazi kwa miaka 46 kulijenga Hekalu hili! Je, ni kweli unaamini kwamba unaweza kulijenga tena kwa siku tatu?”
21 Lakini Yesu aliposema “hekalu hili”, alikuwa anazungumzia mwili wake. 22 Baada ya kufufuliwa kutoka katika wafu, wafuasi wake wakakumbuka kwamba alikuwa ameyasema hayo. Hivyo wakayaamini Maandiko, na pia wakayaamini yale aliyoyasema Yesu.
© 2017 Bible League International