Book of Common Prayer
18 Ninyi ni watu wa Mungu, kama watu wa Israeli walipofika katika Mlima Sinai. Lakini hamjaufikia mlima halisi wa kuweza kushikwa. Mlima huo haupo kama ule waliouona, uliokuwa ukiwaka moto na kufunikwa na giza, utusitusi na dhoruba. 19 Haipo sauti ya tarumbeta au sauti iliyoyasema maneno kama hayo waliyoyasikia. Walipoisikia sauti, wakasihi kamwe wasisikie neno lingine. 20 Hawakutaka kusikia amri: “Kama chochote, hata mnyama, akigusa mlima, lazima kiuawe kwa kupigwa mawe.”(A) 21 Kile walichoona kilikuwa cha kutisha kiasi kwamba Musa akasema, “Natetemeka kwa hofu.”(B)[a]
22 Lakini mmeufikia Mlima Sayuni, kwenye mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa mbinguni.[b] Mmefika mahali ambapo maelfu wa malaika wamekusanyika kusherehekea. 23 Mmefika katika kusanyiko la watoto wazaliwa wa kwanza wa Mungu. Majina yao yameandikwa mbinguni. Mmemfikia Mungu, hakimu wa watu wote. Na mmefika kwenye roho za watu wema ambao wamekamilishwa. 24 Mmemfikia Yesu; yeye aliyelileta kutoka kwa Mungu agano jipya kwenda kwa watu wake. Mmefika kwenye damu iliyonyunyizwa[c] ambayo inasema habari za mema zaidi kuliko damu ya Habili.
25 Muwe makini na msijaribu kupuuza kusikiliza Mungu anaposema. Watu wale walipuuza kumsikiliza yeye alipowaonya hapa duniani. Nao hawakuponyoka. Sasa Mungu anasema kutoka mbinguni. Hivyo sasa itakuwa vibaya zaidi kwa wale watakaopuuza kumsikiliza yeye. 26 Alipozungumza pale mwanzoni, sauti yake iliitetemesha dunia. Lakini sasa ameahidi, “Kwa mara nyingine tena nitaitetemesha dunia, lakini pia nitazitetemesha mbingu.”(C) 27 Maneno “Kwa mara nyingine” yanatuonyesha kwa uwazi kwamba kila kitu kilichoumbwa kitaangamizwa; yaani, vitu vinavyoweza kutetemeshwa. Na ni kile tu kisichoweza kutetemeshwa kitakachobaki.
28 Hivyo tunahitajika kuwa na shukrani kwa sababu tunao ufalme ambao hauwezi kutetemeshwa. Na kwa sababu sisi ni watu wa shukrani, tunahitajika kumwabudu Mungu kwa njia itakayompendeza yeye. Tunahitajika kufanya hivi kwa heshima na hofu, 29 kwa sababu “Mungu wetu yuko kama moto unaoweza kutuangamiza sisi.”(D)
Yesu na Yohana Mbatizaji
22 Baada ya hayo, Yesu na wafuasi wake wakaenda katika eneo la Uyahudi. Kule Yesu alikaa pamoja na wafuasi wake na kuwabatiza watu. 23 Yohana naye alikuwa akiwabatiza watu kule Ainoni, eneo karibu na Salemu mahali palipokuwa na maji mengi. Huko ndiko watu walipoenda kubatizwa. 24 Hii ilikuwa kabla ya Yohana kufungwa gerezani.
25 Baadhi ya wafuasi wa Yohana walikuwa na mabishano pamoja na Myahudi mwingine juu ya utakatifu.[a] 26 Ndipo wakaja kwa Yohana na kusema, “Mwalimu, unamkumbuka mtu aliyekuwa pamoja nawe ng'ambo ya Mto Yordani? Yule uliyekuwa ukimwambia kila mtu juu yake.” Huyo pia anawabatiza watu na wengi wanaenda kwake.
27 Yohana akajibu, “Mtu anaweza tu kuyapokea yale ambayo Mungu anayatoa. 28 Ninyi wenyewe mlinisikia nikisema, ‘Mimi siye Masihi. Mimi ni mtu yule aliyetumwa na Mungu kutengeneza njia kwa ajili ya Masihi.’ 29 Bibi arusi siku zote yupo kwa ajili ya bwana arusi. Rafiki anayemsindikiza bwana arusi yeye hungoja na kusikiliza tu na hufurahi anapomsikia bwana arusi akiongea. Hivyo ndivyo ninavyojisikia sasa. Ninayo furaha sana kwani Masihi yuko hapa. 30 Yeye anapaswa kuwa juu zaidi yangu mimi, na mimi napaswa kuwa chini yake kabisa.”
© 2017 Bible League International